Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi akimkabidhi afisa wa usalama kutoka shirika la TANESCO
Mkoa wa Singida Juma Mauba zawadi ya cheti na TV flat screen baada ya
kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora mwaka 2017.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi akiwa ameshikama na Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya
wafanyakazi TUCTA Mkoa wa Singida Aaran Jumbe (kulia kwake) na Mkuu wa
Wilaya ya Singida Elias Tarimo (kushoto kwake) wakiimba wimbo maalumu wa
wafanyakazi wa Mshikamano daima pamoja na wimbo wa taifa.
Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kwa
Mkoa wa Singida.
Watumishi wa Kutoka Halmashauri ya
Ikungi wakipita mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi na
kuonyesha mazao ambayo huzalishwa kwa wingi wilayani humo ambayo ni
viazi vitamu na alizeti katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kwa
Mkoa kwa Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi akitoa zawadi ya mpira kwa viongozi wa wafanyakazi
wanawake kwa halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida ili waweze kuunda
timu za wanawake katika halmashauri zao.
…………………..
Waajiri wote Mkoani Singida
hususani wakurugenzi wa halmashauri ambao ndio wenye watumishi wengi
wameelekezwa kujenga mahusiano mazuri baina yao ili kuboresha utumishi
wao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi ametoa maelekezo hayo wakati wa
maadhimisho ya siku ya
wafanyakazi mkoani hapa yaliyofanyika katika uwanja wa Peolpe’s mjini
Singida.
Dkt. Nchimbi amesema mwajiri
na mtumishi sio maadui bali wanapaswa kujenga mahusiani mazuri hasa kwa
mwajiri kujenga mazoea ya kufahamu sifa za watumishi wake, shida na
matatizo yao.
Ameongeza kuwa waajiri
wamekuwa wakisubiria watumishi wakosee ndio wawape adhabu lakini
haipaswi kuwa hivyo kwani mwajiri anatakiwa ahakikishe anaweka mazingira
mazuri na kumuelimisha mtumishi asifanye makosa.
“Ukiona mtumishi anafanya
mambo yanayokinzana na sheria, kanuni na utaratibu, usimkaripie wala
kumtega, mtafutie afisa ustawi wa jamii. Kwa vyo vyote afisa ustawi wa
jamii atamrejesha kwenye mstari stahiki na mambo yatakwenda vizuri”.
Aidha Dkt Nchimbi amewataka
wakurugenzi kutofanya ziara nyingi nje ya halmashauri zao bali wajikite
katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi na watumishi wao ambazo
watazibaini endapo watafanya ziara za kutosha katika halmashauri zao.
Amesema ili kuboresha maslahi
ya watumishi, waajiri wanapaswa kuandaa mafunzo kwa watumishi juu ya
matumizi bora ya fedha ili waweze kutunza fedha zao, kila halmashauri
kutenga maeneo kwa ajili ya watumishi kupewa viwanja vya makazi pamoja
na kila halmashauri kuwa na afisa ustawi wa jamii atayehusika na
watumishi kwa ajila ya masuala ya ushauri.
Pia Dkt. Nchimbi amekemea
tabia mbaya ya baadhi ya wakuu wa idara/vitengo ya kuwa na mahusiano ya
kimapenzi na wafanyakazi wa kike walio chini yao.
“Wakuu hawa wa idara/vitengo
wanakiuka sheria kanuni na taratibu kwa kuanzisha mahusiano ya kimapenzi
humo humo kazini. Wakati mwingine wanafanya mapenzi na wake za watu.
Tabia hii haikubaliki na haivumiliki hata kidogo. Viongozi au wakuu wa
idara/vitengo wenye tabia ya aina hii, waiache mara moja”, amesema
Dk.Nchimbi.
Kwa upande wao wananchi na
watumishi Mkoani Singida wamempongeza rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zake utumishi wa umma ambapo
kwa sasa amerejesha nidhamu na uadilifu kwa kiwango cha kuridhisha.
Wananchi hao wamesema chini ya
serikali ya awamu ya tano watumishi wa umma wamebadilika sana na sasa
wanatoa huduma kwa ukarimu mkubwa, wepesi na uharaka zaidi tofauti na
ilivyokuwa awali.
“Huko nyuma watumishi wa umma
wengi walikuwa wana urasimu wa hali ya juu. Walikuwa wakitoa huduma huku
macho na akili zao zikiwa kwenye ‘whatsapp’. Mbaya zaidi mwananchi
ukipeleka kero zako, wanakuona ni msumbufu. Hivi sasa mambo ni tofauti
kero za wananchi zinatafutiwa majibu na majawabu kwa wakati,” ameongeza
Dkt. Nchimbi akiunga mkono maoni ya wananchi.
Mmoja wa wananchi
waliohudhuria maadhimisho hayo Sombi Hangida amekiri kwamba ni kweli
watumishi wa umma wamebadilika mno na sasa wanatoa huduma bila kuomba
rushwa na wamekuwa na lugha rafiki kwa wananchi.
Awali mwenyekiti wa Shirikisho
la Vyama vya wafanyakazi TUCTA Mkoani Singida Aaran Jumbe amehimiza
kuhusu mabaraza ya wafanyakazi kufanyika katika maeneo ya kazi kwa
mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na hasa kuwashirikisha vyama vya
wafanyakazi.
Jumbe ameongeza kuwa
halmashauri zimekuwa zikitoa ushirikiano kwa vyama vya wafanyakazi na
kuomba ushirikiano huo uendelee huku akisisitiza zawadi za mfanyakazi
hodari zinazo ahidiwa na taasisi na halmashauri zitolewe kwa wakati.
No comments:
Post a Comment