KATIKATI ya foleni katika
jiji la Dar es Salaam ndani ya gari nyeupe aina ya Mercedes S550,
Jacqueline Ntuyabaliwe, mrembo wa miaka 38, macho yake yalikuwa
yametulia katika simu yake ya mkononi.
Alikuwa akiangalia seti ya samani
za eneo la kulia chakula. Kwa bashasha, baada ya muda kidogo anatanua
picha hiyo kisha ananisogezea simu yake ya mkononi kunionesha picha
anayoiangalia.
“Hii ni moja ya samani
tulizonazo,” anasema huku akinionesha seti hiyo ambayo imetengenezwa na
Molocaho by Amorette, kampuni ya kutengeneza samani aliyoianzisha hivi
karibuni.
“Samani hizi zimetengenezwa
kutokana na mbao zilizotwaliwa kutoka katika mashua za zamani za mizigo
kwenye fukwe za Tanzania upande wa bahari ya Hindi,” anasema
mjasiriamali huyo.
Samani hizo za eneo la kulia
chakula (Dining Table) anasema zimeagizwa na familia moja iliyopo Ulaya
ambayo siku za karibuni ilitembelea duka lake (showroom) Dar es Salaam
wakati wakiwa likizo na kwamba anajiandaa sasa kuisafirisha seti hiyo ya
samani kwa wateja wake wapya wa Ulaya.
Lakini kwanza alichokuwa
anakifanya kwa siku ile ni kwenda kiwandani kuangalia seti hiyo ya
samani kwa mara ya mwisho kabla ya kusafirishwa ili kujihakikishia
kwamba imemaliziwa urembeshaji kwa namna inavyotakiwa kuwa.
Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi.
Jacqueline Ntuyabaliwe, anayetaka
umaridadi uliokamilika, ni binti ambaye huangalia vitu vidogo vidogo
kuona kama vipo sawa katika hali inayokubalika viwe.
Pamoja na kuwa na ratiba yenye changamoto sana (Yeye ni Balozi wa WildAid
na yumo ndani ya bodi kadhaa; mama wa watoto pacha wavulana; mke kwa
mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na akiendesha taasisi ya hisani
ya elimu), Ntuyabaliwe huhakikisha anakagua kila samani inayozalishwa
kiwandani kwake kabla ya kuuzwa au kusafirishwa.
“Napenda kitu bora chenye uhakika!” anasema mlimbwende huyo wa zamani wa Tanzania ambaye pia ni mwanamuziki.
“Kila kitu tunachokifanya
Molocaho lazima kiwe chenye uhakika hakina makosa wala dhaifu, lazima
kiwe kimetulia,” anasema mrembo huyo.
“Tunashindana na watu maarufu duniani wanaofanya vyema kwa hiyo kama sisi tusipofanya vyema kuliko wao tutashindwa,” aliongeza.
The Crown Chair by Molocaho
Ntuyabaliwe, mzaliwa wa Tanzania,
aliyefunzwa kubuni uzuri wa ndani, ni mwanzilishi na mbunifu mkuu wa
Molocaho by Amorette, kampuni ya Tanzania inayojishughulisha na
utengenezaji wa samani bora kwa namna mteja anavyohitaji, samani, nyuzi,
taa, urembaji, samani za nje na kwenye bustani.
Molocaho inatengeneza samani
zenye mahadhi ya kiafrika ikichanganya utamaduni wa Tanzania katika
mazingira ya kisasa na kumalizia na ubunifu wa kimataifa.
Molocaho, moja ya makampuni ya
Afrika Mashariki ya samani yanayokua kwa kasi, imejipatia nafasi kubwa
ya heshima kwa kuhakikisha kwamba inatumia mali ghafi na mbao njema
pekee za Tanzania kutengeneza samani zenye kwenda kimataifa.
“Mpango wetu mkubwa ni kujenga nembo ya biashara ya samani za Tanzania inayotambulika kimataifa.
Ni dhahiri itatuchukua muda
kufikia huko , lakini tumedhamiria,” alisema wakati tukizunguka naye
katika duka kubwa la maonesho la Molocaho lililopo eneo la Masaki jijini
Dar es Salaam.
Ntuyabaliwe ni mojawapo ya watu
wanaotambulika kirahisi kabisa nchini Tanzania. Mwaka 2000 alishinda
taji la urembo la Miss Tanzania na kuiwakilisha Tanzania katika shindano
la ulimbwende la dunia ( Miss World). Baada ya muda alipata heshima ya
kuwa mmoja wa wanamuziki mahiri na kuweza kutoa nyimbo kadhaa
zilizoshika chati Afrika Mashariki.
Pamoja na kuwa mlimbwende na mwanamuziki anasema mapenzi yake makubwa ni ubunifu wa uzuri wa ndani wa nyumba.
“Mimi ni mbunifu kutoka moyoni,” anasema.
“Kwa namna ninavyokumbuka, mimi
ninavutiwa na ubunifu wa ndani na wa samani, sanaa na fasheni na
nimekuwa mwanafunzi bora kabisa wa masuala ya ubunifu na historia yake.
Kama mtoto mara zote nilikuwa nachora vitu mbalimbali. Ni mojawapo ya
vitu ninavyovifanya kwa raha kubwa.”
Wakati muziki wake unakamata chati akajiona amekinai na hivyo kuingia katika awamu nyingine ya maisha yake.
Alitoka na kwenda shule
Uingereza. Huko alienda kujifunza ubunifu wa ndani na lengo kubwa ni
kuboresha weledi katika hilo na mwaka 2012 alianzisha kampuni ya
Amorette, yenye makao makuu Dar es Salaam iliyokuwa inajishughulisha na
masuala ya urembaji wa ndani.
Amorette imepata mafanikio
makubwa na Ntuyabaliwe amekuwa akifanya kazi na watu wengine wenye
kaliba ya juu katika masuala ya ubunifu wawe binafsi au makamapuni ya
kimataifa nchini Tanzania, akichanganya mawazo na ubunifu wao
kutengeneza bidhaa zenye kaliba ya juu katika ubunifu, staili, rangi ili
wateja wake wawe na maisha mazuri ama majumbani mwao au katika
mazingira yao ya kazi.
Na katika muda wote wa kufanya hayo, mjasiriamali huyu alikuwa na tabia ya kuchora muonekano wa samani.
“Napenda samani , sijui kwanini
labda kwa sababu ya kazi yangu ya ubunifu wa maeneo ya ndani, lakini
nadhani ni kwa kuwa naamini samani zako zinakuonesha wewe ni mtu wa
namna gani. Awali nilitengeneza michoro ya samani kwa ajili ya kujenga
ubunifu tu, lakini mara nyingi mume wangu huangalia michoro hiyo na
kunipongeza. Alikuwa akisema kwamba situmii vyema kipaji changu. Mara
nyingi amekuwa akinihimiza kujikita katika usanii na kuanzisha kampuni
ya kushughulika nao,” anasema Ntuyabaliwe akikumbuka alivyoanza.
Mume wake, Dkt.Reginald Mengi, ni
tajiri mwenye mafanikio makubwa nchini Tanzania ambaye ameujenga
utajiri wake kwa kufanya karibu kila kitu kuanzia uzalishaji wa kinywaji
cha Coca-Cola hadi uchimbaji wa madini na kumiliki vituo vya
televisheni na magazeti.
“Ukiwa na mume mwenye mafanikio
makubwa namna hii, unashawishika kusaka mafanikio. Kwa hiyo
nikatengeneza mpango biashara, kuanza kuajiri wafanyakazi na hivyo
kuiweka hai ndoto yangu.”
Amorette, ikiwa ni chata yenye
mafanikio makubwa miongoni mwa watu wa daraja la juu nchini Tanzania na
huku ikipanda kwa kasi na watu wakiifuata, Septemba 2016 Ntuyabaliwe
alizindua Molocaho by Amorette kama kampuni ya kubuni na kutengeneza
samani. Miezi michache tu tangu kuundwa kwake kampuni imefanya vyema na
inaonekana kunedelea kukua kimafanikio.
“Tumekuwa katika pilikapilika
sana,” anasema na kuongeza: ” Sikuwa natarajia kufanya biashara kama
tulivyofanya katika miezi michache iliyopita.”
Ntuyabaliwe ndiye mbunifu mkuu wa
Molocaho. Akitumia ufundi wa asili katika mazingira ya sasa,
Ntuyabaliwe hubuni na kutengeneza samani za kuvutia kwa ajili ya
majumbani na maofisini na hata kwa watu binafsi.
Ukiangalia samani za Molocaho
utabaini uzuri wake kusukwa kwa namna rahisi lakini yenye hisia kali na
hivyo kufanya ubunifu wake kuwa wa bashasha , uliotulia na wenye
kutuliza kiu. Lakini ukiangalia kwa karibu zaidi utabaini kwamba kile
unachokiona rahisi ni tata, kimeumbwa kwa namna ambayo ni makini na
yenye ugumu wa aina yake kwa lengo la kukupatia kitu bora kabisa.
Hivyo ndivyo Ntuyabaliwe
anavyotaka unapoangalia samani zake yaani unaziona za kawaida lakini
zenye uzuri na ubora wa hali ya juu.
Kwa Ntuyabaliwe,ubunifu wa samani
za Molocaho unatokana na wakati mwingine na mambo ambayo hukuyatarajia
kabisa. Wakati mwingine tukio asili linaweza kabisa kusababisha ubunifu
wa aina Fulani.
Mathalani tukio la radi (mwale na
mlipuko) ndio uliotengeneza kiti kinachoitwa radi ambacho kimefanya
vyema katika mauzo ya ndani na nje.
Katika kiti hiki sehemu ya kuegemea kuna mwale wa radi.
Molacaho hutengeneza vitu kwa namna ambavyo mteja anataka na maana yake kazi zake nyingi ni za oda.
“Wateja wetu huangalia kitabu
chetu cha aina mbalimbali za samani kisha wanachagua wanachotaka na
kutueleza kitu gani cha ziada wanataka kiwepo. Na hapa huwa tunafanya
mazungumzo na wateja wetu ili tuweze kufahamu hasa wanachofikiria na
wanachohitaji,” anasema Ntuyabaliwe.
Samani zinazotengenezwa kutokana na maagizo kwa kawaida ni gharama kwa kuwa hutengenezwa kwa mahitaji ya mteja.
Ntuyabaliwe anakiri kwamba
Watanzania wengi hawana uwezo wa kununua bidhaa zake. Wengi wa
watanzania ni maskini; Bidhaa za Molacaho zinaanzia kokote kule kuanzia
dola za Marekani 250 kama stuli hadi dola za Marekani 6,000 kwa kitanda.
“Bidhaa zetu zimepambanua wateja,” anasema na kuongeza kwamba wao si rahisi lakini pia si ghali sana.
“kazi zetu si rahisi sana na wala
si ghali sana hapa mjini. Mwishoni wa siku huwa tunapata taarifa kutoka
kwa wateja wetu kwamba tuna bei nzuri kulinganisha na bidhaa
tunazotengeneza.”
Wakati Ntuyabaliwe anatengeneza
fedha amesema pia anatengeneza mfumo wa kuwaendeleza mafundi nchini
Tanzania. Mapema mwaka huu, Amorette, kampuni yake inayoshughulika na
ubunifu wa masuala ya ndani ilianzisha programu ya kusimamia mafunzo kwa
mafundi wa hapa Tanzania.
Lengo kuu ni kuwafanya mafundi wa Tanzania kufikia uwezo wa kubuni na kutengeneza bidhaa zenye hadhi ya kimataifa.
Chini ya programu hii, mafundi
ambao tayari wana ujuzi na kufanya shughuli za useremala au kitu
kinachofanana na hicho wanapewa mafunzo ya miezi miwili na mafundi
wanaotambulika kimataifa.
Nia ni kuhamisha maarifa, ujuzi
na teknolojia kutoka kwa wataalamu hao wa kimataifa na kuwawezesha
watanzania kubadilika katika utendaji.
Molocaho pia wamejikita katika
kuhifadhi mazingira kwa kuhakikisha kwamba hakuna wanachotupa
kinachotokana na mchakato wa kutengeneza samani.
Kampuni hii hutumia bidhaa za
mbao kutoka katika vyanzo mbalimbali na pia inaunga mkono kampeni
mbalimbali za upandaji miti nchini Tanzania.
“Mwishoni mwa siku biashara si tu
iwe inayoleta faida lakini pia lazima ijali maslahi ya jamii ambapo
biashara hiyo ipo,” anasema.
Leo hii, Molocaho imeajiri zaidi
ya wafanyakazi wa kudumu 30 huku wakiwa katika njia nzuri ya kutengeneza
faida katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwake.
“Hakika tumeanza,” anasema
Ntuyabaliwe wakati tunaondoka katika duka la Molocaho. “Tutaendelea
kumkuza mtoto huyu ili siku moja awe kampuni kubwa. Wewe tufuatilie tu”
Imeandikwa na Mfonobong Nsehe , wa Forbes na kutafsiriwa kwa wasomaji wa Kiswahili na Mzige Media kupitia TheBeauty.co.tz
No comments:
Post a Comment