WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameagiza walimu wanaishi mbali na shule wakati shule zao zina majengo
wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba za shule.
Amesema haifai kuacha walimu
waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo inachangia uchelewaji
kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia jioni
pale wanapohitajika kufanya hivyo.
Ametoa agizo hilo wakati
akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata ya Mbekenyera,
wilayani Ruangwa jana mchana (Ijumaa, Desemba 30, 2016) kwenye mkutano
uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.
“Nimeambiwa kuwa walimu wako
wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi walimu. Mbona
wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati hawana
magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo, walimu wote
warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo,”
amesisitiza.
“Uamuzi wa walimu kuishi jirani na
shule ulifikiwa ili mwalimu awepo na kuwasimamia wanafunzi wakati
wakifanya usafi na wakati mwingine aweze kutoa msaada kwa wanafunzi
wanaojisomea jioni pindi wakihitaji msaada au ufafanuzi,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue
asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu
walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna
upungufu wa walimu.
Amesema ili kusaidia juhudi za
Serikali za kuboresha elimu nchini, ni vema kila kijiji kikaweka
utaratibu wa kuchangia matofali ili iwe rahisi kuanza ujenzi wa nyumba
za walimu.
Akiwa katika kijiji cha
Mkutingome, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa
aliwahamasisha wakazi wa kijiji hicho wachangie matofali 100 kutoka kila
kaya ili yapatikane matofali 40,000 yatakayotumika kujenga zahanati ya
kijiji hicho.
Yeye aliahidi kuwachangia mabati
150 ambayo kati yake, mabati 100 yatatumika kuezekea zahanati ya kijiji
na mengine 50 yatatumika kukamilisha nyumba ya Mwalimu ambayo imekaa kwa
muda mrefu bila kumaliziwa.
Katika kuhakikisha ujenzi wa
zahanati hiyo unaanza mara moja, Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya
Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alichangia mifuko 100 ya
saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Mkutingome.
Nao Umoja wa Wachimbaji Wadogo katika mgodi wa Namungo ambao uko jirani
na kijiji hicho waliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, DESEMBA 31, 2016
No comments:
Post a Comment