Pages

Saturday, July 1, 2017

Serikali Yawataka Wataalam wa Mikataba Kuwa Wazalendo


unnamed (93)
Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Wataalamu wa majadiliano ya mikataba wametakiwa kuweka maslahi ya Taifa mbele wanapoandaa mikataba ya kimataifa ili kulinda na kusimamia raslimali za nchi.
Wito huo umetolewa jana na Naibu Mwansheria Mkuu wa Serikali, Gerson Mdemu wakati
akifunga mafunzo ya maafisa waandamizi wa serikali za nchi tisa za kiafrika kuhusu majadaliano ya mikataba ya kibiashara ya kimataifa yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mdemu aliwasititiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia ujuzi walioupata kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika kwa majuma mawili kwa ajili ya maslahi ya nchi zao ili kulinda raslimali  za nchi husika ili zitumike kwa manufaa ya umma.
“Tangulizeni maslahi ya nchi na si ya kwenu binafsi katika mikataba ya kimataifa na kuondokana na vitendo vya rushwa”, alisema Mdemu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mafunzo wa Uongozi Institute, Kadari Singo amesema mafunzo hayo yameandaliwa kutokana na nchi za kiafrika kuwa nyuma katika majadaliano ya mikataba ya kimataifa.
“Tumeamua kufanya mafunzo haya kuwafundisha maafisa waandamizi toka nchi za kiafrika ili kuwapa ujuzi na utaalamu wa kufanya majadiliano ya mikataba ili iweze kuwa na manufaa kwa nchi husika”, alisema Singo.
Kwa mujibu wa Bwana Singo, mafunzo ya aina hiyo yatakuwa endelevu kwa watumishi wa Serikali ii kuiwajengea uwezo katika eneo hilo na yatakuwa yakifanyika kujumuisha wataalam wa sekta husika kama vile, sekta madini, misitu, wanyamapori na sheria.
Aidha, Singo alisema mafunzo haya yatahakikisha yanapinga vikali vitendo vya rushwa kwenye mikataba ili kuzinusuru nchi za kiafrika kutumbukia katika mikataba isiyowanufaisha wananchi.
Mafunzo haya yameandaliwa na Uongozi Institute na yamewajumuisha watumishi wa serikali waandamizi kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Kenya, Ghana, Nigeria, Uganda, Namibia na wenyeji Tanzania.
Hivi karibuni, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati akipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa madini alimtaka Spika wa Bunge kutumia Bunge lake kupitia sheria za madini ili kuhakikisha sheria hizo zinaleta manufaa kwa wananchi.
Mikataba ya madini na mali za asli nyingine imekuwa ikipigiwa kelele kuwa haina lengo la kuinufaisha nchi bali watu wa nchi nyingine. Hivyo Miswada ya Maliasili za nchi imepelekwa Bungeni kwa Hati ya Dharula ili kutoa nafasi ya kutunga sheria mapema iwezekanavyo za kuleta manufaa na tija kwa nchi hasa kupitia madini na maliasili nyingine zikiwemo mbuga za wanyama na hifadhi nyingine za Taifa.
Kwa kuzingatia unyeti na umuhimu wa suala hilo, muda wa kumaliza Bunge umeongezwa badala ya kumaliza Juni 30 sasa litaenda hadi Julai 5, 2017.

No comments:

Post a Comment