Benny Mwaipaja, WFM, DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Norway imeipatia
Tanzania msaada wa Dola Milioni 10 za Marekani kupitia programu ya
maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, inayotarajiwa kuanza Mwaka Mpya
wa Fedha- Julai Mosi mwaka huu.
Mpango huo pamoja na uzinduzi wa
Awamu ya Pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya
Mafuta, umezinduliwa
Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Borge Brende,
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango na Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo kwa niaba ya
Serikali zao.
Dkt. Mpango ameishukuru Serikali
ya Norway kwa msaada huo mkubwa utakaochangia kuboresha utendajikazi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuijengea uwezo zaidi wa kitaalamu,
miundombinu na vitendeakazi vingine vitakavyo changia kuongeza uwezo wa
Mamlaka hiyo wa kukusanya mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo amesema
kuwa hatua ya Serikali ya Norway kuendelea kufadhili programu ya pili ya
Mpango wa kuendeleza Sekta ya Mafuta utaiwezesha Serikali kubobea
katika masuala ya utaalamu wa masuala ya sheria na usimamizi wa sekta
hiyo.
Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa
Norway, Mhe. Borge Brende amesifu utendaji kazi mahili wa Mhe. Rais
Dokta John Pombe Magufuli wa kupambana na ufisadi na vitendo vya rushwa
pamoja na kuimarisha ukusanyaji kodi, hatua ambayo itaifanya nchi ipige
hatua za maendeleo haraka.
Amesema kuwa hajawahi kuona nchi
yoyote duniani ikiendelea bila kuweka nidhamu na uwajibikaji serikali
pamoja na kutokusanya mapato yake ipasavyo na kuahidi kuwa nchi yake
itaendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano kufanikisha mipango
yake ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
No comments:
Post a Comment