Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Watanzania wanaosoma nchini China (TASAFIC) Bw.
Remidius Emmanuel akizungumza katika mkutano wa Jumuiya hiyo uliofanyika
mjini Wuhan, jimbo la Hubei hivi karibuni.
Balozi
wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki akihutubia katika mkutano
wa Shirikisho la Jumuiya ya Watanzania wanaosoma katika Taifa la
China(TASAFIC) uliofanyika mjini Wuhan, jimbo la Hubei hivi karibuni.
……………..
Na Happiness Shayo- China
Balozi wa Tanzania nchini
China Mhe Mbelwa Kairuki amewataka Watanzania wanaosoma katika Taifa
hilo kutumia fursa hiyo kuunga mkono juhudi za Tanzania kuelekea Uchumi
wa kati ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa
shirikisho la Jumuiya za Watanzania wanaosoma katika Taifa la
China(TASAFIC) uliofanyika hivi karibuni katika mji wa Wuhan, Jimbo la
Hubei.
Balozi Kairuki alisema kuwa
yapo maeneo kadhaa ambayo Watanzania hao wanaweza kutoa michango yao
katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwenye ujenzi wa
Viwanda ili sekta hiyo isaidie na kuleta tija katika ukuaji wa Uchumi.
Akizungumzia kuhusu sekta ya
Utalii, Balozi Kairuki aliitaja China kama soko jipya wanalopatikana
watalii na kwamba kwa mwaka 2016 ni Wachina Millioni 120 waliokwenda nje
ya nchi kutalii sawa na idadi ya watu wote wa nchi za
Tanzania,Kenya,Uganda,Burundi na Rwanda, idadi inayoonekana ni kubwa
sana,ambapo kwa mwaka huo huo ni watalii 30,000 walipokelewa Tanzania
kutoka China.
“Zipo hatua kadhaa ambazo sasa
zimechukuliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini China, hivi sasa
tunazungumza na kampuni kubwa inayomiliki mitandao ya kijamii hapa ya
China ya TENCENT ili tuweze kutumia mtandao wao wa QQ kurusha vivutio
vyetu vya utalii hapa China mubashara, lakini pia mwezi huu tulikuwa na
Mazungumzo na Serikali ya China kuwajulisha nia ya shirika letu la ndege
la Air Tanzania kuanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam
hadi Guangzhou. Matarajio yetu ni kuona kwamba ifikapo Mwezi Septemba
mwakani lengo hilo linatimia. Vilevile tumeanza kuzungumza na Mamlaka za
China kuangalia uwezekano wa mashirika ya ndege ya China kuifanya
Tanzania kuwa kitovu (HUB) ya safari zao Barani Afrika. Maana yake nini?
Ndege kadhaa za China zinazokwenda Afrika zitakuwa zitasimamna
(stopover) pale Dar es salaam au KIA au Mbeya (Songwe) kwa ajili ya
kujaza mafuta na kupata huduma nyinginezo. Alisema Balozi Kairuki.
Kwa upande wa Sekta ya Elimu
Balozi Kairuki amewataka Watanzania wanaosoma katika taifa hili
kuendelea kutafuta fursa za masomo hapa China kwa faida ya watanzania
wengine na kwamba China ina vyuo takribani 2000 hivyo jambo hili sio
jukumu la Ubalozi pekee, hususani maeneo yenye upungufu katika taifa
letu, huku akitoa kipaumbele kwenye kozi za Kilimo na Uhandisi ambazo
alizitaja kama nguzo muhimu katika Uchumi wa viwanda.
“Kilimo ni uti wa mgongo wa
taifa letu. Kilimo kimeajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wote
ambao wengi wao wapo vijijiji. tunahitaji kilimo kuzalisha malighafi za
viwandani na hatuwezi kutimiza malengo ya kujenga uchumi wa viwanda bila
kufanya maboresho makubwa ya sekta ya kilimo.Lakini pia tunaamini
kabisa Mtanzania anayekuja kusoma uhandisi hapa China mbali na elimu ya
darasani, atapata pia exposure kubwa ya kazi za uhandisi
zinazofanyika hapa China na tayari tumeanza kuzungumza na makampuni ya
ujenzi ya hapa China kuyaomba yatoe fursa kwa wanafunzi watanzania
kufanya elective programs ili mshiriki kwenye miradi mikubwa ya ujenzi.
Aidha , Balozi Kairuki aliwataka
Watanzania hao kutumia fursahizo kuvutia wawekezaji . “Tunahitaji
uwekezaji wa mitaji, teknolojia na ujuzi katika kuanzisha na kuendesha
viwanda nchini na kazi yetu kubwa ni kuendelea kuvutia uwekezaji wa
viwanda kutoka China sambamba na kutafuta teknolojia rahisi na nafuu
zinazoweza kupelekwa nyumbani kuwezesha watanzania kufanya shughuli za
uzalishaji. Hivi sasa uwekezaji nchini kutoka China unakadiriwa kufikia
dola za kimarekani Bilioni 3.7. Lengo letu ni kufikia Dola za Kimarekani
Bilioni 5 ifikapo mwaka 2020. Wanafunzi wanaosoma China ni muhimu
kuwatumia pia Wahadhiri katika vyuo vyao, ambao wengi wao wanayo
mahusiano na wa kichina ambao wana mitaji na wangependa kuwekeza barani
Afrika. Alisema Kairuki.
Akihitimisha hotuba yake
Balozi kairuki aliwataka Watanzania hao kuheshimu tamaduni na sheria
za taifa la China,Kila mmoja kutambua kusudi la uwepo wake hapa nchini
kuepuka maisha ya kifahari, Kuchukua tahadhari juu ya Madawa ya
Kulevya, kuepuka migomo kwa kuzingatia taratibu na sheria za vyuo
vyao,kutunza na kulinda Afya zao na kwa wanafunzi wa shahada za uzamili
na Uzamivu aliwataka kufanya Tafiti zenye tija kwa Taifa la
Tanzania.Ingawa pia alitumia nafasi hiyo kuwatambua Watanzania kadhaa
wanaosoma katika Taifa hilo kutambua michango wao mkubwa walioutoa kwa
manufaa ya Tanzania kupitia sekta ya Kilimo na Uhandisi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Shirikisho hilo Bw. Remidius Emmanuel alisema Mkutano huo ulilenga
kuwakutanisha Watanzania wote wanaosoma katika taifa la China kwa lengo
la kujadili masuala mbalimbali juu ya Elimu na changamoto mbalimbali
wanazokutana nazo lakini pia kutengeneza sauti ya pamoja na kuona namna
bora zaidi ya kutumia fursa hiyo ya uwepo wao katika taifa hilo kwa
manufaa ya Tanzania.
“Tunamshukuru sana Balozi wetu
Mhe. Mbelwa Kairuki wakati wote amekuwa karibu na sisi lakini kutumia
muda mwingi kuzifanya taaluma zetu katika matumizi mapana yanayolenga
kuendana na sera za nchi yetu hususani kipindi hiki ambacho taifa letu
liko kwenye kasi ya kuelekea uchumi wa kati.Kwa hiyo Madaktari,Wataalam
kilimo ,Wahandisi,Wachumi na wataalam wengine wote sasa wanaelekeza
taaluma zao kwa manufaa ya taifa letu” Alisema Remidius.
Mapema akisoma Taarifa ya
Mkutano huo Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Bw,Hussein Mtoro alisema
mbali na kuwaunganisha Watanzania kwa Umoja wao , Shirikisho hilo linalo
jukumu la kuhakikisha Watanzania wote wanaosoma katika taifa la China
wanatoa mawazo,fikra zao ,kwa kutumia taaluma na uzoefu wao kwa manufaa
ya Taifa la Tanzania.
“Shirikisho limeweza kuweka
mazingira mazuri kwa Watanzania wanaowasili China kwa mara ya kwanza
kila mwaka, tunaendelea kutatua changamoto kwa baadhi ya mawakala wasio
waaminifu ambao wamekuwa wakiwatelekeza na kuwalaghai wanafunzi
wapowaleta katika taifa hili, lakini tunajivunia kuwa na wataalamu
mbalimbali ambao kutoa michango wa moja kwa moja kwa taifa letu, Mfano
wataalam kutoka fani za Kilimo na uhandisi”.Alisema Bw. Hussein
Mkutano huo Ulihudhuriwa na
Watanzania wanaosoma katika Taifa la China na baadhi ya watumishi
kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini China.
No comments:
Post a Comment