Baadhi ya Watumishi wa Umma, Viongozi wa Dini na Viongozi wa Taasisi Binafsi
wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye
ukumbi wa Benjamin Mkapa jijini Mbeya julai 31, 2017.
NA OWM, MBEYA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza
Kamanda wa ...Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya
Bw. Emanuel Kiabo kumkamata na kumuhoji Mheshimiwa Atanas Kapunga
aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya na wenzake 11 kwa tuhuma za kuisababishia
Serikali hasara ya sh. bilioni 63.448.
"Serikali hii haiwezi ikawaacha watu hawa
ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa halmashauri moja. Kama
wako humu ndani nagiza wakamatwe na waanze kuhojiwa na ambao wamestaafu au
kuhamishwa kituo cha kazi wasakwe popote walipo ili nao waje kuhojiwa.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu,
Julai 31, 2017) alipozungumza na watumishi wa Halmashauri za wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji
la Mbeya katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Benjamin Mkapa.
Wengine ni waliowahi kuwa wakurugenzi wa Jiji
hilo ambao ni Bw. Mussa Zungiza, Bi. Elizabeth Munuo, Bw. Juma Idd na Dkt.
Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya Ukurugenzi.
Aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji, Bw. James
Jorojik pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ambao ni Bw. Mussa
Mapunda, Bw. Samweli Bubengwa, Bw. Davis Mbembela, Bi. Lydia Herbert na Bw.
Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo bila ya kuzingatia
maslahi ya Jiji pamoja Emily Maganga ambaye hakuishauri vizuri bodi hiyo.
Waziri Mkuu amesema watumishi hao wanatakiwa
kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kwa kuwa wameisbabishia Serikali
harasa kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko la Mwanjelwa Jijini Mbeya ambalo
hadi sasa halijaonyesha tija.
Amesema mradi huo wa soko la Mwanjelwa
uligubikwa na changamoto nyingi kuanzia hatua za awali ambapo hata uchukuaji wa
mkopo haukuwa umezingatia mpango mkakati wa biashara, hivyo kusababisha
Halmashauri ya Jiji kuchukua mkopo zaidi ya kiasi kilichokusudiwa.
Waziri Mkuu amesema mbali na kuzidisha kiasi
cha mkopo pia baada ya kukamilika kwa ujenzi watuhumiwa hao waligushi mikataba
ya upangaji, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya
Umma. Pia waligawa vizimba kwa wafanyabiashara bila ya kupitia mchakato wa
manunuzi.
Amesema hata wahanga ambao walikuwepo awali
kabla ya kuungua kwa soko hawakupewa kipaumbele katika mchakato wa upangishaji
wa soko jipya, ambapo kwa hali ya kawaida ilitarajiwa wangekuwa wa kwanza
kufikiriwa kutokana na hasara waliyoipata baada ya kuunguliwa mali zao.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya. Bw. Amos Makalla kukutana na Madiwani wa Halmashauri ya Jiji na kuweka
mikakati na namna gani wataweza kupanga bei ya vizimba katika soko hilo ili
wafanyabiashara wapange na wao kuweze kuanza kupata fedha za kupunguza deni.
No comments:
Post a Comment