Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akimsikiliza kwa
makini mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo Africa
(AfDB), Bi, Lekhethe Mmakgoshi (wa pili kushoto), wakati alipokutana na
Bodi hiyo jijini Dar es salaam leo kujadiliana namna ya kushirikiana
kuboresha sekta ya miundombinu ya uchukuzi hapa nchini.
Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa
Barabara nchini TANROADS Eng. Crispinius Ako wa (tatu kushoto),
akifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya
Maendeleo Africa (AFDB), walipotembelea Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasiliano kubadilisha uzoefu katika maseuala ya miradi ya ujenzi wa
miundombinu jijini Dar es Salaam leo.
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto ), akifafanua jambo
kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo Africa (AfDB),
bi, Lekhethe Mmakgoshi, Dkt. Weggoro Nyamajeje na Dkt. Bright Okogu (wa
kwanza kulia), alipokutana na Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo
kujadiliana namna ya kushirikiana kuboresha sekta ya miundombinu ya
uchukuzi hapa nchini.
Picha ya pamoja kati ya viongozi
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) walipokutana Jijini
Dar es salaam leo.
……………………….
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameiomba Bodi ya Wakurugenzi wa Benki
ya Maendeleo Africa (AfDB), kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika
mkakati wake wa kukuza uchumi kwa kuwekeza katika sekta ya miundombinu.
Akizungumza na Wakurugenzi wa Bodi
ya AfDB waliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Prof.
Mbarawa ameishukuru benki hiyo kwa ushirikiano inaoipa Serikali ya
Tanzania katika miradi mingi ya ujenzi wa barabara na kuiomba kuiunga
mkono katika uwekezaji mkubwa inaoufanya katika miradi ya usafiri wa
anga na reli.
“Tumejipanga kukuza uchumi kwa
kuimarisha sekta za barabara,anga,reli na bandari hivyo tunaomba
ushirikiano wenu kadri tunavyouhitaji ili kufikia malengo yetu kwa
wakati”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameitaja baadhi ya miradi ya
barabara ambayo Tanzania imenufaika na AfDB kuwa ni barabara ya
Kibondo-Kasulu-Manyovu Km 250, Makutano-Nata-Mugumu-Mto wa Mbu hadi
Loliondo Km 213, Makurunge-Saadani-Pangani-Tanga KM 178 na barabara za
pete jijini Dar es Salaam Km 34.
“Kuimarika kwa Sekta ya
miundombinu nchini hasa sekta ya anga, reli na barabara, kutaimarisha
sekta za utalii na kilimo na hivyo kuongeza ajira na kukuza uchumi wa
taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye mjumbe wa Bodi ya AfDB Dkt.
Weggoro Nyamajeje Calleb amezungumzia umuhimu wa miradi ya ujenzi
inayoanzishwa hapa nchini kutoa fursa za ajira kwa wananchi na kuwekewa
mazingira endelevu ili ilete mabadiliko chanya katika maisha ya watu na
taifa kwa ujumla.
Dkt. Calleb amesisitiza umuhimu
wa ushirikishwaji wa sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ili
kuiwezesha nchi kuwa na miundombinu bora na yakutosha na hivyo kuchochea
maendeleo.
Ujumbe wa AfDB upo hapa nchini
ambapo pamoja na mambo mengine leo umepata fursa ya kubadilishana uzoefu
na viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili kujua
mikakati yake katika kuboresha miundombinu hapa nchini na namna
inavyoweza kutoa ushirikiano katika kuiwezesha.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment