Afisa
Lishe kutoka Kitengo cha Lishe Wizara ya Afya Fatma Ali Said
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wiki ya unyonyeshaji katika
ukumbi wa Wizara hiyo Mnazimmoja Mjini Zanzibar. (Picha na Ramadhani
Ali)
………………………………………………………………………….
Na Ramadhani Ali-Maelezo Zanzibar
Akinamama
wamehimizwa kuendelea kunyonyesha watoto wao maziwa ya kifua pekee...
katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila ya kuwapa chakula chengine
ili kuwajenga katika afya bora na kukua vizuri kiakili na kimwili.
Afisa
Lishe kutoka Kitengo cha Lishe Wizara ya Afya Fatma Ali Said ameeleza
hayo katika ukumbi wa wizara hiyo Mnazimmoja alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji iliyoanza
jana.
Alisema
maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzao
yanamkinga mtoto na maradhi mengi kwani yanavirutubisho vya kutosha vya
kuwawekea kinga na kujenga upendo baina yake na mama.
Afisa
huyo alisema mama anaponyonyesha mtoto kipindi hicho bila kumpa kitu
chengine inapunguza kutoka damu nyingi katika siku 40 baada ya
kujifungua na humsaidia kurudi katika hali yake ya kawaida kwa haraka.
Alikumbusha
kuwa kunyonyesha mtoto maziwa ya kifua pekee katika miezi sita ya
mwanzo hakuna gharama kwa wazazi na baadhi ya akinamama inawasaidia
kujiepusha na mimba nyengine katika kipindi hicho na kupelekea uzazi wa
mpango.
Alisema
bado jamii kubwa ya Wazanzibari haina mwamko wa kunyonyesha maziwa ya
mama pekee miezi sita ya mwanzo na utafiti uliofanywa mwaka jana
unaonyesha ni asilimia 20 tu ya akinamama ndio wanaonyonyesha kwa
kutumia utaratibu huo.
Aliongeza
kuwa madai ya baadhi ya watu kwamba maziwa ya mama pekee bila chakula
chengine hayamtoshelezi mtoto hayana ukweli iwapo mtoto atanyonyeshwa
kwa muda unaotakiwa.
Alisema
mtoto anatakiwa anyonye kwa dakika zisizopungua 20 bila kupumzika ili
apate maziwa yalioko mbali ambayo ndio yenye chakula na mafuta kwa ajili
ya kumjenga mtoto.
“Maziwa
ya mwanzo ya mama yanamaji mengi lakini maziwa yanayochelewa kwa
dakika 20 yanavirutubisho vyote muhimu katika makuzi ya mtoto,”
aliongeza Afisa Lishe.
Aliwataka
akinamama wanaofanyakazi sehemu mbali mbali kufanya juhudi ya
kuwakamulia maziwa watoto wao na kuyahifadhi vizuri ili waweze kupewa
wakati hawapo majumbani.
Aidha
aliwakumbusha akinamama kuendelea kunyonyesha watoto wao iwapo itatokea
bahati ya kupata mimba nyengine wakati mtoto aliezaliwa bado anaumri
mdogo kwani maziwa ya mama mjamzito hayana madhara yoyote kwa mtoto.
Kilele
cha wiki ya unyonyeshaji kitakuwa tarehe 7 mwezi huu katika Wilaya ya
Micheweni na kauli mbiu ya mwaka huu Tudumishe unyonyeshaji kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment