Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Katika kukabiliana na athari za
ukame, Serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa hali ya
chakula na lishe ni imara nchini.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi Dkt. Charles Tizeba ameyasema hayo leo Mjini, Dodoma katika
Kikao cha Bunge alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya
chakula na lishe kwa mwaka 2016/2017
.
“Tathimini imebainisha kuwa
Halmashauri za wilaya 55 zinahitaji jumla ya tani 1,969 za mbegu bora za
mahindi, mtama na mizizi inayokomaa kwa muda mfupi na kustahimili
ukame,” alifafanua Dkt. Tizeba.
Aliendelea kwa kusema kuwa mbegu
hizo zinahitajika ziwafikie mwezi Februari 2017 iliziweze kupandwa
katika msimu wa 2016/2017 katika maeneo yanayoendelea kupata mvua wakati
huu wa mwaka.
Dkt. Tizeba alizitaja hatua ambazo Serikali inazichukua kuhakikisha kuwa hali ya chakula na lishe ni imara kuwa ni pamoja na;
Kusimamia usambazaji wa mbegu za
mazao ya kilimo zinazostahimili ukame na zinazozaa kwa muda mfupi ambazo
ni pamoja na mtama, uwele na mbegu za mazao aina ya mizizi za mihogo na
viazi vitamu ili kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha sasa.
Kuhamasisha wakulima kupanda
mazao aina ya mizizi, mtama na uwele kwa maeneo yanayopata mvua za
masika ambazo zinaendelea kunyesha na mawakala wa pembejeo pamoja na
vivutio vya utafiti vilivyopo katika kanda mbalimbali hapa nchini.
Vile vile Serikali kupitia Wakala
(NFRA) inaendelea kuhifadhi kwa uangalifu chakula kilichopo ili
kitumike pale kitakapohitajika.
Hatua nyingine ni Kuhamasisha
sekta binafsi kununua mazao ya chakula katika maeneo yaliyo na ziada na
kuyauza katika maeneo yenye uhaba wa chakula. Aidha wafanyabiashara
waliohifadhi mahindi wanaombwa kusambaza chakula hicho katika masoko ya
ndani ya nchi ili kupunguza mfumuko wa bei.
Aidha Serikali inaendelea
kuhimiza usindikaji wa mazao ya chakula kwa kuyaongezea thamani na
kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhiimu wa kula vyakula vya aina zote.
Dkt. Tizeba amesema kuwa kutokana
na hali ya mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli na msimu kutoridhisha
katika maeneo mengi ya nchi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanashauriwa
kuendelea kuhamasisha na kusimamia wakulima kutuma mbegu zinazokomaa
mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame.
Aidha Serikali imewataka
wakulima kuendelea kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda
mazao yanayostahimili ukame na kukomaa kwa muda mfupi na pia waendelee
kutunza na kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu.
No comments:
Post a Comment