Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa licha
ya Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati, Maji na Mafuta (EWURA)
kuridhia ombi la TANESCO la kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari
mosi,2017 bei ya umeme haitapanda.
Rais Dkt. Magufuli amezungumza
hayo leo Jumapili ya Januari Mosi, 2016 wakati wa Ibada katika Kanisa
la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma,Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Bukoba
anapoanza rasmi ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kagera.
Rais Magufuli ameshangazwa na
kitendo cha watendaji waliopandisha bei ya umeme bila hata ya
kushauriana na yeye, Makamu wa Rais,Waziri Mkuu au Waziri mwenye dhamana
ya Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo na hivyo kumshukuru Waziri
Muhongo kwa kutengua maamuzi hayo.
”Ninamshukuru sana Waziri wa
Nishati na Madini kwa maamuzi ya kusitisha hayo kwa hiyo umeme hakuna
kupanda bei,haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa
katika mikakati mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka vijijini,na
umeme huu unaenda kwa watu masikini walioumbwa kwa mfano wa Mungu halafu
mtu pekee kwa sababu ya cheo chake anapandisha bei,hili haliwezekani”
Alisema Rais Dkt. Magufuli.”
Aidha, Rais Dkt Magufuli
ameendelea kuwataka watanzania katika mwaka huu mpya 2017 kuendelea
kufanya kazi kwa bidii kama maandiko matakatifu yanavyoelekeza kuwa
asiyefanya kazi na asile badala ya kulalamika kuwa fedha zimepotea.
Kwa upande wake,Askofu Msaidizi
Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu Methodius Kilaini,akitoa mahubiri kwa
waumini waliohudhuria ibada hiyo amempongeza Rais Dkt Magufuli kwa
uongozi wake imara,huku akisema kupungua kwa urasimu katika ofisi za
umma kunatokana na utendaji kuongezeka na kuwataka wana Kagera na
Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa
bidii na uaminifu.
Mara baada ya Ibada ya Misa
Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu
Desderius Rwoma,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli aliwatakia heri ya mwaka mpya waumini wa kanisa hilo na
watanzania kwa ujumla.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
01 Januari, 2017
No comments:
Post a Comment