Pages

Saturday, December 3, 2016

BUZWAGI YAADHIMISHA SIKU YA UKIMWI DUNIANI KWA KUZINDUA MAHUSIANO CUP ILI KUHAMASISHA JAMII KUPIMA VVU

 Tarehe 1 Desemba kila mwaka ni siku ya maadhimisho ya Ukimwi Duniani,mwaka huu 2016 Kampuni ya Uchimbaji Madini ya dhahabu ya Acacia kupitia mgodi wa Buzwagi uliopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeadhimisha siku hiyo kwa kuzindua Mashindano ya mpira wa miguu na pete “Mahusiano Cup” ili kuhamasisha jamii inayozunguka mgodi huo kupima virusi vya Ukimwi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Mahusiano yaliyoenda sambamba na zoezi la upimaji wa VVU katika uwanja wa taifa mjini Kahama , Meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo alisema kampuni yao inazidi kufarijika kuona namna mahusiano baina ya mgodi na wananchi wanaozunguka mgodi huo.
“Mahusiano na jamii yamekuwa yakiimarika siku hadi siku,awali tulipoanza mashindano haya mwaka 2009 ni kata ya Mwendakulima pekee ndiyo ilikuwa ikinufaika kwa kuzikutanisha timu zinazounda mitaa yake ambayo ni Mwime,Chapulwa,Busalala na Mwendakulima”,alisema Mhandisi Mwaipopo.

Mhandisi Mwaipopo alisema mashindano hayo yataendelea hadi Desemba 8 mwaka huu yakikutanisha timu 14 za mpira wa miguu na timu 6 za mpira wa pete.
“Timu zote 20 zimekabidhiwa jezi na mipira vyote vikiwa na gharama ya shilingi 20,355,000/=,kwa timu ya mpira wa miguu na pete  mshindi wa kwanza atapewa zawadi ya shilingi 400,000/= na kombe,mshindi wa pili 300,000/= na mshindi na kwa upande wa kampeni ya utoaji elimu ya Ukimwi jumla ya shilingi 25,600,000/= zimetumika kununulia vifaa vya upimaji na uendeshaji wa zoezi lenyewe”,aliongeza Mhandisi Mwaipopo.

Alisema kwa kubadilisha mtazamo wa uendeshaji wa michezo ya mahusiano Cup awamu hii wamezihusisha kata nyingi zaidi za tarafa ya Kahama Mji na itakuwa fursa muhimu kwa wadau wa michezo kuweza kuona vipaji vya wanamichezo na kutafuta namna nzuri ya kuviendeleza.
Alizitaja timu za mpira wa miguu zitakazoshiriki kuwa ni Nyihogo,Nyahanga,Busoka,Kahama mjini,Zongomela,Malunga,Majengo,Mwendakulima,Ngogwa,Nyasubi,Mhongolo,Wendele na timu ya mgodi wa Buzwagi na timu za mpira wa pete kuwa ni Kahama mjini,Mhungula,Mwendakulima,Mhongolo,Ngogwa na Zongomela.
Katika hatua nyingine mhandisi Mwaipopo alisema kiwango cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi vimeshuka katika mgodi wa dhahabu wa Acacia Buzwagi wilayani Kahama mkoani Shinyanga kutoka asilimia 2.6 mwaka hadi kufikia asilimia 0.4 mwaka 2016 baada ya kuwahamasisha kupima afya zao.
Mwaipopo alisema pamoja na kiwango cha ndani ya mgodi kuridhisha maeneo yanayozunguka mgodi wa Buzwagi yana kiwango cha juu cha maambikizi ya VVU ambapo takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha maambukizi kwa wilaya ya Kahama kwa takwimu za kitaifa ni asilimia 9.6,mkoa wa Shinyanga asilimia 7.4.
Naye mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu aliupongeza mgodi huo kwa kuchukua hatua ya kuhamasisha jamii kupima VVU kupitia michezo kwani takwimu za maambukizi zinatisha wilayani humo ambapo asilimia 70 ya vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 49 wamepata maambukizi ya VVU,ambao ndiyo nguvu kazi ha taifa.
Nkurlu aliupongeza mgodi huo kwa kuwa mdau mkubwa wa michezo wilayani humo kwa kudhamini timu kadhaa na kuziwezesha kushiriki katika mashindano mbalimbali ndani nan je ya mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu (katikati) akisindikizwa na meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo kwenda kukagua  timu zinazoshiriki Mahusiano Cup mara baada ya kuwasili katika uwanja wa taifa wa Kahama.Kulia ni Meneja Uendelevu mgodi wa Buzwagi George Mkanza na wa kwanza kushoto ni mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Kahama Ibrahim Khan akifuatiwa na mkuu wa polisi wilaya ya Kahama 
Kulia ni afisa mawasiliano na habari wa mgodi wa Buzwagi bwana Magesa Magesa (mwenye shati la bluu) akiongozana na maafisa wa serikali walipowasili uwanjani. Kushoto kwake ni katibu tawala wilaya ya Kahama Timoth Ndanya ,Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama Anderson Msumba pamoja na maafisa wengine wa serikali
Washiriki wa Mahusiano Cup wakiwa uwanjani wakisubiri kukaguliwa na mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akisalimiana na wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Nyihogo

No comments:

Post a Comment