Kaimu Kamishna wa Nishati na
Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga (kulia) akipokewa na Meneja
Mkuu wa Hoteli ya Serena Mivumo River Lodge, Ellieta Mbisse (kushoto)
mara bada ya kuwasili katika uwanja mdogo wa Stiegler’s Gorge, Rufiji
mkoani Pwani kabla ya kuanza kwa ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na
Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na
wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia
maji kutoka Ethiopia pamoja na wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi
wa mabwawa kutoka Tanzania wakiongozwa na mwenyeji wao Naibu Waziri wa
Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini
Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye helikopta, mara bada ya kuwasili
katika uwanja mdogo wa Stieglers Gorge, Rufiji mkoani Pwani kabla ya
kuanza kwa ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka
Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya
ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia
pamoja na wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka
Tanzania
Naibu Waziri wa Nishati na Madini
Dk. Medard Kalemani ( wa pili kulia mbele) akimwongoza Waziri wa Maji,
Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (katikati
mbele) kwenye ziara ya kukagua eneo la ujenzi wa mradi wa kuzalisha
umeme kwa kutumia nguvu za maji la Stiegler’s Gorge, Rufiji mkoani Pwani
katika ziara hiyo
Waziri wa Maji, Nishati na
Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (kushoto) akieleza
jambo kwa Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) katika ziara hiyo. Anayesikiliza
katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.
Kipimo cha kupimia kina cha maji (water gauge) katika sehemu ya mto Rufiji uliopo katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini
Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye boti kwa ajili ya kuelekea kwenye
eneo la Stieglers Gorge kutakapojengwa mradi huo.
Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) akifafanua
jambo kwa Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk.
Seleshi Bekele ( wa pili kushoto). Katikati ni Naibu Waziri wa Nishati
na Madini Dk. Medard Kalemani.
Waziri wa Maji, Nishati na
Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Sileshi Bekele ( wa tatu kushoto)
akieleza jambo katika ziara hiyo.
Sehemu ya Mto Rufiji
kutakapojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji
katika eneo la Stieglers Gorge wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Kaimu Kamishna wa Nishati na
Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) akielezea
maandalizi ya mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji wa
Stieglers Gorge kwa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Ethiopian Construction Design and Supervision kutoka Ethiopia, Dk. Negede Kassa (kulia) katika ziara hiyo.
………………………………
Megawati 5000 kupatikana 2021
- Ni baada ya kukamilika kwa mradi wa Stieglers Gorge
Juni 30, 2017
Na Greyson Mwase, Rufiji.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini
Dk. Medard Kalemani amesema Tanzania inatarajia kupata umeme wa uhakika
wa Megawati 5000 ifikapo mwaka 2021, mara baada ya kukamilika kwa mradi
wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji katika maporomoko ya maji
ya Mto Rufiji kwenye eneo la Stiegler’s Gorge lililopo Rufiji mkoani
Pwani ambao utaongeza umeme wa kiasi cha Megawati 2100 katika gridi ya
taifa
Dk. Kalemani aliyasema hayo jana
tarehe 29 Juni, 2017 katika ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na
Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na
wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia
maji kutoka Ethiopia kwenye eneo la mradi wa kuzalisha umeme kwa
kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji ya Stieglers Gorge wilyani
Rufiji mkoani Pwani.
Wengine walioshiriki katika ziara
hiyo ni pamoja na wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa
kutoka Tanzania, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya
Nishati na Madini.
Ziara hiyo inafuatia maombi ya
Rais John Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia ya kutuma wataalam wa
masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za
maji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na wataalam wa masuala ya umeme
na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania.
Dk Kalemani alisema kuwa
kupatikana kwa umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021 kutachochea ongezeko
la viwanda hivyo kuongezeka kwa fursa za ajira na biashara na kukuza
uchumi wa nchi.
Alisema mradi huo mkubwa ni moja
ya mikakati ya Serikali kuhakikisha nishati inakuwa na mchango mkubwa
katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa yenye lengo la
kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika orodha ya nchi maskini duniani na
kuingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Alisisitiza kuwa mbali na mradi
huo mkubwa, serikali imeweka mikakati ya kutumia vyanzo vingine vya
nishati kama vile Gesi, Makaa ya Mawe, Jotoardhi, Upepo ili kuhakikisha
kuwa nchi inapata umeme wa uhakika.
Akielezea mafanikio ya mradi huo
mbali na upatikanaji wa umeme wa uhakika, Dk. Kalemani alisema kuwa
mradi huo utachochea ukuaji wa shughuli za uvuvi katika mkoa wa Pwani.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni
pamoja na kukuza sekta ya Utalii katika mkoa wa Pwani pamoja na kuzuia
mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika mto Rufiji na
kuathiri makazi ya wakazi waishio pembezoni na mto huo.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya
maandalizi ya ujenzi wa mradi huo mkubwa, Dk. Kalemani alisema baada ya
timu ya wataalam kutoka Tanzania na Ethiopia kufanya ziara katika eneo
la mradi hatua inayofuatia ni wataalam kukaa vikao mbalimbali kujadili
namna bora ya kutekeleza mradi pamoja na kubadilishana uzoefu.
Alisema mara baada ya ujenzi wa
mradi huo kukamilika, moja ya kazi zitakazofanywa ni pamoja na ujenzi wa
njia ya kusafirisha umeme hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 200 na
njia ya kusafirisha umeme kutoka eneo la Mradi hadi Singida yenye
urefu wa kilometa 800
Waziri Kalemani aliwataka wananchi
na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya
Tano ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji hususan katika mto
Rufiji.
Wakati huohuo, katika ziara hiyo
Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi
Bekele alisema kuwa mradi huu mkubwa ni mzuri na unatekelezeka na
kuongeza kuwa Ethiopia ipo tayari kutoa ushirikiano mkubwa kupitia
wataalam wake lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa mradi unafanikiwa na
kukamilika kwa wakati.
No comments:
Post a Comment