Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wafanyakazi katika
kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika Kitaifa katika
Uwanja wa Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
…………………………………………………………………
Na Nuru Juma, Husna Saidi – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aahidi nyongeza ya kawaida kwa
mishahara na kuwapandisha madaraja wafanyakazi wanaostahili.
Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo
leo alipokuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi
Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chuo Cha Ushirika,
Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Magufuli alisema Serikali
ilisitisha upandishaji wa vyeo na mishahara kutokana na kuwepo na
watumishi hewa na walioghushi vyeti lakini baada ya kuondolewa Serikali
itahakikisha inashughulikia maslahi ya wafanyakazi.
“Watumishi 9932 walikuwa na vyeti
feki,watumishi hewa walikuwa 19706 hivyo kama Serikali ingeongeza
mishahara inamaana watumishi hawa pia wangefaidika na pesa ambazo
hawakustahili kuzipata”, alisema Dkt. Magufuli.
Aidha aliwataka waajiri kuheshimu
na kutoa mikataba ya kazi na kutowanyanyasa wafanya kazi wao na
wafanyakazi kuomba kazi kulingana na elimu zao na waache tabia ya
kughushi vyeti.
Aliongeza kuwa Serikali
itashughulikia mfumuko wa bei za bidhaa na kuhakikisha viwanda vingi
vitajengwa sehemu mbalimbali nchini ili kuongeza ajira kwa vijana wa
kitanzania.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
TUCTA Dkt. Yahya Msigwa ameipongeza Serikali kwa kutekeleza ahadi zake
na kuopngeza kuwa hiyo ni ishara tosha kuwa Serikali inayodhamira ya
dhati ya kuwajali wananchi wake wakiwemo wafanyakazi.
Ameongeza kuwa wanayo imani kubwa
kwa Serikali kuwa itatekeleza ahadi yake ya kufanyia maboresho ya
maslahi ya umma kama ambavyo umeonyesha nia njema ya kutekeleza ahadi
zake.
Alizitaja baadhi ya ahadi
zilizotekelezwa kuwa ni pamoja, kupiga vita rushwa na ufisadi, kuondoa
watumishi hewa, Serikali kuhamia Dodoma, ujenzi wa miundombinu ya reli,
vita dhidi ya dawa za kulevya pamoja na ununuzi wa ndege.
“Ni imani yetu kuwa ahadi hii ya
kuboresha maslahi kwa Watumishi wa Umma itatekelezwa kwa wakati kwani
tayari umekwisha ondoa mambo yaliyokuwa yanakwamisha zoezi hilo,”
alisema Dkt. Msigwa.
Wakati huohuo Katibu Mkuu huyo
ameiomba Serikali kuharakisha kubuni namna ambavyo wafanyakazi
watanufaika na Mifuko ya Jamii na wanaodai mapato yao kusikilizwa kesi
zao kwa wakati.
Maadhimisho hayo yameuhudhuriwa
na viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwemo Makamu wa Rais Mama Samia
Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job
Ndugai,Naibu Spika Tulia Ackson, Mawaziri Jenister Mhagama na Angella
Kairuki, Profesa Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John
Kijazi pamoja na baadhi ya Wabunge. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Uchumi wa Viwanda Vizingatie Haki, Maslahi na Heshima ya Mfanyakazi”.
No comments:
Post a Comment