Muonekano wa baadhi ya Nyumba
zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) Bunju, nje kidogo ya jiji
la Dar es Salaam zikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo
Nchini (TBA), Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua hatua iliyofikiwa
kwenye ujenzi wa nyumba kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa
nyumba hizo jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa moja ya mtungi wa
kutengenezea gesi ukaa (Biogas), inayoendelea kujengwa katika Nyumba
zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA), eneo la bunju jijini
Dar es Salaam. Gesi hiyo itatumika kutoa huduma kwa wakazi wa eneo hilo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo
Nchini (TBA), Arch. Elius Mwakalinga (wa tatu kulia), akimuonyesha
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani,
hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam zinazojengwa na Wakala huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa
Uongozi wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA), alipokagua maendeleo ya
ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kulia
ni Meneja Kikosi cha Ujenzi cha TBA, Arch. Hamphrey Killo.
Muonekano wa moja ya jengo la
hosteli ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambalo limekamilika
na majengo hayo yataanza kutumika wiki ijayo kufuatia ujenzi wake
kukamilika.
……………………………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani ameupongeza Wakala wa Majengo Nchini
(TBA), kwa jitihada wanazozifanya katika kuongeza mapato na
kununua
vifaa vipya na kisasa vitakavyowezesha wakala huo kumudu ujenzi wa
miradi mingi mikubwa kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kukagua
mradi wa nyumba 851 ulioko Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na
mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Eng. Ngonyani ameeleza
kuridhishwa kwake na mabadiliko makubwa ya utendaji yanayoendelea katika
wakala huo.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri ya
ujenzi wa nyumba za kisasa za makazi ya watu, ongezeni ubunifu ili
nyumba zote zinunuliwe na kuwawezesha Watanzania kupata makazi bora kwa
bei nafuu’ amesema Eng. Ngonyani.
Ameitaka TBA kuhakikisha inapata
faida ili kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali kama ilivyo kwa
taasisi nyingine za Umma na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza kasi
katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
‘Ongezeni kasi katika ukusanyaji
wa madeni kwa watu binafsi wanaokaa kwenye nyumba zenu na sisi Wizarani
tutawasaidia katika kuhakikisha mnalipwa kwa wakati kwa wadaiwa wa
Serikalini’ amesisitiza Eng. Ngonyani.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri
huyo ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya TBA katika ujenzi wa
mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo
yanatarajiwa kukabidhiwa kwa chuo hicho wiki ijayo.
Mbweni hayo yenye uwezo wa
kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,840 yamejengwa na TBA katika kipindi
kisichozidi miezi sita na yamegharimu takribani shilingi bilioni 10.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch.
Elius Mwakalinga amemhakikishia Naibu Waziri Eng. Ngonyani kuwa Wakala
huo umejiimarisha kwa kuwa na vifaa vya kisasa na watendaji wenye sifa
hivyo Serikali iendelee kuuamini na kuupa miradi mingi ya ujenzi wa
nyumba na ofisi.
“Tunao wahandisi 74, wachoraji
ramani 66, wakadiriaji majenzi 52 na bado tunao wataalam mbalimbali
kutoka kwenye vyuo vikuu nchini wanaowezesha wakala wetu kuwa imara
wakati wote’ amesema Arch. Mwakalinga.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yuko
katika ziara ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi
inayosimamiwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) jijini Dar es Salaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment