Mratibu
wa Jinsia kutoka TACAIDS Jacob Kayombo na Afisa Jinsia kutoka TACAIDS
Judith Luande wakijadili baadhi ya maoni, maswali na mapendekezo ya
wajumbe ambao ni timu ya kudhibiti Ukimwi ya Mkoa wa Singida wakati wa
Mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia.
Mjumbe wa
mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia Afisa wa Serikali za
Mitaa Hussein Mwatawala akipitia fomu zitakazotumika katika kukusanya
taarifa za masuala ya Kijinsia mkoani Singida.
Serikali kupitia
Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imeandaa Mpango wa
uendeshaji wa Kijinsia kwa ajili ya mwitikio wa Masuala ya Ukimwi ambao
umetambulishwa rasmi kwa timu ya Kuthibiti Ukimwi Mkoani Singida.
Mratibu
wa Jinsia Kutoka TACAIDS Jacob Kayombo ameongoza mafunzo hayo kwa timu
ya kuthibiti Ukimwi Mkoa wa Singida ambapo amewaeleza kuwa mafunzo hayo
yatawasaidia kuratibu na kutoa dira katika utekelezaji wa program
mbalimbali za Ukimwi kwa ngazi ya Mkoa.
Kayombo amesema Mafunzo
hayo yamelenga kuutambulisha mpango huo pamoja na fomu zitakazotumika
katika ukusanyaji wa taarifa zihusuzo jinsia na Ukimwi.“Mafunzo haya
tunayotoa yamejikita katika kuufafanua mpango huu utakavyotumika pamoja
na namna ambavyo fomu hizi zitatumika kukusanya taarifa za jinsia na
Ukimwi kwa Mkoa wa Singida na jinsi ambavyo taarifa hizo zitasaidia
kufanya maamuzi sahihi kuhusu masuala ya Ukimwi”, amesema Kayombo.
Ameongeza
kuwa matarajio yanayotegemewa baada ya mafunzo hayo kutolewa ni kuona
masuala yote ya kijinsia yanapewa kipaumbele katika program mbalimbali
za Ukimwi.Kayombo amesisitiza kuwa mpango huu utakuwa ni mwongozo wa
wadau wa masuala ya Ukimwi ili waweze kutekeleza shughuli zao kwa
kuzingatia usawa wa kijinsia hasa katika kuweka mikakati ya kuthibiti
Ukimwi yenye uelekeo wa Usawa wa kijinsia.
Amebainisha kuwa
mpango huu ambao umedumu katika kipindi cha mwaka 2016 mpaka 2018 una
mwelekeo mpya wa program za ukimwi wenye kuzingatia masuala ya kijinsia
pamoja na kuondoa changamoto zitokanazo na mila na desturi potofu za
masuala ya kijinsia.
Naye Mjumbe wa mafunzo hayo Afisa wa
Serikali za Mitaa Hussein Mwatawala amesema mafunzo hayo yametoa mwanga
na mwelekeo utakawaosaidia katika kusimamia wadau wanaotekeleza
shughuliza Ukimwi ili wazingatie usawa wa kijinsia mkoani hapa.
Mwatawala
amesema maafisa waliopata mafunzo hayo wamepewa elimu ya kutosha juu ya
mpango na wameufahamu vema kazi iliyobaki ni kuhakikisha masuala ya
usawa ya kijinsia yanapewa kipaumbele katika kila program ya Ukimwi
inayotekelezwa na wadau mkoani hapa.Mpango wa uendeshaji wa masuala ya
Kijinsia 2016-2018 umeanzishwa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa wadau wa
masuala ya Ukimwi ili watekeleze program zao katika mtazamo wa usawa wa
kijinsia.
Mpango huu unashughulikia tofauti za kijinsia zikiwemo
ukatili wa kijinsia, unyanyapaa na ubaguzi ili kulinda haki za watu wote
wakiwemo wanaume,wanawake,wasichana na wavulana ili wapate huduma za
uzuiaji wa maambukizi ya VVU, tiba, matunzo na msaada.
Aidha
mpango huu unahusianishwa na Mkakati wa tatu wa taifa wa kuthibiti
Ukimwi 2013-2018 na Mkakati wa tatu wa kuthibiti VVU na Ukimwi wa Sekta
ya Afya 2013-2017 ambapo mikakati hiyo ina kanuni ambazo zinajumuisha
usawa wa kijinsia na ulinzi wa haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment