Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA
Kuu ya Tanzania imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa kupinga sheria ya
mtandao iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka
2015 ili kulinda maslahi ya Taifa ya kupambana na kutoa mwelekeo wa
kukabiliana na makosa ya mtandao.
Hukumu
hiyo ya kihistoria ilitolewa na jopo la majaji watatu, Prof. John
Ruhangisa, Winfrida Korosso na Lugano Mwandambo mara baada kuona hoja
zilizowalishwa na wakili wa kujitegemea Jebra Kambole kuwa hazina
msingi.
Hata
hivyo, mahakama hiyo imetoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kufanya marekebisho kwenye kifungu kimoja kati ya 18 vya sheria hiyo
vilivyokuwa vikilalamikiwa kwa vile kifungu hicho kinakiuka haki ya
msingi ya mwananchi ya kusikilizwa.
Pamoja
na kutoa maelekezo hayo, mahakama imeona vifungu vingine ndani ya
sheria hiyo havikuwa na mapungufu yoyote ya kikatiba kama ilivyokuwa
inadaiwa na mwombaji (Kambole).
Katika
malalamiko yake, Kambole alidai kuwa Sheria ya mtandao ilikuwa na
baadhi ya maneno ambayo hayakutafasiriwa ambavyo kwa namna moja au
nyingine vingeweza kuchambuliwa vibaya na vyombo vya usalama na hivyo
kumwonea mwananchi.
Hata
hiyo, jopo la majaji hao waliona hoja hizo hazina mashiko mara baada ya
kupitia kwa kina vifungu vya Sheria husika na kuona kuwa vifungu hivyo
lalamikiwa vinaainisha kosa ambalo linaweza kutendeka na kutoa adhabu
inayotakiwa.
Majaji
hao wamebainisha kuwa vifungu namba 4, 5, 6, 7, 8, 9, 14, 19, 21 na 22
vya sheria ya mtandao vilivyolalamikiwa vinaenda sambamba na Ibara ya 17
(2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo haviwezi
kwenda kinyume na katiba.
Kwa
mujibu wa jopo hilo, mwananchi anayonafasi ya kupinga maamuzi
yanayotolewa na kiongozi kwa kupeleka maombi ya mapitio (judicial
review) mahakama kuu kama itabainika kuwa alienda kinyume na madaraka
yake aliyopewa kisheria.
Mara
baada ya kufikia uamuzi kuwa vifungu hivyo vya sheria ya mtandao
havikinzani na Ibara ya 17 (2), 20 (5) na 30 (2) vya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, majaji hao walikataa wito wa mlalamikaji wa
kuviona vifungu hivyo vinakiuka katiba.
Kambole
katika maombi yake alilalamikia pia vifungu namba 38 na 50 vya sheria
ya mtandao kwamba vinakiuka Ibara ya 13 ya Katiba juu ya mwananchi kuwa
na haki ya kusikilizwa.
Mlalamikaji
huyo alidai kuwa kifungu namba 38 kinatoa uhuru kwa mamlaka kupeleka
maombi mahakamani ambayo yanaweza kusikilizwa kupitia upande mmoja bila
upande wa pili katika maombi hayo kuhusishwa.
Hata
hivyo, majaji hao walibainisha kuwa kifungu hicho kinahusiana na
maswala ya kufanya upekuzi, kukamata, kukusanya na kuweka wazi takwimu
kwa lengo la upelelezi. Katika mazingira hayo, majaji waliona kuwa
malalamiko yaliyotolewa hayakuwa na msingi wowote kwa vile maswala ya
upelelezi hayatoi ukomo katika kutatua haki ya mwananchi.
No comments:
Post a Comment