Serikali imesema itahakikisha
inaendelea kuwasimamia wakandarasi wa Ujenzi wa Barabara kuhakikisha
wanajenga barabara zote nchini kwa viwango vilivyokusudiwa na kumaliza
kwa wakati ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa
wananchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa leo jijini Dar
es salaam mara baada ya... kukagua Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Ujenzi
wa barabara za kupunguza msongamano jijini humo ambapo ameridhishwa na
kasi ya utekelezaji wake na kusisitiza kwa Wakala wa Baraba (TANROADS),
mkoa wa Dar es salaam kuwa wakali katika usimamizi ili kuhakikisha
barabara hizo zinajengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba.
“ Serikali imekuwa ikitumia Fedha
nyingi katika kutekeleza miradi hii, hivyo TANROADS hakikisheni
mnasimamia wakandarasi hawa kujenga barabara hizi kwa viwango na kwa
wakati”, amesema Waziri Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa amefafanua
kuwa utekelezaji wa awamu hiyo unaendelea vizuri ambapo unahusisha
barabara ya Kifuru – Msigani (km 4.5) ambayo kwa sasa imefika asilimia
87, Goba – Makongo (km 4.5), nayo imefikia asilimia 52 na Goba – Madale
(km 5) yenye asilimia 5.
Profesa Mbarawa ametoa wito kwa
wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi naTANROADS
mkoa wa Dar es salaam wakati mradi huo ukiendeleaa kutekelezwa ili
kusaidia kumaliza kwa wakati.
Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa
Serikali inaendelea kushughulikia suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi
wa maeneo hayo ambao wamepitiwa na mradi huo.
Kwa upande wake, Meneja wa
TANROADS mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Julius Ndyamkama,
amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa watasimamia mradi huo usiku na
mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyo
bora.
Mhandisi Ndyamkama amebainisha
changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa mradi huo ikiwemo suala
la ulipaji wa fidia kwa baadhi ya maeneo hasa katika kipande cha
barabara chenye urefu wa kilometa 1 kuanzia Mto Mbezi kuelekea Makongo.
Naye, Mratibu wa Mradi wa barabara
ya Goba – Madale (km 5), kutoka kampuni ya Ujenzi ya Mwananchi
Engineering and Contracting Co. Ltd (MECCO), Mhandisi Crispin Mwombeki,
amesema kuwa tayari wameshakamilisha usanifu wa mradi na wanategemea
kuanza kazi za Ujenzi hivi karibuni.
Utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya
mradi wa Ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika jiji la Dar
es salaam umeanza mwezi Desemba, mwaka 2016 ambapo umehusisha barabara
tatu za Kifuru – Msigani (km 4.5), Goba – Makongo (km 4.5), na Goba –
Madale (km 5) na kugharimu Jumla ya Shilingi Bilioni 24.2.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment