Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,
Ajira na Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati), akipata maelezo
kutoka kwa Meneja Kiongozi Masoko na Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume (kulia), wakati alipotembelea banda la NSSF
kwenye maonyesho ya Biashara ya 40 ya Kimataifa katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa
la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara.
Christian
Gaya, Majira Jumanne
Julai 26, 2016
Mikakati inayofanywa na serikali
pamoja mifuko ya hifadhi ya jamii, ili kuhakikisha ya kuwa mwananchi anapata
nyumba ya gharama nafuu kwa ajili ya makazi, lakini lengo hilo halijafanikiwa
kwa wananchi wengi wenye kipato cha chini kununua nyumba hizo.
Hii ni kutokana na ughali wa nyumba
hizo na kipato kidogo ambacho hakimwezeshi mwananchi kumudu manunuzi ya nyumba
ambazo zimejengwa ili kumuupa unafuu wa maisha mwananchi huyo wa hali ya chini.
Uwekezaji katika ujenzi wa nyumba na
makazi bora kwa wananchi wenye vipato vya chini ni muhimu kama mifuko ya
hifadhi ya jamii ina malengo ya kujenga uchumi endelevu kwa watu wote na kuhakikisha ya kuwa kila mwanachama anamiliki nyumba na
kuboresha maisha na familia yake .
Pamoja na mikakati inayofanywa na
mifuko hii ya hifadhi ya jamii, mara nyingi wanachama na wadau wa hifadhi ya
jamii na hata kwa kupitia vya yombo habari mbalimbali wamekuwa wakijiuliza maswali mbalimbali juu ya nyumba
za gharama nafuu zinazojengwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kwa ajili ya
kuwakopesha wanachama na wadau wengine wa hifadhi ya jamii.
Kulingana na utafiti uliofanywa hivi
karibuni baadhi ya maswali ya msingi yanayoulizwa juu ya ujenzi huu wa nyumba
za gharama nafuu ni kama vile kwa nini nyumba nyingi zinauzwa kwa gharama ya
juu wakati zinaitwa na kutangazwa kuwa ni nyumba za gharama nafuu?
Kufuatana na mahojiano kati ya Kituo
cha HakiPensheni na meneja mkuu wa uhusiano na huduma kwa wateja Bi Eunice
Chiume wakati kiipotembelea
banda la NSSF kwenye maonyesho ya Biashara ya 40 ya Kimataifa katika viwanja
vya
Sabasaba jijini Dar es Salaam anasema kabla ya kuanza kujenga nyumba hizi za gharama nafuu NSSF lilianza kufanya utafiti juu ya mapato ya uwezo wa walengwa wa wateja wake kimapato na kugundua ya kuwa wanachama na wadau wamegawanyika katika makundi makuu matatu kiuwezo wa kimapato.
Kundi la kwanza lilionekana kuwa ni lile
la kipato cha juu, kundi la pili ni lile la kipato cha kati na kundi la mwisho
ni lile la kipato cha chini. Baada ya kupata mwongozo huu wa utafiti ndipo
walipoanza kujenga nyumba hizi za gharama nafuu kwa kufuata uwezo wa makundi ya
wateja wao.
Kwa kutambua ya kuwa idadi kubwa ya
wananchi wa Tanzania wenye uhaba na wanaohitaji nyumba za makazi wamo katika
kundi la kipato cha chini, mfuko ulianza kujenga nyumba za gharama nafuu
kulingana na kundi la watu wa kipato cha chini.
“Mfano mzuri ni nyumba za gharama
nafuu zilizojengwa mwaka 2005 Tabata eneo la Kinyerezi wilaya ya Ilala ambazo
ziliuzwa kuanzia shilingi za kitanzania milioni 9 mpaka mpaka milioni 29
ikijumuisha pamoja na kodi ya 18% kwa kila nyumba” Eunice anasema.
Anasema hii ina maana ya kuwa kama
serikali wangeweza kuondoa kodi hiyo ya 18% ili kuwawezesha wananchi kujikwamua
na tatizo la uhaba wa makazi ya nyumba kama mojawapo la mahitaji ya lazima kwa
binadamu, mwanachama au mwananchi yeyote angeweza kupunguziwa makali ya kununua
nyumba ya shilingi milioni 9 kwa shilingi milioni 7.4 tu, na za shilingi
milioni 29 zingewezekana kuuzwa kwa shilingi milioni 23.8 bila kodi.
Na jambo lingine ambalo mlaji huyu
wa mwisho anakumbana nalo ni kwamba gharama zote za ujenzi zinawekwa ndani ya
bei ya mnunuzi huyu wa nyumba. Na kama pia mifuko hii ya hifadhi ya jamii
ingeweza kupunguziwa kodi hii ya thamani wakati inaponunua vifaa vya ujenzi pia
ingeweza kupunguza gharama hizi za ujenzi wa makazi ya nyumba, na hivyo kuweza
kufanya bei ya nyumba hizi kuwa rahisi kununuliwa na idadi kubwa ya wananchi.
“Lakini kwa kawaida mahali popote
duniani huduma muhimu kama maji, barabara na umeme ni wajibu wa serikali
kuwapatia wananchi wake. Pia kama serikali ingeweza kugharamia miundo mbinu hii
basi pia gharama ya bei ya kununulia nyumba hizi ingeweza kushuka chini zaidi
na zaidi kwa mwananchi wa kipato cha chini na ndiyo maana tunaita nyumba za
gharama nafuu” Eunice anafafanua.
Ambapo kiwango cha chini kabisa
kinachotakiwa kulipa kwa kila mwezi mpaka kumaliza na nyumba kuwa yako ni
shilingi laki moja (100,000/=) tu. Na nyumba zote zina huduma zote za muhimu
kwa mahitaji ya binadamu kama vile maji, umeme, na barabara.
Abbas
Abbas ambaye ni afisa mauzo wa NSSF anasema pamoja na hayo Mfuko umeweza pia
kujenga nyumba zipatazo 300 kwa ajili ya watu wa kipato cha kati zilizoko Mtoni
Kijichi Kibada awamu ya I na II ambazo ni za kisasa zaidi ukilinganisha za zile
za kipato cha chini, ambazo zinauzwa papo kwa papo au kwa mkopo kuanzia
shilingi milioni 75 mpaka milioni 133 pamoja na kodi na kati ya shilingi
milioni 65 mpaka shilingi milioni 113 bila kodi kila nyumba.
Kufuatana na Abass ni kwamba hapo
hapo Mtoni Kijichi Kibada kwa awamu ya III tena kuna nyumba ambazo zimejengwa
aina ya Maisonatte kwa ajili ya watu wa kipato cha juu zaidi zenye vyumba vinne
vyote ambavyo kila kimoja kinajitegemea yaani self contain.
Kila Nyumba ya aina hii ina baadhi ya vifaa
au nyenzo za ziada ambazo vimewekwa kwa kila nyumba, kwa mfano, stoo, jiko,
jiko la kuchemshia maji la umeme wa jua na maegesho ya magari mpaka magari 3 na
eneo la ziada ambalo unaweza kupanua ukubwa nyumba yako au kufanya bustani.
Nyumba hizi zinauzwa papo kwa papo
au kwa mkopo kuanzia shilingi milioni 290 mpaka milioni 330 pamoja na kodi na
kati ya shilingi milioni 237.8 mpaka shilingi milioni 270.6 bila kodi kwa kila
nyumba.
Vile
vile ndani ya awamu ya III hapo Mtoni Kijichi Kibada kuna nyumba aina ya Block
Flats zilijengwa ambazo zina vyumba vitatu vitatu kila flat, yaani vyumba 2 vya
kawaida vya kulala na kimoja kinachojitegemea “self contain”.
Ndani
ya flat moja vikiwemo pamoja na stoo, jiko, jiko la
kuchemshia maji la umeme wa jua na maegesho ya magari mpaka magari 3 na eneo la
ziada ambalo unaweza kupanua ukubwa nyumba yako au kufanya bustani. Pia flats hizo zinauzwa papo kwa
papo au kwa mkopo kwa kulipa kila mwezi kwa muda wa miaka 15
Kwa upande wa utaratibu wa ulipwaji
ni kwamba mfuko umeweka utaratibu wa kipekee kwa ulipaji wa mkopo wa nyumba kwa
wateja wake ni kwamba kama mteja anataka kununua kwa mkopo anatakiwa
kutanguliza malipo ya mkupuo wa miezi 3 kwanza na ndipo anapokabidhiwa ufunguo
wa nyumba yake, baada ya hapo ataendelea kulipa kila mwezi.
“Ambapo kwa mjasiriamali anaweza
kupangisha kwa watu wengine kwa kodi ya juu zaidi na hivyo kutengeneza faida
zaidi wakati huo huo akiendelea kulipa deni la mkopo wa nyumba hiyo kila mwezi
mpaka miaka 15 atakapomaliza deni” Eunice anawakumbusha wateja kutumia fursa
kama hii ya kipekee.
Christian Gaya ni
mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala
ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com
Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz
au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13
13 41
No comments:
Post a Comment