*Aagiza akiba iliyopo itunzwe hadi msimu ujao wa mavuno
* RC, Ma-DC, Ma-DED waagizwa kuelimisha umma utunzaji wa chakula
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi
ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo
iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.
Ametoa agizo hilo jana jioni
(Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa
NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma
mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo
hicho.
Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya
tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini
ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha
inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.
“Angalieni ninyi wenyewe hali ya
joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu
na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa
mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka.”
“Kama mvua haijanyesha hadi leo,
ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea
kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu
kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na
ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha
chakula,” alisisitiza.
“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo
na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi
tutakapoamua vinginevyo,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa
NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba
msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima
lakini hadi kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3
zenye thamani ya sh. bilioni 5.28.
Alisema kanda ya Songea ni
miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo inahudumia mkoa wa
Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote nchini kuwa ni
Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.
“Kanda ya Songea inayo maghala
sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka. Lakini hivi sasa
kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa Hifadhi (NFRA
Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa
kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.
“Kanda ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos
12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili yenye uwezo
wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani
56,000 mradi huu utakapokamilika.”
Alisema kukamilika kwa mradi huo,
kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 85,000
ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.
Alipolizwa ni kwa nini hawajaweza
kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma alisema
kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani
wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza
(kawaida ni Julai mosi kila mwaka).
“Kuimarika kwa barabara za mkoa
kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo kuwawezesha
wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia sokoni
na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.
Alisema changamoto nyingine
inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima ambao
alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula
na biashara. “Ubora hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye
nafaka zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na
takataka,” alisema.
Waziri Mkuu leo anatembelea wilaya
ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme katika kijiji cha Mtepa,
atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako pia atazungumza na watumishi
wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia
atakagua shamba la miti la TFS katika kijiji cha Wino.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 5, 2017.
No comments:
Post a Comment