WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewakaribisha wawekezaji kutoka Italia ili waje kuwekeza kwenye viwanda
na usindikaji bidhaa za mifugo na uvuvi kwa sababu ni eneo wanalolimudu
vizuri.
“Tumedhamiria kujenga Tanzania ya
viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoa Italia ili
waje kuwekeza
kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya mifugo pamoja na uvuvi kwa sababu
tunatambua kuwa ninyi mmebobea katika eneo hilo,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Jumanne, Februari 28, 2017) alipokutana na Balozi wa Italia nchini
Tanzania, Bw. Roberto Mengoni kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es
Salaam.
“Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa
umaskini miongoni mwa wananchi wake. Tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye
maeneo mbalimbali,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Balozi Mengoni
alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika muda wa miezi nane ambayo ameishi
hapa nchini, amebaini kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa nyingi za
kiuchumi. “Ni soko kubwa ambalo halijaguswa (untapped market) hasa
kwenye masuala ya viwanda na uwekezaji.
Hata hivyo, Balozi huyo alikiri
kwamba bado wananchi wengi wa Italia wanahitaji kupatiwa elimu zaidi juu
ya fursa zilizopo hapa nchini. “Hadi leo kuna Waitaliano ambao hawajui
kuwa Mlima Kilimanjaro uko Tanzania. Wengi wanajua uko Kenya, kwa hiyo
elimu zaidi inahitajika katika suala zima la kutangaza utalii wa
Tanzania,” alisema.
Alisema tangu afike nchini,
wawekezaji kutoka Italia wameonesha nia ya kuwekeza kwenye nishati
jadidifu, kiwanda cha kutengeneza nguo za michezo (sports wear) na
kwamba wafanyabiashara wengine zaidi wanatarajia kuja hapa nchini.
Ili kutoa uelewa mpana kwa
wafanyabiashara na raia wa Italia, ubalozi kwa kushirikiana na Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) tumeandaa mkutano mkubwa kuhusu biashara na
uwekezaji utakaotoa maelezo kuhusu fursa zilizopo Tanzania katika nyanja
mbalimbali.
“Mkutano huu utakaofanyika Mei 6,
mwaka huu, utawalenga zaidi wafanyabiashara na utajikita kwenye maeneo
makuu sita ambayo ni viwanda vya usindikaji, viwanda vya nguo
(textiles), ngozi na mazao yake, miundombinu, nishati na utalii,”
alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amekutana na Balozi wa Japan hapa nchini, Bw. Masaharu Yoshida ambapo
katika mazungumzo yao wamejadiliana mambo mbalimbali yakiweo ya
miundombinu, elimu na nishati.
No comments:
Post a Comment