Mwenyekiti
wa Chama cha Wahudumu wa Baa Tanzania (Chawabata), Ali Hussein (kulia),
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akipinga
zoezi linalofanywa na Manispaa ya Ilala la kukagua leseni za wauza vileo
usiku. Kushoto ni Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck.
Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck akitoa ufafanuzi
katika mkutano huo.
Na Dotto Mwaibale
CHAMA
cha Wahudumu wa Baa Tanzania (Chawabata) kimepinga zoezi linalofanywa na
Manispaa ya Ilala la kukagua leseni za wauza vileo usiku.
Akizungumza
Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa chama hicho, Ali Hussein alisema
zoezi hilo linawatisha wateja wanapokuwa wakipata vinywaji katika baa
mbalimbali.
Hussein alisema chama hicho kimepokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa baa ambao ni wanachama wao.
Alisema
wiki moja kabla ya kuanza kwa sikukuu za mwishoni mwaka maofisa
biashara wa Manispaa ya Ilala walikuwa wakipita katika baa mbalimbali
maeneo ya Ukonga na vitongoji vyake kuanzia saa mbili usiku kukagua
leseni.
Alisema maofisa hao walikuwa wameongoza na askari polisi waliokuwa na bunduki jambo ambalo kiusalama sio zuri.
“Huu
utaratibu wa kukagua leseni usiku na mtutu wa bunduki unaweza kutoa
fursa kwa wahalifu nao kwenda kwenye mabaa na kujifanya ni maofisa
biashara na kufanya uporaji tunaomba serikali kuliangalia jambo hili”
alisema Hussein.
Alisema
hali hiyo imejitokeza baada ya serikali kuzuia baa kufunguliwa asubuhi
kama ilivyokuwa awali ambapo chama hicho oktoba mwaka jana kiliiomba
serikali kupitia mtandao huu na katika vyombo vya habari kuruhusu
kufunguliwa kwa baa wakati wote ili kutoa nafasi ya wauza vileo kufanya
biashara na kuweza kukusanya fedha za kulipa kodi ya serikali.
Alisema
kwa nyakati za mchana ni vigumu kukuta baa zikiwa wazi na ndio maana
maofisa hao wameamua kwenda usiku kukagua leseni hizo jambo ambalo ni
hatari kwa wateja na maofisa hao
“Muda
wa kufungua baa kuanzia saa 10 jioni unawaathiri wateja wetu kwani kwa
masaa matano ya kufanyabiashara ya vileo na vinywaji vingine ni mchache
mno” alisema Hussein.
Alisema
hatua hiyo ya serikali ya kuamuru baa kufunguliwa kuanzia saa 10
imeathiri wahudumu wa baa ambao wengi wao wamepunguzwa kazi ambapo
wanaiomba serikali kuangalia jambo hilo.
Meneja
wa Baa ya Serengeti iliyopo eneo la mabaa Banana katika manispaa hiyo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Emanuel alisema kitendo cha maofisa
hao kukagua leseni za biashara usiku ni kigeni kwao na kinawatisha
wateja wao ambapo ameomba manispaa kuangalia upya muda wa kufanya
ukaguzi huo.
Ofisa
Habari wa Manispaa ya Ilala, Neema Njau alisema zoezi hilo lipo kisheria
na linafanywa na kamati maalumu iliundwa na manispaa hiyo ambayo ipo
chini ya wakuu wa polisi wa wilaya hiyo.
“Ukaguzi
wa leseni hizo hauwezi kufanyika mchana kwa kuwa baa nyingi zinakuwa
zimefungwa lakini wasiliana na ofisa biashara wa manispaa atakupa
maelezo mazuri zaidi” alisema Njau.
No comments:
Post a Comment