Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumatatu Januari mbili, 2017
amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Kagera kwa kuwatembelea baadhi
ya wananchi walioathiriwa na tetemeko la ardhi pamoja na kukagua baadhi
ya miundo mbinu iliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuweka jiwe la msingi
la ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari ya Ihungo Omumwani
iliyobomolewa na tetemeko la ardhi la Septemba 10,2016.
Mara baada ya ukaguzi huo Rais
Dkt Magufuli akazungumza na wananchi wa Mkoa huo wa Kagera katika
viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ihungo na kuagiza kuvunjwa kwa kamati
ya maafa ya Mkoa huo iliyokuwa ikiratibu utoaji wa misaaada na kufanya
tathmini ya athari ya tetemeko hilo.
”Kila kitu huwa kina mwanzo
na mwisho wake ukiwa na harusi huwa kuna kamati ya harusi,ukishamaliza
kufunga ndoa kamati ya harusi huwa inavunjwa,na ukiwa kwenye msiba huwa
kuna kamati ya msiba na msiba mkishazika kamati ya mazishi
huvunjwa,kamati ya maafa ya Kagera huu ni mwezi wa tano na inawezekana
hata kwenye kamati huwa wanalipana posho,sasa nataka hii kamati nayo
iishe,yalishapita yamepita”
Aidha Dkt Magufuli amewataka wote
walioahidi kuchangia katika kamati ya tetemeko la ardhi ya mkoa wa
Kagera ambao bado hawajatekeleza ahadi zao ambazo ni jumla ya shilingi
bilioni nne nukta tano wakamilishe ahadi hizo ili ziweze kumalizia
miundombinu ya Serikali iliyoathiriwa na tetemeko hilo.
Ameongeza kuwa wale wote
wanaoendelea kuguswa kusaidia wapeleke michango yao moja kwa moja kwa
wananchi badala ya kuipeleka serikalini kwa kuwa hakuna mchango mwingine
utakaopokelewa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pia Rais Dkt Magufuli ameagiza
shule ya Sekondari ya Omumwani iliyokuwa inamilikiwa na Jumuia ya Wazazi
wa Chama Cha Mapinduzi CCM imilikiwe na Serikali kutaka wanafunzi wote
wanaosoma katika shule hiyo kutolipa ada kama zilivyo shule nyingine za
serikali.
Dkt Magufuli ameuagiza uongozi wa
Mkoa wa Kagera kupunguza utitiri wa kodi katika zao la kahawa ili bei
ya zao hilo ipande na kuwanufaisha wakulima
Balozi wa Uingereza hapa Nchini
Bi Sarah Cooke ambaye nchi yake imechangia kiasi cha shilingi bilioni
sita kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Ihungo, amempongeza
Rais Dkt Magufuli na serikali yake kwa jitihada za kupambana na rushwa
suala ambalo nchi yake ya Uingereza inalipa kipaumbele sambamba na kutoa
elimu bila malipo jambo linalowawezesha watoto wengi wa kitanzania
kupata elimu bure
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
02 Januari, 2017
No comments:
Post a Comment