Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akizungumza na Bodi na
Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati alipotembelea
makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti
wa Bodi hiyo Dkt. Buruhani Nyenzi na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
mamlaka hiyo Dkt. Hamza Kabelwa
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akiangalia picha za
usafiri wa anga na majini ambazo usafiri wake unategemea utabiri wa hali
ya hewa wakati alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akipatiwa
taarifa ya hali ya hewa kwa usafiri wa anga na Meneja wa Utabiri wa Hali
ya Hewa Bwana Samwel Mbuya wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati
alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akiangalia picha ya ujenzi
wa barabara ya mabasi ya mwendokasi ambapo ujenzi wa miundombinu ya
barabara, reli unategemea utabiri wa hali ya hewa wakati alipotembelea
makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akiangalia picha ya rada
ya hali ya hewa iliyopo kwenye vituo vya utabiri wa hali ya hewa wakati
alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jijini
Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akipatiwa maelezo na
msomaji wa taarifa ya hali ya hewa kwenye vituo mbalimbali vya
televisheni Bi. Hellen Msemo kuhusu namna wanavyotoa taarifa za utabiri
wa hali ya hewa wakati alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam
……………………
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye ameilekeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
kujitangaza umuhimu wake katika nyanja ya kiuchumi na kijamii kwa
wananchi na taifa kwa
ujumla. Mhandisi Nditiye ameyasema hayo
alipotembelea makao makuu ya TMA na kuzungumza na bodi ya Mamlaka hiyo,
menejimenti na wafanyakazi kwa lengo la kutambua majukumu yao na
kufuatilia utekelezaji wake ili kufikia malengo ya Serikali ya
kuwatumikia wananchi.
Akizungumza na Bodi, menejimenti
na wafanyakazi, Mhandisi Nditiye amewaeleza kuwa TMA ni chombo muhimu
sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa letu na wananchi kwa
ujumla kwa kuwa sekta ya usafiri wa anga, majini, ujenzi wa majengo
mbalimbali, miundombinu ya barabara na reli, afya, kilimo na mazingira
vyote vinategemea taarifa za hali ya hewa kutoka kwenye Mamlaka hii.
“Mtambue kuwa hakuna ndege inayoweza kutua wala kuruka bila kupata
taarifa kutoka kwenu, vile vile mkandarasi anayejenga reli ya kisasa ya
SGR nae anategemea taarifa zenu kwa kiasi kikubwa, hivyo mtambue ninyi
ni muhimu na mjitangaze,” amesema Mhandisi Nditiye.
Amesisitiza kuwa ni vema
mjitangaze ili wananchi na wadau mbalimbali wafahamu majukumu na umuhimu
wa taasisi yenu kwa kuwa uchumi wa taifa hili unategemea taarifa zenu
ambapo wananchi wengi wamezoea kusikia na kuwaona mkitoa taarifa za
tahadhari za hali ya hewa zinazohusiana na majanga na matukio mengine
yanayohusiana na utabiri wenu angali ninyi mna taarifa muhimu zaidi na
tofauti na mtazamo wa wananchi walio wengi.
Amefafanua kuwa wananchi
wanaziamini taarifa zenu za hali ya hewa kwa kuwa kwa kiasi kikubwa yale
mnayotabiri na kuwaeleza ndiyo yanayotokea iwe ni mvua kubwa, upepo
mkali au joto kali kama ilivyo sasa. “Nimetembea na kukagua mitambo,
vifaa vya kisasa na namna wanavyofanya kazi na nimebaini kuwa taarifa
zinazotolewa hapa zimekusanywa kutoka vituo mbali mbali vya hali ya hewa
nchini ambapo hapa makao makuu wataalamu wanazichakata, kusambaza kwa
wahusika na kuhifadhiwa, na zinaonesha kuwa ni taarifa za uhakika kwa
kiwango cha asilimia 87.5 ambapo imeongezeka kutoka asilimia 82.1 kwa
miaka mitatu iliyopita,” amesema Mhandisi Nditiye.
Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Dkt.
Buruhani Nyenzi wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye
amesema kuwa Mamlaka hii ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya taifa letu
na wananchi kwa ujumla kwa kuwa utoaji wa taarifa na huduma za hali ya
hewa nchini zimewezesha uokoaji wa maisha ya watu na mali zao; kuepuka
au kupunguza athari na hasara zinazosababishwa na matukio ya hali ya
hewa; kuongeza tija na mafanikio katika shughuli za kiuchumi kama vile
kilimo, ufugaji, uvuvi; kuwa na miundombinu imara kama vile barabara,
madaraja; kuongeza ufanisi katika sekta za usafiri na mawasiliano;
kuchangia katika sekta za ujenzi na uendeshaji wa viwanda nchini na
kukuza pato la taifa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA
Dkt. Hamza Kabelwa amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa wahitaji wa taarifa
za hali ya hewa kutoka kwa taasisi na wadau mbalimbali ambao wanahitaji
kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii wamekuwa wengi
na teknolojia ya utabiri wa hali ya hewa na utoaji wa taarifa zake
umebadilika ambapo inatulazimu kuhuisha Sheria Na. 6 ya Hali ya Hewa ya
Mwaka 1978 na kukamilisha Sera ya Taifa ya Hali ya Hewa ili ziweze
kwenda na wakati pamoja na kuboresha chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kwa
kuwa ndio chuo pekee nchini kinachotoa elimu ya awali na ya kati ya hali
ya hewa.
Ameongeza kuwa TMA imepatiwa cheti
cha ubora wa utoaji huduma na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) kwa
kutoa huduma kwa sekta ya anga nchini. Pia, inashirikiana na Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa
jangwa la Afrika (SADC), Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwa kubadilishana taarifa za hali
ya hewa, mabadiliko ya hali ya hewa yanayohitaji ushirikiano wa
kimataifa, na kuendeleza na kutunza mtandao wa vituo vya uangazi wa hali
ya hewa ili kukidhi makubaliano ya kimataifa ya kubadilishana taarifa
hizo.
Dkt. Nyenzi amemshukuru Mhandisi
Nditiye na kumueleza kuwa TMA inafarijika kusikia kuwa anafahamu kwa
undani umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa nchini, hivyo ni imani yake
kuwa ataisamimia vema ili ifikie malengo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment