Pages

Tuesday, January 3, 2017

WASIMAMIZI UCHAGUZI MDOGO ZINGATIENI SHERIA KANUNI NA MAADILI, MSIKUBALI KUYUMBISHWA NA MTU


odo
 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw.kailima Ramadhani akifungua mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma.
odo-2odo-3odo-4
Baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao wakati wa Uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017 leo mjini Dodoma.

Picha na Aron Msigwa – NEC.
…………..
Na.Aron Msigwa – NEC
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi
wa Uchaguzi mdogo wa Udiwani utakaofanyika katika Kata 20 za Tanzania
Bara na Ubunge katika jimbo la Dimani Visiwani Zanzibar  Januari 22,
2017 kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ili Uchaguzi huo uwe Huru na
wa Haki.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhan wakati akifungua mafunzo ya siku 3 ya
Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya
jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi Kailima amewataka Wasimamizi hao kuzingatia matakwa ya
Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali katika kushughulikia
mambo yatakayojitokeza wakati wa uchaguzi huo.
Katika kutimiza majukumu yao wawe tayari kutoa ufafanuzi juu masuala
mbalimbali kwa kuzingatia sheria na kutokuwa tayari kukubali
kuyumbishwa na mtu yeyote atakayekiuka  miongozo, sheria na kanuni za
Uchaguzi.
Amewataka Wasimamizi hao watende mambo yote kwa kuzingatia kanuni na
Sheria na kutoa maamuzi sahihi kwa mustakabali wa Taifa na
kuwasisitiza kuepuka kutoa upendeleo katika maamuzi wanayoyafanya  na
wasikubali kuyumbishwa na matakwa ya baadhi ya watu.
 Amewaeleza kuwa milango ya Tume iko wazi pale watakapohitaji
ufafanuzi huku akitoa wito kwa Wasimamizi hao kuwasiliana na watendaji
wa Tume katika mambo yanayowatatiza ili wapate ufafanuzi.
Aidha, amewataka wawe makini na hatua ya utangazaji wa matokeo kwa
kutoa taarifa kwa wananchi mara kwa mara juu ya hatua zinazoendelea
vituoni wakati wa ukusanyaji wa matokea ili kuwaondolea wasiwasi pindi
wanapoona matokeo yamechelewa kutolewa.
” Hili naomba nilisisitize, mnapoona baadhi ya taratibu hazijakamilika
tokeni nje muwaambie wananchi nini kinaendelea ili wawe na taarifa na
hii itawaongezea imani wananchi wanaosubiri matokeo na kuepusha vurugu
vituoni” Amesisitiza Bw.Kailima.
Amesema kuwa mfumo wa Uchaguzi wa Tanzania ni wa uwazi kwa kuwa kila
chama kinakuwa na Wakala anayesimamia maslahi ya chama chake wakati wa
uchaguzi, pia uwazi katika hatua zote za uchaguzi ikiwemo upigaji wa
kura, uhesabuji wa Matokeo na ujumlishaji wa matokeo ambayo
hulinganishwa na vishina.
Kwa upande wa Mawakala wa Vyama vya Siasa watakaoshiriki katika
Uchaguzi mdogo amesisitiza kuwa wanatakiwa kuzingatia maadili ikiwemo
kuepuka kutoa matokeo ambayo hawajaruhusiwa kuyasema wakati wa zoezi
la upigaji wa kura na wanatakiwa kuapa kiapo cha kutunza siri na
kujaza fomu kwa mujibu  matakwa ya kikanuni.
” Wakala Chama cha Siasa haruhusiwi kutangaza matokeo kwa mgombea wake
wakati zoezi la kuhesbu kura likiendelea kituoni, na hili
nalilisisitiza Mawakala wote ni lazima waape kiapo cha kutunza Siri,
ni matakwa ya  kikanuni, wakala asiyeapa na kujaza fomu asipewe ridhaa
ya kuwa wakala wa chama cha siasa ndani ya kituo” Amesisitiza Bw.
Kailima.
Amesema kila Chama kitakuwa na Mawakala wa aina tatu kwa maana ya
Wakala wa Kupiga kura, Wakala wa kuhesabu kura, Wakala wa kujumlisha
kura na Kutangaza Matokeo ambao watakua na jukumu la kulinda maslahi
ya vyama vyao na wagombea wawapo kituoni, kumsaidia msaidizi wa kituo
pamoja na kuangalia taratibu zinavyokwenda kituoni.
Amesisitiza kuwa maamuzi ya kituo yatatolewa na Msimamizi wa kituo na
Wakala ambaye hatakubaliana na maamuzi hayo atajaza fomu namba 16
kuonyesha kuridhika au kutokuridhika.
Kuhusu mafunzo amesema yanalenga kuwajengea uwezo Wasimamizi wa
Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na
Maafisa Uchaguzi kuelewa Misingi, Sheria na Wajibu wa namna bora ya
kutekeleza majukumu yao katika usimamizi wa  hatua zote za uchaguzi
ikiwemo upigaji wa kura na utangazaji wa matokeo.
Ameongeza kuwa Wasimamizi na Waratibu hao watafundishwa maadili ya
kuzingatia wakati wakitekeleza majukumu yao ikiwemo maadili ya
uchaguzi,maelekezo kwa wasimamizi ya Uchaguzi, wajibu wao, majukumu ya
makarani , taratibu za kupiga kura, kuhesabu kura, kujumlisha kura na
kutangaza matokeo, kuandaa taarifa za uchaguzi pamoja na masuala
mbalimbali kuhusu uchaguzi huo.
Akizungumzia kuhusu Rufaa za mapingamizi ya wagombea amesema kuwa kwa
mujibu wa kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za
Mitaa Sura ya 292, Tume ilipokea Rufaa  za wagombea kutoka Kata
mbalimbali ikiwemo ya Kijichi – Manispaa ya Temeke, Misugusugu-
Halmashauri ya mji Kibaha, Pwani na Kata ya Ihumwa  Manispaa ya
Dodoma.
Amesema katika kikao cha Tume cha Desemba, 30, 2016 Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ilitoa   maamuzi ya Rufaa zote kwa haki na  kwa kuzingatia
kanuni, taratibu, miongozo na sheria zinazosimamia  Uchaguzi ikiwemo
Rufaa ya Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambayo
imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa mwenyewe na amejitoa katika
ugombea Udiwani kabla Rufaa yake haijasikilizwa.
 Kwa Upande wa Rufaa ya jimbo la Dimani, Zanzibar Bw. Kailima ameeleza
kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 40 (6)
ilipokea Rufaa ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi ya kupinga maamuzi ya
Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kumthibitisha mgombea wa Chama cha
Wananchi CUF kwamba ni mgombea halali katika uchaguzi mdogo wa jimbo
la Dimani, Zanzibar.
Bw. Kailima ameeleza kuwa katika kikao cha Maamuzi cha Tume cha
kupitia Rufaa za wagombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikubaliana na
Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kuwa mgombea wa Chama
cha Wananchi CUF aliyewekewa pingamizi na mgombea wa CCM amekidhi
vigezo na uteuzi wake ni halali hivyo anaweza kuendelea na kampeni za
kugombea nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo.
” Napenda nisisitize kuwa maamuzi yote yaliyofanywa na Tume
yamezingatia Kanuni, Taratibu, Sheria na miongozo inayosimamia
chaguzi, hali hii ya wagombea kukubali maamuzi ya Tume inatujengea
msingi imara wa kuendelea kufanya vizuri zaidi kuelekea kwenye
Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 huku tukitimiza majukumu yetu kwa mujibu wa
sheria bila kupendelea” Amesisitiza Bw.Kailima.

No comments:

Post a Comment