Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili kuwa Tanzania ambayo yatakuwepo Zanzibar.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Nape Nnauye ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma
alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya jitihada mbalimbali ambazo Tanzania
inazichukua katika kukuza Lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Kimataifa.
Nape amesema kuwa maamuzi hayo ya
kuifanya Tanzania kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili yametokana na
Tanzania kuzalisha walimu wengi wa Kiswahili ambao wanatumika katika
ngazi mbalimbali za elimu ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Wizara hiyo, Anastazia Wambura amesema kuwa Wizara hiyo kwa sasa
inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa
mawakala wa kulinda Lugha ya Kiswahili ambapo Baraza la Kiswahili la
Taifa (BAKITA) kwa kushirikiana na wadau wa Kiswahili limeendelea
kuendesha semina, warsha, makongamano na kutoa elimu inayohusu matumizi
fasaha ya Lugha ya Kiswahili.
Aidha, aliendelea kwa kusema kuwa
Waandishi wa Habari wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha Lugha hiyo
inaendelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya
Lugha hiyo katika majukumu yao ya kila siku.
“Kutumia zana kama vile Kamusi na
vitabu vya miongozo ya uandishi pamoja na kuhudhuria makongamano ya
Kitaifa na ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili inasaidia kuongeza ujuzi
na uweledi wa Lugha ya Kiswahili, kujua istilahi za kisayansi na
kiteknolojia na hivyo kuandika na kutangaza kazi bora na zenye maudhui
lengwa kwa jamii na kuepuka upotoshaji wa maneno ya Kiswahili usio wa
lazima,” alifafanua Anastazia Wambura.
Hata hivyo Wizara hiyo iko katika maandalizi ya Sera ya Lugha
ambayo itabainisha majukumu ya Vyombo vya Habari katika matumizi na
uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili.
No comments:
Post a Comment