WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mrajisi wa Ushirika Dkt. Titto Haule aangalie kwa umakini
utendaji na ufanisi wa chama cha Ushirika cha MAMCU na viongozi wote
ili kubaini kama wanakidhi makusudio yake
Amesema ikiwezekana chama hicho
kivunjwe ili waanzishe vyama kilele viwili vitakavyoweza kuhudumia
wakulima katika maeneo yao ili waweze kuongeza tija.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo leo
(Jumanne, Februari 27, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya
Chiungutwa wilayani Masasi.
Pia Waziri Mkuu amerudia kutoa
agizo hilo alipozungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Mji
wa Newala na Halmashauri ya wilaya ya Newala.
Amesema anapata mashaka kuhusu
uwezo wao wa kuwahudumia wakulima, hivyo ameagiza kuharakishwa kwa
utekelezaji wa agizo hilo ili kurahisisha utoaji wa huduma.
MAMCU inahudumia wakulima wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Manispaa ya Mtwara, Halmashauri ya
Nanyamba, Nanyumbu na Halmashauri ya wilaya ya Masasi.
Amesema kwa takwimu hizo haamini
kama chama hicho kina uwezo wa kuhudumia maeneo hayo, hivyo kusababisha
wakulima kutofikiwa kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewaagiza wakulima wa korosho wajiwekee akiba ya fedha ili ziweze
kuwasaidia katika ununuzi wa pembejeo.
Amesema kwa mwaka huu Serikali
haitogawa pembejeo ya salfa kwa sababu mwaka jana iligawa bure ili
kuwahamasisha wakulima kufufua zao hilo.
Kadhalika amewataka wakulima wa
korosho wapande miche mipya ya mikorosho na kuiondoa mikorosho ya zamani
iliyozeeka ili waweze kuzalisha mazao bora.
No comments:
Post a Comment