WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Eng. Evarist Ndikilo apige kambi
katika kata ya Miono wilayani Bagamoyo na kuwasaka wafugaji wanaopiga
wakulima.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo
wakati akizungumza na wakazi wa kata hiyo ambao
walisimamisha msafara
wake wakati akienda kukagua miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani
iliyoko wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Akitoa kero za eneo hilo, Diwani
wa Kata ya Miono, Bw. Juma Mpwimbwi alisema kata hiyo inakabiliwa na
tatizo la wakulima kupigwa na wafugaji na wakipelekwa kituo cha polisi
hawachukuliwi hatua yoyote.
“Wafugaji wanatupiga lakini
wenzetu hawachukuliwi hatua na hata ukienda kushtaki polisi, hawakai kwa
sababu wanadai wao wana fedha,” alisema diwani huyo.
Pia alisema mbali ya kero sugu ya
maji, waliahidiwa barabara ya lami tangu miaka saba iliyopita lakini
hadi sasa hawana hata kipande kidogo tu cha barabara hiyo.
Naye Bw. Shabani Mkwimbi ambaye
alipewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, alisema kata
hiyo ina kituo cha polisi na mahakama lakini utendaji kazi wa viongozi
waliopo hapo unatia shaka.
“Waziri Mkuu tunataka ukimaliza
kuongea na sisi, uondoke na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Miono, Bw. Maro
na msaidizi wake Bw. Rashidi pamoja na Hakimu wa hapa, kwa sababu hawa
watu habari yao ni nyingine. Mkulima akienda polisi au mahakamani
hashindi kesi hata siku moja, lakini mfugaji akienda anashinda,” alisema
huku akishangiliwa.
“Hawa watu wanadai wana hela na wanafanya chochote wanachotaka, na ndiyo maana hawalali polisi hata kama wameua mtu,” aliongeza.
Akijibu kero zao, Waziri Mkuu
aliwahakikshia wakazi hao kwamba Serikali iliyopo madarakani ni yao na
hakuna hata mtu mmoja ambaye yuko juu ya sheria.
Alisema suala la polisi wa kituo
cha Miono litashughulikiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, ambaye
alikuwepo katika msafara wake. “Tena Mkuu wa Mkoa yuko hapa na yeye
ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huu, atasimamia
hilo.”
Akifafanua kuhusu suala la
wafugaji kuwapiga wakulima, Waziri Mkuu alisema msimamo wa Serikali ni
kuwaona wakulima wanafanya kazi zao kwa uhuru na wafugaji nao wanafanya
kazi zao kwa uhuru. “Hakuna mfugaji anayeruhusiwa kupeleka ng’ombe wake
kwenye mashamba yenye chakula. Hili haliruhusiwa hata kidogo,”
alisisitiza.
“Mkuu wa Mkoa hili ni agizo. Njoo
upige kambi hapa na watu wako, na usake wahusika hadi wabainike. Ni
lazima tuwajue ni akina nani wamehusika na hili,” alisema.
Aliwataka maafisa mifugo wa mkoa
huo waende kwa wafugaji na kutambua mifugo waliyonayo na kama kuna
maeneo wahakikishe wanapatiwa maeneo rasmi ili waweze kupatiwa matibabu
kwa ajili ya mifugo yao.
Aliwataka wafugaji wanaokata
mabomba ya maji ya mradi wa maji wa Chalinze (CHALIWASA) ili kupata maji
ya kunywesha mifugo yao, waache tabia hiyo mara moja na akaonya kuwa
watakaokamatwa, wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri
Mkuu alikuwa amefuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa pwani, Eng. Evarist
Ndikilo, viongozi wa wilaya ya Bagamoyo na Mbunge wa jimbo hilo,
Ridhiwani Kikwete.
No comments:
Post a Comment