Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Rais wa Shirikisho la Filamu
Tanzania, Simon Mwakifamba amekana kuhusika na utumaji wa ujumbe katika
mitandao ya kijamii juu ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini
Dar es Salaam na Rais wa Shirikisho hilo alipokuwa
akizungumza na
waandishi wa habari juu ya ujumbe huo uliokuwa ukisambazwa katika
mitandao mbalimbali ya kijamii na kumuhusisha Rais wa Shirikisho hilo.
Mwakifamba amesema kuwa ujumbe huo
umeeleza kuwa Rais wa shirikisho hilo atakuwa na mkutano na waandishi
wa habari utakaohusu wasanii waliokipigia kampeni Chama cha Mapinduzi
(CCM) na kutolipwa fedha zao pamoja na kuunga mkono jitihada za msanii
Wema Sepetu kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Kiukweli sikushiriki kwa namna
yoyote katika kuuandika ujumbe huo na nimesikitishwa kuona kwamba huo
ujumbe unasambazwa ukiwa na jina langu hivyo umeniletea picha mbaya
kwani ni kinyume na taratibu na sheria za Shirikisho,”alisema
Mwakifamba.
Amefafanua kuwa Shirikisho hilo
sio chama cha siasa na hawajasajiliwa na msajili wa vyama vya siasa bali
wamejisajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kazi zote
zinafanyika kwa Sheria Na. 4 ya mwaka 1976 ambayo iko chini ya Bodi ya
Filamu Tanzania.
Ameongeza kuwa mwanachama wa
shirikisho hilo hafungwi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa
lakini kwa mujibu wa katiba ya vyama na shirikisho ni marufuku siasa
kuletwa katika shirikisho au vyama vyake.
Kwa upande wake Afisa Mipango wa
Chama cha Waigizaji, Saimon Mwapagaja ametoa rai kwa wananchi wanaotumia
vibaya mitandao ya kijamii kwa lengo la kuchafua majina ya watu kuacha
tabia hiyo kwani inashusha hadhi ya mtu husika na sio utaratibu mzuri.
“Changamoto tulizonazo katika
tasnia ya filamu ni nyingi sana hivyo ifike wakati wasanii tuanze
kuangalia vitu vya msingi na vyenye tija vitakavyomaliza changamoto
hizo, pia wananchi wapunguze kujiamulia kufanya mambo ambayo baadae
yanaweza kumsababishia muhusika matatizo mabukwa,” alisema Mwapagaja.
No comments:
Post a Comment