Na Lilian Lundo-MAELEZO,Dar es Salaam
KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa
nchini (TPBC) imemfungia Bondia Francis Cheka kushiriki katika mchezo wa
ngumi kwa kipindi cha miaka miwili na kulipa faini ya shilingi laki
tano kwa kitendo cha kukacha pambano baina yake na Bondia Abdallah Pazi
(Dulla Mbabe).
Akizungumza na waandishi wa habari
leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Msaidizi wa TPBC, Chatta Michael
alisema kamisheni hiyo ilitoa kibali cha pambano kati ya Cheka na
Abdallah Pazi lakini bondia huyo hakufika katika pambano hilo huku akiwa
ameshalipwa kiasi cha shilingi milioni tatu.
Chatta alisema kuwa Cheka
aliaharisha pambano hilo lililokuwa lifanyike katika ukumbi wa Sabasaba
tarehe 25 Desemba mwaka huu pasipo na kutoa taarifa, wakati Promota wa
pambano hilo alikwishaingia gharama mbalimbali za maandilizi ya pambano
hilo.
“Kamisheni imejiridhisha kuwa
kiasi cha shilingi milioni tatu kilitolewa kwa Francis Cheka kabla ya
pambano, hivyo alitakiwa apatiwe kiasi kilichobaki baada ya pambano kama
alivyokubali na kusaini mkataba wa pambano hilo,” alifafanua Chatta.
Aliongeza kuwa kitendo cha kutotii
makubaliano na kuchukua fedha bila kuifanyia kazi si jambo la kawaida
kwa kuwa lina madhara makubwa katika kuendeleza mchezo wa ngumi za
kulipwa nchini.
Kwa mujibu wa Chatta alisema TPBC
imetoa adhabu hiyo ili kuwa fundisho kwa mabondia wengine ambao wanaweza
kusababisha mchezo wa ngumi kupoteza uaminifu kwa wakuzaji na
kusababishha uvunjifu wa amani kwa watazamaji iwapo wataendelea
kudanganywa kuhusu uwepo wa mapambano hewa.
Kwa upande wake, Rais wa
TPBC,Chaurembo Palasa alisema adhabu hiyo ni mwanzo wa kuboresha mchezo
wa ngumi za kulipwa kwani mchezo huo umekuwa ukiendeshwa bila kufuata
sheria, kanuni na taratibu kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment