Mnamo Novemba Tano mwaka huu, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
atatimiza mwaka mmoja tangu alipoapishwa kuongoza Nchi hii katika
kipindi cha miaka mitano ijayo.
Katika uongozi wake wa mwaka
mmoja, Sekta ya Utalii nchini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika
kuongeza mapato ya serikali kupitia mikakati mbalimbali ambayo imeifanya
kuwa sekta kuwa yenye manufaa zaidi ya kiuchumi.
Hatua hii inatokana takwimu
zilizotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambazo zinaoonyesha kuwa
katika kipindi cha mwaka 2015 idadi ya watalii waliongia nchini ilikuwa
1,376,182 na kuingizia mapato kiasi cha Dola za Marekani 1.9 bilioni.
Aidha ,idadi ya watalii walioingia
nchini katika kipindi cha Julai mpaka Agosti imeongezeka asilimia 11,
na hivyo kuifanya ni eneo linaloiingizia Serikali takribani asilimia 25
ya fedha za kigeni.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili
na Utalii, Mhe.Profesa Jumanne Mghembe anasema kwa kuzingatia dhamira ya
Serikali ya kujitegemea kiuchumi Wizara yake imeanzisha kodi ya
ongezeko la thamani (VAT) katika sekta ya utalii, hatua iliyolenga
kuiongezea Serikali mapato yatakayoweza kuchangia katika kutoa huduma za
jamii.
“Uanzishaji wa kodi ya ongezeko la
thamani (VAT) katika sekta ya utalii, kumesaidia kuongeza watalii
nchini na mapato yamekuwa kwa asilimia 22 zaidi,” anasema Waziri
Maghembe.
Waziri Maghembe anasema uanzishaji
wa VAT haujaathiri ongezeko la idadi ya watalii nchini, na badala yake
Tanzania inaendelea kuwa kimbilio la watalii duniani
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na
Wizara ya Maliasili na Utalii, idadi ya watalii wanaoingia katika
Hifadhi za Taifa (TANAPA) katika kipindi cha Juni-Julai 2016 imeongezeka
kwa wastani wa asilimia 2.2 na mapato yatokananyo na viingilio
hifadhini yameongezeka kwa wastani wa asilimia 19.7
Huduma za malazi pia zimekuwa
zikitozwa kodi na Serikali hivyo kuondoa msamaha wa miaka 10 uliokuwepo
awali na sasa vinachangia zaidi katika mapato ya nchi moja kwa moja kwa
kuondoa msamaha huo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa pamoja
na huduma za utalii zimeanza kutozwa VAT kwa asilimia 18, lakini safari
kwa ujumla zimeongezeka kwa asilimia chini ya hiyo kwa sababu huduma za
malazi zimekuwa zikitozwa kodi hiyo tangu miaka ya nyuma.
Katika hatua hiyo Watalii
mbalimbali waliohojiwa nchini wameonyesha kuunga mkono hatua hiyo ya
Serikali za kuwatoza kodi kwani fedha zitakazokuwa zikilipwa na wataliii
zitasaidia katika shughuli nyingine za uchumi.
Pia katika kuendeleza kutangaza
Sekta ya Utalii nchini, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imetenga kiasi
cha Tsh Milioni 648 kwa ajili ya shughuli za utangazaji wa Utalii nje ya
nchi na Tsh.Milioni 300 kwa ajili ya utangazaji wa vivutio vya utalii
wa ndani ya nchi.
Wizara ya Maliasili na Utalii
inaendelea kutekeleza majukumu yake licha ya mabadiliko na changamoto
mbalimbali na inatarajiwa kuwa rasilimali za maliasili, malikale na
utalii zitaendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa juhudi za kukuza uchumi
wa Taifa.
Kwa upande wa Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB) katika kipindi cha mwaka mmoja imeimarisha utangazaji wa
vivutio vya utalii kupitia mtandao wa kompyuta yaani Tourism Destination Portal
pamoja na mitandao ya kijamii kwa kuweka taarifa zaidi za vivutio vya
utalii katika tovuti hiyo maalumu ya utalii zikiwemo ramani (digital
map), picha za video na picha za mgando kwa kila kivutio cha utalii
katika tovuti hiyo.
Aidha, TTB imeendelea kushirikiana
na watu maarufu katika kutangaza utalii wetu. Miongoni mwa watu hao ni
wasanii wa ndani wakiwemo mchezaji maarufu wa Tanzania anayecheza mpira
wa miguu nchini Ubelgiji Mbwana Samatta na mwanamuziki Vanessa Mdee.
Mpaka kufikia mwezi Juni 2016
idadi ya watalii wa Kimataifa waliongia nchini ilikuwa ni 519,582
ikilinganishwa na watalii 504,711 waliongia nchini mpaka kufikia
mwezi Juni 2015.
Idadi hii ni sawa na ongezeko la
asilimia 2.86. Kwa kipindi cha miezi ya Julai na Agosti 2016 inaonyesha
kuwa idadi ya watalii waliongia kwenye hifadhi za Taifa imeongezeka kwa
wastani wa asilimia 11.16.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa
Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Magufuli aliwataka
mabalozi wanaowakilisha Tanzania nchi za nje kutumia fursa zilizopo
katika kutangaza utalii wa nchi ili kuweza kuongeza pato la Taifa
No comments:
Post a Comment