Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati), Balozi wa China nchini
Tanzania Bi. Wang Ke (wa pili kulia), Mwakilishi wa masuala ya Uchumi na
Biashara wa Ubalozi wa China Bw. Lin Zhiyong (wa pili kushoto) pamoja
na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika
picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya pande hizo
kuhusu Biashara, uwekezaji na ushirikiano, katika ukumbi wa Wizara ya
Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango (Kulia) na mgeni wake Bi. Wang Ke, wakitoka nje ya Jengo
la Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika
kwa mkutano kati yao uliohusu masuala mtambuka ya ushirikiano kati ya
Tanzania na China.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) na Balozi wa China nchini Tanzania
Bi. Wang Ke, wakiagana baada ya kumalizika kwa Mkutano kati yao
ambapo balozi huyo aliahidi kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii
na kiutamaduni kati nchi hizo mbili, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akiagana na Mwakilishi wa masuala
ya Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania Bw. Lin
Zhiyong baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya Waziri huyo na Balozi wa
nchi hiyo Bi. Wang Ke (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya
Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Kamishina wa Fedha za Nje Bw. John
Rubuga (kushoto) na Afisa anayeshughulikia masuala ya nje katika dawati
la China Bw. Alfonce Mayala kutoka Wizara ya Fedha na Mipango
wakifuatilia kwa makini majadiliano kati ya Balozi wa China nchini
Tanzania Bi. Wang Ke, na Waziri wa Fedha na Mipango (hawapo pichani),
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), wa pili kulia akieleza kuhusu fursa
zilizopo katika Sekta ya Utalii wakati wa Mkutano kati yake na Balozi
wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke, (hayupo pichani), Jijini Dar es
Salaam, kulia ni Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango,
Bw. John Rubuga.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), wa tatu kulia akiwa katika mkutano na
Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke (wa pili kushoto) ambapo
walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika Biashara na uwekezaji kwa
manufaa ya pande hizo mbili, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara
ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akieleza kuhusu kuwa na uwiano wa
kibiashara kati ya Tanzania na China kwa manufaa ya pande hizo mbili
wakati wa mkutano kati yake na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang
Ke, (hayupo pichani), Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa Nchini Bi.
Wang Ke, (katikati) akiongoza maafisa wake wa ubalozi wa nchi hiyo hapa
nchini wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa nchini, Bi.
Wang Ke, akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango
………………..
Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
BALOZI wa China hapa nchini, Wang
Ke, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kushawishi taasisi za
fedha ikiwemo Benki ya EXIM ya nchini humo kushiriki ujenzi wa reli ya
kati kwa kiwango cha kimataifa baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu
wa mradi huo.
Alisema kuwa kutokana na ukubwa wa
mradi huo, unaokadiriwa utagharimu Dola za Marekani bilioni 7.6 hadi
kukamilika kwake, utahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu ili kukidhi
masharti ya kupata mkopo kupitia Benki ya Exim na taasisi nyingine
zitakazotaka kujenga mradi huo muhimu.
“Mradi huu ni muhimu na wa
kihistoria kwa nchi hizi mbili, China ingependa kuona mradi huo
unaboreshwa ili uweze kutoa huduma ya kusafirisha mizigo na abiria na
kwamba kuimarika kwake kutaokoa miundombinu ya barabara kwa kuwa shehena
kubwa ya mizigo itasafirishwa kupitia reli hiyo.
Aidha, Balozi Ke alisema kuwa nchi
yake inasubiri pia kukamilika kwa taratibu za ndani kati yake na
Tanzania ili mradi wa reli ya TAZARA uanze ili kuboresha usafiri na
usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia pamoja na
nchi za maziwa makuu.
Balozi Ke alitumia fursa hiyo
kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa
kukusanya kodi, kusimamia matumizi adili ya fedha za umma, kupunguza
matumizi yasiyo ya lazima na kupambana na rushwa.
Akizungumza mara baada ya
mazungumzo na mgeni wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango
alisema kuwa Serikali imeridhia uamuzi wa China wa kufanya upembuzi
yakinifu wa mradi huo wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR)
ili China kupitia taasisi zake iweze kujenga sehemu ya mradi huo.
“Tayari mradi umeanza kujengwa
kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kwahiyo kujitokeza kwa China kutaka
kufadhili ujenzi wa mradi huo kutasaidia kukamilisha mradi huo muhimu
kwa haraka na kwa wakati” Alisema Dkt. Mpango.
Alisema pia kuwa China imeonesha
nia ya kusaidia kuujenga na kuupanga mji wa Dodoma kutokana na nchi hiyo
kuwa na uzoefu wa kupanga miji ambapo nchi hiyo imeonesha nia ya
kujenga miundombinu ya elimu, barabara, uwanja wa ndege wa
kimataifa-Msalato, kujenga mfumo wa maji safi na maji taka pamoja na
majengo ya kisasa.
Kuhusu biashara, Dkt. Mpango
alisema wamekubaliana kuwa China itaisaidia Tanzania kukuza kiwango cha
biashara ambapo takwimu zilizoko zinaonesha kuwa urari wa biashara kati
ya nchi hizo unaonesha kuwa Tanzania imekuwa ikinunua bidhaa nyingi
kutoka nchini humo kuliko inavyo uza bidhaa na huduma zake.
“Mwaka 2016 Tanzania iliuza China
bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za marekani milioni 460 wakati
China iliuza hapa nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani
bilioni 1.2, kiwango ambacho ni kikubwa karibu mara 5 ya kile
tulichowauzia” Alisema Dkt. Mpango.
Ili kuvutia Sekta ya utalii,
Tanzania imeiomba China kuanzisha safari ya ndege wa moja kwa moja
kutoka China hadi Tanzania ili kuvutia watalii wengi kutoka nchini humo
na kwamba utaratibu utafanyika ili Mamlaka ya usafiri wa anga iweze
iratibu na kusaini makubaliano ya ushirikiano na hivyo kufanikisha jambo
hilo.
“China imeandaa maonesho makubwa
ya uwekezaji na biashara ya bidhaa na huduma mbalimbali mwezi Novemba,
2018, hivyo wafanyabiashara wa Tanzania pamoja na Bodi ya Utalii nchini
wahakikishe wanashiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ili kutumia
nafasi hiyo kujitangaza” Alisistiza Dkt. Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango alieleza kuwa
Balozi Wang Ke, amesema kuwa Nchi yake itashiriki katika ujenzi wa
miradi ya bandari ili kukuza masuala ya usafiri kwa kuboresha bandari za
Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Bagamoyo, Dar es Salaam, Mtwara na katika Ziwa
Victoria na Ziwa Tanganyika.
Waziri huyo wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Mpango alitoa wito kwa wawekezaji kutoka China na nchi
nyingine kuja kuwekeza nchini katika kipindi hiki ambacho Tanzania
inaipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Miradi mikubwa ambayo China
imewekeza na kufadhili hadi sasa hapa nchini ni Reli ya TAZARA, Kiwanda
cha Urafiki, ujenzi wa barabara, majengo, ujenzi wa bomba la gesi kutoka
Mtwara hadi dar es Salaam, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere Jijini Dare Salaam, Ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na miradi mingine kadha wa kadha.
No comments:
Post a Comment