Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar .
Mwenyekiti wa Taasisi ya
Mwanaharakati Bibi Siti bint Saad, Bi Nasra Moh’d Hilali amewataka
wanawake kushikamana kwa pamoja kupinga udhalilishaji wa kijinsia kwa
wanawake na watoto .
Kauli hiyo ameitoa alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake ndani ya Wizara ya
Habari Utalii Utamaduni na Michezo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema udhalilishaji wa kijinsia
umekithiri katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar jambo ambalo
linapelekea kudhoofisha maendeleo nchini hivyo amewashauri akinamama
kupiga vita vitendo hivyo .
Katika kupambana na vitendo hivyo
Bi Nasra ameitaka jamii kujenga mashirikiano ya pamoja katika mfumo
mzima wa malezi ya watoto na kuona watoto ni wa jamii na sio ya
wazazi wawili pekee.
“Tujiunge kwa pamoja tuseme
hatutaki udhalilishaji na tusiiachie Serikali pekee kwani suala hilo ni
kubwa na linaathiri watu wengi kisaikolojia,”alisema Bi. Nasra
Alieleza tukio la hivi karibuni
la mwanamke kuchomwa moto na mpenzi wake katika kijiji cha Paje
linaonyesha udhalilishaji uliokithiri katika jamii na kuchangia
kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Alifafanua kuwa kauli mbaya
wanazotoa wanaume kwa wake zao zinachangia udhalilishaji uliowazi na
amewataka akinababa kuwa na kauli nzuri kwa familia zao.
Aidha aliwataka akinamama kuwa
tayari kutoa taarifa wanapobaini dalili za mtoto wa jirani anataka
kudhalilishwa ili hatua za kuzuia vitendo hivyo ziweze kuchukuliwa kwa
haraka.
No comments:
Post a Comment