Na Mwashungi Tahir -Maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na
kampuni ya 361 ya Dar es salaam inaandaa Kongamano la pili la biashara
baina ya Tanzania na Commoro.
Kongamano hilo ambalo
linaratibiwa na Wizara ya Biashara , viwanda na masoko Zanzibar
litafanyika Novemba 19,2016, katika hoteli ya Seacliff iliyopo Kama nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Biashara, viwanda na masoko Amina Salum Ali wakati akizungumza na
waandishi wa habari huko ofisini kwake Migombani.
Waziri Amina amesema Mgeni rasmi anaetarajiwa
kulifungua kongamano hilo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein.
Amesema katika ufunguzi wa
Kongamano hilo kutafanyika shughuli za uwasilishaji mada na majadiliano,
mikutano ya ana kwa ana (B2B) na maonyesho ya wajasiriamali.
Ameongeza kuwa kutakuwa na mada
zitazowakilishwa na kugusa maeneo ya uwekezaji,biashara na miundombinu
ya usafirishaji wa bidhaa baina ya Tanzania na Comoro na kuangalia fursa
na vikwazo katika biashara ili kurahisisha Sekta ya biashara.
Waziri Amina amesema kongamano
hilo la biashara baina ya Tanzania na Commoro ni la pili, ambapo tamasha
la kwanza kama hilo lilifanyika nchini Commoro April 23, mwaka jana.
Akielezea kuhusu kongamano la
kwanza, amesema washiriki zaidi ya hamsini kutoka Tanzania wakiongozwa
na aliekuwa Waziri wa Mambo ya nchi za nje Benerd Membe walishiriki
Kongamano hilo.
“Kongamano la pili la biashara
baina ya Tanzania na Commoro linatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya
mia moja wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji , wajasiriamali na wadau
kutoka taasisi za umma” alisema waziri Amina.
Balozi Amina ameongeza kuwa
katika kongamano hilo atashauri kuangaliwa upya suala la kodi kwani
wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilalamikia kodi iliyopo kati ya
Tanzania na Comoro kuwa ni kubwa.
Naye Balozi wa Commoro Elbadaoui
Fakih amesema Tanzania imekuwa msaada mkubwa kwa nchi yake hasa kwa
kusaidia mambo mengi ikiwemo biashara na masuala ya kiuchumi
No comments:
Post a Comment