Na: Lilian Lundo – MAELEZO.
Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira
ikishirikiana na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC),
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo imefanya operesheni kwa
baadhi ya wasambazaji wa pombe za kali zinazofungashwa katika plasti
maarufu kama kiviroba ili
kujiridhisha kama wameitikia wito wa kusitisha
utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa pombe hizo.
Akiongea na vyombo vya habari
Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard
Muyungi amesema kuwa operesheni hiyo imeanza na wasambazaji, wauzaji na
watumiaji huku wakiendelea kupitia baadhi ya maombi ya wamiliki wa
viwanda juu ya usitishaji wa pombe hizo.
Aidha operesheni hiyo imefanyika
katika wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala kwa kutembelea maghala
yanayohifadhi pombe hizo ili kujua idadi ya pombe ambazo bado zipo
katika maghala hayo pamoja na kufuatilia ikiwa wamiliki wa maghala hayo
wametii amri ya kusimamisha usambazaji wa Pombe hizo zilizofungiwa
kuanzia Marchi 01, 2017.
Msimamizi wa ghala la Pombe za
Viroba aina ya Kiroba Original lililopo Mabibo wilaya ya Kinondoni
Mhina Rashid amesema kuwa akiba ya pombe hizo za viroba zilizobaki
katika maghala yao ni katoni 6600 za ujazo wa Ml 50 na katoni 4909
zenye ujazo wa Ml100.
“Kwa sasa tumefunga maghala na
hakuna usambazaji wowote wa pombe aina ya kiroba unaofanyika hapa
tunasubiri taratibu za Serikali kujua nini cha kufanya kwa pombe ambazo
bado zipo katika maghala,” alifafanua Mhina Rashid.
Aliendelea kwa kusema kuwa
ikiwezekana Serikali iongeze muda wa matumizi ya pombe hizo kutokana na
kuwa na mzigo mkubwa katika maghala mengi yanayohifadhi pombe hizo.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi
wa Viwango na Mkaguzi wa TBS Banza Suleiman amesema kuwa viroba Original
vina nembo ya TBS lakini kutokana na sheria mpya ambayo imepiga
marufuku matumizi ya pombe hizo hivyo wasambazaji hawaruhusiwi kusambaza
pombe hizo bali wanapaswa kusubiri maelekezo toka Serikalini.
Vile vile operesheni hiyo
imefanyika katika kiwanda cha Afro American kilichopo Mwenge ambao ni
watengenezaji wa pombe za viroba aina ya Zed, Royal na Dollors na kukuta
zaidi ya tani 5 ya pombe hizo.
Msimamizi wa kiwanda hicho
Muhandisi Sabra Voleti amesema kuwa wamesimamisha uzalishaji wa pombe za
viroba huku wakisubiri maelekezo toka Serikalini. Aidha amesema kuwa
kiwanda hicho kinaendelea na uzalishaji wa pombe ambazo vifungashio
vyake ni vya chupa.
Kwa upande wake Mwanasheria wa
NEMC Manchare Heche Suguta amesema kuwa adhabu ya matumizi ya
vifungashio vya plastiki (Viroba) vinatofautiana kati ya mtengezaji,
msambazaji, muuzaji na mtumiaji. Aidha adhabu yake ni faini kati ya
shilingi elfu 50 na Milioni 5 au kifungo kisichopungua miaka 3.
Hivyo amewataka watanzania kujiepusha na matumizi ya pombe hizo pamoja ikiwa ni pamoja na utengenezaji na usambazaji wake.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Kassim Majaliwa akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Manyara
Februari, 2017 aliagiza pombe hizo kutoendelea kutumika kuanzia Marchi
1, 2017.
No comments:
Post a Comment