Waziri Mkuu wa Shirikisho la
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn
(katikati) akifurahia zawadi ya picha ya Bandari ya Dar es Salaam mara
baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Pro f.
Ignas Rubaratuka (kulia). Kushoto ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Kassim.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Kassim akisalimiana na
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA mara baada ya kuwasili bandari ya
Dar es Salaam kumpokea mgeni wake Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn hivi karibuni.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi
Deusdedit Kakoko akisalimiana na Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn mara baada ya
kuwasili bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni kwa ziara fupi.
………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
TPA
Waziri Mkuu wa Shirikisho la
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn amesema
Shirika la Meli la Ethiopia (Ethiopian Shipping Line) lipo tayari kuanza
kuitumia Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kutoa huduma nzuri.
“Shirika letu la Meli ambalo ni
la kihistoria na lililobaki pekee katika ukanda wa Afrika likiwa
linamilikiwa na Serikali ya Ethiopia sasa lipo tayari kufanya kazi na
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania,” amebainisha Mhe. Desalegn.
Ameongeza kuwa mbali na shirika
hilo la meli kuwa tayari kuanza kuleta meli zake Bandari ya Dar es
Salaam pia Shirika Kongwe la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airline) lenye
mafanikio makubwa nalo litaanza kusafirisha mizigo inayopitishwa katika
Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine Mhe. Desalegn
amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Menejimenti ya TPA katika
kuboresha huduma zake ambapo amesema jitihada hizo sio tu zitanufaisha
Serikali zote mbili bali pia ustawi wa maisha ya watu wa Tanzania na
Ethiopia nao utaimarika.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Kassim amemshukuru Waziri Mkuu wa
Ethiopia kwa kuja nchini ambapo amemuahidi kwamba mahusiano mazuri
yaliyopo baina ya nchi hizi mbili yatadumishwa kwa maslahi mapana ya
mataifa yote.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu
wa Tanzania, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Makame
Mbarawa amesema TPA itaendelea na mipango iliyopo ya kuhakikisha
inaboresha Bandari zake ili ziweze kuhudumia vyema wateja wote kwa
wakati.
“Tutaendelea kuboresha huduma
zetu za Bandari na za sekta ya uchukuzi kwa ujumla ili tuweze kufikia
malengo yenu na wateja wetu ya kuhakikisha kwamba tunawahudumia vizuri
na kwa ufanisi,” amesema Mhe. Mbarawa.
Mapema akitoa taarifa ya utendaji
wa Mamlaka, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko
alimweleza Waziri Mkuu wa Ethiopia kwamba kwa sasa TPA inaendelea na
mpango wake wa kujenga uwezo wa kuhudumia wateja wake kwa kuzingatia
kwamba sekta ya uchukuzi inakuwa kwa kasi.
“Kutokana na kasi kubwa ya ukuaji
wa uchumi nchini na Duniani kwa ujumla, TPA inaimarisha uwezo wake wa
kuhudumia mizigo na meli kubwa ili kujenga uwezo kabla ya mahitaji
makubwa kujitokeza”, amesisitiza Mhandisi Kakoko.
No comments:
Post a Comment