Pages

Friday, December 29, 2017

VIONGOZI WA AMCOS 10 WATIWE MBARONI KWA KUHUJUMU MINADA YA KOROSHO PWANI-RC NDIKILO


IMG_0823
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, ambae pia ni mkuu wa Mkoa huo, mhandisi Evarist Ndikilo ,akionyesha picha zinazoonyesha korosho zilizochanganywa mawe na mchanga ,na kusababisha kutia doa minada ya Korosho inayoendelea mkoani hapo ,wakati alipokuwa wilayani Mkuranga
IMG_0860
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, ambae pia ni mkuu wa Mkoa huo, mhandisi Evarist Ndikilo , akizungumza na baadhi ya wakulima wa korosho wakati alipotembelea ghala moja lililopo wilayani Mkuranga.
Picha na Mwamvua Mwinyi
…………..
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ameliagiza jeshi la polisi mkoani hapo ,kuwakamatana na kuwahoji viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS)kumi ,kutokana na kosa la kufanya udanganyifu wa ubora na uzito wa korosho ili kujipatia fedha .
Amesema kuna baadhi ya AMCOS zimehusika kuchakachua na kutelemsha ubora wa korosho pamoja na kuweka mawe na michanga kwenye magunia ya korosho zilizokuwa zinauzwa kwenye minada .
Aidha mhandisi Ndikilo ,amekemea maghala ya vichochoroni na majumbani ambayo yamejaa na kusababisha kuchafua na kuharibu minada inayofanyika mkoani Pwani.
Akizungumza wilayani Mkuranga ,wakati akizungumzia kero hiyo iliyojitokeza alieleza,viongozi wa AMCOS hizo wakiwemo wenyeviti wake ,makatibu,kalani na wenye ghala wakamatwe na kueleza kiini cha kutelemsha ubora.
Alisema lifunguliwe jalada la uchunguzi wahojiwe mazingira na kiini cha kubadili ubora kutoka kiwango kinachohitajika na kushusha kiwango cha chini.
Mhandisi Ndikilo, alisema biashara hiyo haitaki kwani imesababisha wakulima wa korosho kushindwa kulipwa fedha zao.
“Kuna hii Mchukwi A -Amcos Two ambayo imechakachua korosho kutoka grade 52 hadi 45.1 ,Misugusugu wameshusha kiwango na kufikia 43,Mchukwi A -Amcos One ,Kibaoni ,Ruaruke ,Mahege,Mlanzi na Tuamke hawa wote wamejipanga kabisa ,maana haiwezekani viwe vyama vya msingi kumi huu ni mpango ,haikubaliki ,jamani haikubaliki” alisisitiza .
Akitoa maagizo mengine manne ,mhandisi Ndikilo alitaka wanunuzi walioshinda mnada na kushindwa kuwalipa wakulima fedha zao wakamatwe .
“Wapo wanunuzi walioenda nje ya masharti ya mnada wanapaswa walipe fedha za wakulima ndani ya siku nne” alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo ambae pia ni mkuu wa Mkoa huo ,aliagiza pia makampuni yaliyoshinda na kutolipa wakulima yakamatwe ama yahakikishe yanalipa ndani ya siku moja.
Alisema, AMCOS ya Mkiu viongozi wake wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwa kuweka mawe na mchanga kwenye magunia na kuchanganya na korosho.
Alibainisha huo ni wizi,uhujumu uchumi na kuaibisha sifa ya nchi ya Tanzania nje ya nchi kwani magunia hayo yangefika India na nchi nyingine ingekuwa aibu na fedheha.
Mhandisi Ndikilo alisema kero hizo zilisababisha Mkoa kuchukua hatua ya kufanya uhakiki upya wa korosho ili kuaminika kwa wanunuzi ambao  baadhi yao waligomea kuingia kwenye soko la korosho mkoani humo .
“Amcos zote nazipa salamu zijiandae ,zile Amcos zinazong’ang’ania kutumia maghala ya vichochoroni ili kudhurumu wakulima ,;:”‘.   Watie akilini msimu ujao 2018/2019 hawatatumia maghala ya majumbani yatatumika maghala makubwa matatu likiwemo la Mkuranga, , Kibiti na Kwamfipa Kibaha.”
Alisema ghala la Mkuranga litakuwa na uwezo wa kubeba korosho tani 30,000 hivyo aliomba kuondoka katika maghala yasiyo na kichwa wala miguu.
Naibu waziri wa mifugo na uvuvi ambae pia ni mbunge wa jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega alisema watu wachache wenye uroho wa fedha na wasio waaminifu wanataka kuharibu biashara hiyo na kuumiza wakulima.
Alisema kuweka michanga na mawe kwenye korosho imerudisha nyuma minada inayoendelea .
Ulega alisema kuwepo kwa maghala makubwa itainua soko la korosho msimu ujao na kuondoa ubabaishaji wa maghala madogomadogo yanayoleta dosari .
Mbunge huyo ,aliupongeza uongozi huo wa Mkoa kuingilia kati na kuchukua hatua ili kukomesha wizi unaofanywa na baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika vinavyoondoa uaminifu .
Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya Mkuranga, Juma Abeid alisema mfumo wa stakabadhi ghalani unaharibiwa na baadhi ya watu na kusababisha wakulima kuona mfumo huo hauna manufaa kwao .
Alisema kuna ujanja mwingi kwenye kuchakachua ubora wa korosho ndio uliowafikisha walipofikia sasa .
Abeid alisema korosho zipo hadi kwenye nyumba za watu ,kuna maghala Mkuranga zaidi ya 60 ,hivyo ni lazima maghala makubwa yakawepo ili kuondokana na kero zinazojitokeza.
Licha ya minada hiyo ya korosho kuingia kizungumkuti lakini tayari zaidi ya tani 19,815 zimeuzwa na kuingiza kiasi cha sh.bilioni 39 huku wakulima wakulima wa korosho mkoani Pwani wakiwa bado wanadai zaidi ya bilioni tano .

No comments:

Post a Comment