Pages

Thursday, July 28, 2016

CCM YAIJIBU CHADEMA

1 
Msemaji wa Chama cha Mapinduzi CCM Christopher Ole Sendeka akizungumza na waandishi wa habari leo katika Makao Makuu Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba  kushoto ni Mkuu wa Utawala Makao Makuu Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba  Bakari Hamis.
……………………………………………………………………………………………………..
Jana tarehe 27/7/2016 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walitoa kauli kwa Waandishi wa Habari kupitia Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Ndugu Freeman Mbowe (Mb). Tamko hilo kama ilivyo kawaida ya CHADEMA lilijaa uongo mwingi na ghiliba nyingi za kibabaishaji na kuthibitisha ukweli kuwa kwa hakika kutokana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dr. John Pombe Magufuli wapinzani nchi hii wamekosa ajenda na hivyo njia peke yake wanayoona inafaa ili waendelee kufanya utapeli ni kutunga uongo, kujiaminisha katika uongo huo na kuusambaza uongo huo ili kujaribu kupata wafuasi.
Katika uongo na uzushi huo walioutangaza jana, CHADEMA wanasema wameamua kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa tarehe waliyoitaja na maandamano hayo yatafanyika chini ya operesheni waliyoiita UKUTA. Kimsingi hoja walizozitumia kufikia uamuzi wao bila kuzirudia zimejaa upotoshaji na uongo uliokithiri. Kwa mfano wanadai Serikali imezuia mikutano yote ya vyama vya siasa, huku wakijua kuwa ni uongo kwani Serikali haijazuia mikutano kwenye majimbo yao, Wabunge wako huru kufanya shughuli zao kwenye majimbo yao, na tumeona Wabunge wakifanya shughuli zao majimboni bila shida wakiwemo hao wa vyama vya upinzani. 
Lakini vyama vya siasa kufanya shughuli kwa mujibu wa katiba ya vyama vyao sio jambo lililozuiliwa pia, ndiyo maana tumeshuhudia vyama vikifanya mikutano yao ya kikatiba bila tabu.
Lakini mfano mwingine wa hoja za uongo na uzushi, ni hoja eti ya Serikali hii ya Awamu ya Tano kuwa ya kidikteta. Udikteta hasa unaosemwa na Chadema ni upi? Ni huu wa kushughulikia watumishi hewa? Ni huu wa kuwabana wakwepa kodi? Ni huu wa kupunguza na kudhibiti safari za nje? Ni huu wa kubana matumizi ya Serikali? Ni huu wa kufukuza wabadhirifu na wazembe kazini? Hivi udikteta huo ni huu wa kushughulikia mafisadi mpaka kuanzisha mahakama yao? CCM inaamini Watanzania walio wengi wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli na Serikali yake, sasa kama kwa Chadema hatua hizi ndiyo tafsiri yake ni udikteta basi bila shaka wao ni sehemu ya mfumo mbovu ndiyo maana wako tayari kuleta vurugu ili wautetee.
Kwa kuwa CHADEMA wamezoea kujenga Chama chao kwa harakati zinazohusisha kumwaga damu za Watanzania wasiokuwa na hatia, ukweli huu wa maelekezo ya Serikali hawausemi, isipokuwa wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha wanafanya mambo ambayo mwisho wa siku yatasababisha vurugu, uvunjifu wa amani na umwagaji damu.
Lakini pengine ni muhimu Watanzania na wapenda amani nchini na duniani wakajiuliza ni kweli kuwa lengo la hizi vurugu na maandamano haya ni la kujenga na si kubomoa? Kwa nini kila operesheni ikifanywa na CHADEMA huwa inaambatana na umwagikaji wa damu za Watanzania wasiokuwa na hatia? Wakati wa Maandamano hayo inapotokea madhara ni kwa nini waathirika huwa sio viongozi waanzilishi wa maandamano hayo wala wake au waume zao au watoto wao au hata ndugu zao wa karibu bali huwa ni watu wengine nje ya hao ndugu zao wa karibu? Mpaka lini damu za Watanzania wasio na hatia zitaendelea kutumika kutafuta umaarufu wa CHADEMA na viongozi wake?
Hii ni kwa faida ya nani hasa? Kwa nini pamoja na kuelekezwa namna bora ya kufanya siasa wao huwa hawataki kufuata utaratibu? Hivi ni kweli kuwa hawajui bila kufuata utaratibu jambo lolote huwa ni vurugu?
Chama Cha Mapinduzi kinapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa ni vizuri kutafakari na kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kuamua kushiriki au kuruhusu watoto wetu kwenda kuwa kafara ya walafi wachache wa madaraka. Ni vizuri tukayakumbuka matukio kwenye operesheni kama hizi yaliyopoteza maisha ya vijana wetu na matokeo ya kila operesheni.  
Pamoja na ukweli kuwa hakuna operesheni yeyote kati ya zote zilizowahi kufanywa na Chadema ambayo imewahi kuwasaidia Watanzania wa kawaida zaidi ya kujenga umaarufu wa viongozi wachache wa Chadema na kuneemesha matumbo yao na ya familia zao, operesheni zote zimepoteza maisha ya Watanzania kadhaa wasiokuwa na hatia wala wasiofaidika kwa lolote na operesheni hizo.
Kama nia ni njema kwa nini hawataki kufuata Sheria na taratibu tulizojiwekea? Demokrasia gani isiyokuwa na mipaka? Demokrasia bila mipaka ni fujo. Tunaomba vyombo vinavyohusika visisite kuchukua hatua zinazostahili bila kumuonea mtu lakini bila kufumbia macho vitendo vyenye lengo la kuwahujumu Watanzania waliowengi walioamua kuchapa kazi kuitikia wito wa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya kazi.
Lakini pia tunawashauri Watanzania, wapenda amani, utulivu na maendeleo kupuuza wito wa vurugu na uvunjifu wa amani badala yake wajikite kwenye kuchapa kazi na kujitafutia maendeleo yao kwa kufanya kazi kwa bidii.
Maendeleo hayaji kwa maandamano, maendeleo huja kwa kuchapa kazi kwa bidii. Maendeleo hayaji kwa vurugu na fujo nchini, bali amani na utulivu ni vichocheo muhimu vya maendeleo ya kweli.
Imetolewa na:-
Christopher Ole Sendeka (MNEC),
MSEMAJI WA CHAMA
28/07/2016

WAZIRI MKUU ATOA SIKU MOJA KWA HALMASHAURI YA WILAYA TEMEKE KUMALIZA TATIZO LA AJIRA ZA MIKATABA

NDI1 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya  Chamazi jijini Dar es salaam baada ya kuwasili shuleni hapo kukbidhiwa madawati na fedha shilingi milioni 100 kwa ajili ya Shule za Dar es salaam  Julai 28, 2016.Wengine pichani kutoka kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, Theresia Mmbando, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda na Mkuu wa wilaya ya Temeke  Felix Lyaviva. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NDI2 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na wananchi wa Temeke baada ya kuwasili kwenye Shule ya Msingi ya Chamazi kukabidhiwa madawati na fedha shilingi milioni 100  kwa ajili ya Shule za Dar es salam  Julai 28, 2016. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda. (Picha na Oisi ya Waziri Mkuu)
ndi4 
Baadhi ya wanafunzi na mmoja wa wananchi waliohudhuria hafla ya kukabidhi madawati na fedha shilingi milioni 100 kwa Waziri Mkuu kwenye shule ya Msingi yaChamazi jijini Dar es salaam Julai 28, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
ndi5 
Waziri Mlkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi, Augustine Mahiga (katikati) na Murtaza Adamjee wa Jumuiya ya Mabohora Nchini katika hafla ya kakabidhi madawati na fedha  shilingi milioni 100 kwa shule za Dar es salaam  iliyofanyika kwenye Shule ya Msingi ya Chamazi jijini Dar es salam Julai 28, 2016.(Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
ndi6 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Chamazi  jijini Dar es salaam baada ya kupokea madawati na fedha shilingi milioni 100 kwa ajili ya mkoa wa Dar es salaam Julai 28, 2016.Madawati ayo yalitolewa na Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki ikishirikiana na Ubalozi wa Kuwait nchini pamoja na Jumuiya ya Mabohora nchini. (Picha na Ofisi  ya Waziri Mkuu)​
ndi7 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimshukuru , Murtaza Adamjee wa Jumuiya ya Mabohora nchini baada ya kukabidhiwa madawati 105 kwenye Shule ya Msingi ya Chamazi jijini Dar es salam Julai 28, 2016. Kushoto ni Balozi wa Kuwait nchini, Jaseem Al Najem na Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Susan Kolimba. (Picha na Ofisi ya Waziri  Mkuu)
……………………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Temeke kuondoa wafanyakazi wa mkataba kwa anjia ya kuwapa ajira ya kudumu kwa wenye sifa na kuwaondoa wasiokuwa na sifa ifikapo  Julai 30 mwaka huu.
Amesema kitendo cha kutowaajiri na kuwatumikisha kwa mikataba kwa muda mrefu kinasababisha wakose stahiki zao jambo ambalo si halikubaliki.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Julai 28, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo na kusisitiza kwamba ni lazima sula hilo lishughulikiwe haraka kwa sababu hayo ndio matundu watumishi hewa.
“Mnawatumikisha watu kama vibarua kwa muda mrefu, hapa kuna wengine wanafanya kazi kwa mikataba kwa miaka mitano hadi sita hii haikubaliki kwani mnawakosesha stahili zao pale mnapowaachisha kazi,” amesema.
Awali Kaimu Ofisa Utumishi wa Manispaa hiyo Zaitun Hassan alisema wamekuwa wakitoa ajira za mikataba kwa sababu wamekosa watu wenye sifa za kuweza kuajiriwa husan madereva.
“Kwa mara ya mwisho umetangaza lini nafasi za ajira? Katika mkoa wa Dar es Salaam kweli wanaweza kukosekana madereva wenye sifa za kuajiriwa? Alihoji Waziri Mkuu.
Zaitun alisema kuwa madereva wengi wanaojitokeza pindi wanapotangaza ajira wanashindwa kufikia vigezo ikiwemo kuwa na cheti cha VETA na badala yake wanakuwa na cheti cha kidato cha nne tu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kuwa kuna wafanyakazi wengine katika Idara ya Uhasibu na Ujenzi ambao nao wameajiriwa kwa mkataba hivyo amemtaka Ofisa Utumishi kuomba kibali cha kuajiri kwa Katibu Mkuu Utumishi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufanya tathmini ya maeneo yote ya shule kwenye mkoa wake na watakaobainika kuingia katika maeneo hayo waondolewe haraka.
Amesema baada ya kukamilisha utengenezaji wa madawati kinachofuatia sasa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambapo amezitaka halmashauri kuweka mipango  ya kujenga majengo ya madarasa ya ghorofa ili waweze kuwa na madarasa mengi katika eneo dogo.
Awali Waziri Mkuu alipokea msaada wa madawati 705 katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Chamazi wilayani Temeke ambapo kati yake Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania umetoa madawati 600 na Jumuia ya Mabohora imetoa madawati 105.
Pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Agustino Mahiga alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 85 fedha zilizochangwa na watumishi wa wizara hiyo kwa ajili ya kuchangia utengenezaji wa madawati.
Dk. Mahija alisema watumishi hao walichanga sh. milioni 100 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati ambapo sh. milioni 15 wamekabidhi kwa mkuu wa wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe ambaye alikuwa mtumishi wa wizara hiyo ili naye akatengeneze madawati kwa shule za wilayani kwake.
Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini Jaseem Al Najem amesema Serikali ya Kuwait itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika shughuli zote za maendeleo hususan katika sekta za elimu na afya.

WAREMBO WANAOWANIA SHINDANO YA MISS TANGA 2016 USIPIME SASA KUFANYIKA IJUMAA MJINI TANGA

 
 Warembo wanaowania Taji la Mrembo wa Mkoa wa Tanga (Miss Tanga 2016) wakiwa kwenye pozi katika hotel ya Tanga
Beach Resort kutakapofanyika shindano hilo Ijumaa Kesho.
 
Warembo hao wakiwa kwenye picha ya pozi
Warembo wanaowania Taji la Urembo Mkoa wa Tanga(Miss Tanga 2016) ambalo linaandaliwa na Kituo cha Radio cha TK FM cha Mjini Tanga kwa
kushirikiana na Hotel ya Tanga Beach Resort wakiwa kwenye picha ya
mapozi
Mratibu
wa Shindano ya Miss Tanga 2016,Mboni Muya akizungumza na waandishi wa
Habari leo kuhusiana na maandalizi ya kuelekea shindano hilo

Baadhi ya Warembo wakimsikiliza Mdau wa Tasnia ya Urembo hapa nchini
Sinza,Beny Kisaka alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kuitembelea
kambi ya warembo hao wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Five
Brothers Nassoro Makau
Warembo hao wakimsikiliza Mratibu waShindano ya Miss Sinza 2016 ambaye aliitembelea kambi hiyo
leo
 Mdau wa Tasnia ya Urembo hapa
nchini,Benny Kisaka akitoa nasaha kwa warembo wanaotarajiwa kushiriki
kinyang’anyiro cha kumtafuta Mlimbwende wa Mkoa wa Tanga (Miss Tanga
2016 )itakayofanyika Ijumaa kesho  kwenye Ukumbi wa Hotel ya Tanga Beach
Resort.
 Mdau wa Tasnia ya Urembo hapa
nchini,Benny Kisaka akisisitiza jambo wakati akizungumza na warembo
wanaotarajiwa kushiriki shindano la kumtafuta Mlimbwende wa Mkoa wa
Tanga Ijumaa
 
Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha

Manispaa ya Dodoma yakusanya asilimia 80.28 ya mapato katika vyanzo vyake

index 
NA RAMADHANI JUMA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imefanikiwa kukusanya asilimia 80.28 ya mapato kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya ndani katika mwaka wa fedha 2015/2016 uliomalizika Juni 30 mwaka huu.
 Katika mwaka huo wa fedha Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ilipanga kukusanya shilingi 4,566,075,181 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani (own sources) ambapo mpaka mwisho wa mwaka huo makusanyo halisi ni 3,665,699,279 sawa na asilimia 80.28 ya makisio.
Akizungumza katika kikao cha mwaka cha Baraza la Halmashauri ya Manispaa hiyo, Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa, mafanikio hayo yametokana na uchapaji kazi wa watendaji na madiwani wa Manispaa hiyo.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa, Mstahiki Mwanyemba aliwapongeza wote waliohusika kwa namna yeyote katika kufikia hatua hiyo huku akitoa wito kwa Ofisi ya Mkurugenzi na Madiwani wa kuimarishwa kwa juhudi zaidi katika ukusanyaji katika mwaka wa fedha 2016/2017.
“Mwaka mpya wa fedha umeshaanza hivyo Mkurugenzi na watendaji wako anzeni kukusanya kodi mapema…na waheshimiwa madiwani tuongeze nguvu katika kusimamia vyanzo vya mapato katika maeneo yetu” alisema.
Aidha, katika mkutano huo ambao kwa mujibu wa kanuni unakuwa na ajenda mbili tu ambazo ni kujadili taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri kwa mwaka uliopita na kupitia na kupitisha ratiba ya vikao vya Halamshauri kwa mwaka unaofuata, wajumbe walipitisha ratiba ya vikao vya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 .   

HOMA YA INI B NA C KUTOKOMEZWA IFIKAPO MWAKA 2030

 Baadhi ya vijana waliokuwa wakitumia dawa za kulevya wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kutokomeza homa ya ini wakielekea kwenye  maadhimisho ya siku ya homa ya ini yaliyofanyika viwanja vya Mwembe Yanga Dar es Salaam leo mchana.
 Bango likihimiza kuungana kutokomeza homa ya ini.
 Maandamano yakiendelea kuelekea viwanja vya Mwembe Yanga. Katikati ni Mratibu wa Mtandao wa Watu Wanaotumia Dawa za Kulevya (TANPUD), Happy Assan.
 Vijana waliopo kwenye mtandao wa kupinga matumizi ya dawa za kulevya wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Mratibu wa Mtandao wa Watu Wanaotumia Dawa za Kulevya (TANPUD), Happy Assan, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
 Mwenyekiti wa TanPud Tanzania, Godfrey Ten, akizungumza katika maadhimisho hayo.
 
 Ofisa Maendeleo ya Jamii, Mratibu wa Asasi za Kiraia kutoka Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya Tanzania, Salome Mbonile, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
 Mwakilishi wa Taasisi ya Pasada, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
 Mratibu wa Afya- Dawa za kulevya wa Manispaa ya Temeke, Mwajuma Mwihumbo akizungumza kwenye maadhimisho hayo kwa niaba ya Meya wa Manispaa hiyo.
 Maadhimisho yakiendelea.
 Vijana waathirika na dawa za kulevya wakicheza kwenye maadhimisho hayo.
 Meneja wa Afya  Madaktari wa Dunia Dk. Faith Aikaeli kutoka Taasisi ya Medicins Du Monde akizungumza kuhusu ugonjwa huo.
Wageni waalikwa katika picha ya pamoja.
 
Dotto Mwaibale
 
UGONJWA wa homa ini umepangwa kutokomezwa ifika mwaka 2030 imefahamika ambapo watu wapatao  milioni 1.4 upoteza maisha ulimwenguni kutokana na maambuki ya ugonjwa huo ulimwenguni hasa kwa wale wanaotumia mihadarati kwa njia ya kujidunga.
 
Hayo yalibainishwa na Mratibu wa Afya- Dawa za kulevya wa Manispaa ya Temeke, Mwajuma Mwihumbo kwa niaba ya Meya wa Manispaa hiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya homa ya ini yaliyofanyika viwanja vya Mwembe Yanga Dar es Salaam jana.
 
Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza ufahamu kuhusu na kuungana na juhudi za ulimwengu za kutokomeza homa ya ini.
 
Alisema mada ya kampeni ya kimataifa ya homa ya ini ya mwaka huu ni utokomezaji ambao ni mwaka muhimu kwa homa ya ini.
 
Alisema lengo la maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na asasi za kiraia, wafanyakazi wa huduma za afya, taasisi na vikundi vya utetezi na ushawishi ni kuongeza ufahamu wa homa ya ini B na C hasa kwa makundi hatarishi kama watumiaji wa mihadarati wanaojidunga.
 
Meneja wa Afya  Madaktari wa Dunia Dk. Faith Aikaeli kutoka Taasisi ya Medicins Du Monde alisema katika mkutano mkuu wa 69 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ni serikali zote ziliazimia kwa pamoja kuidhinisha mkakati wa ulimwengu wa utokomezaji wa homa ya ini.
 
Alisema hadi Februari 2016 nchi 36 zilikuwa zina mipango ya kitaifa ya utokomezaji wa homa ya ini na nchi 33 zipo katika mikakati ya kuandaa mipango hiyo.
 
“Mkakati unalenga kutokomeza homa ya ini B na C ifikapo mwaka 2030 ambapo unahusisha malengo ya tiba ambayo iwapo yatafikiwa yatapunguza vifo vinavyosababishwa na homa ya ini kwa asilimia 65 na kuongeza huduma ya tiba kwa asilimia 80 hivyo kuokoa maisha ya watu milioni 7.1 ifikapo mwaka 2030”  alisema Dk.  Aikaeli


(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
 
 
 
 
 
 

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA MAJALIWA ATAKA MABARAZA YA MADIWANI KUFANYA MAPITIO YA UPUNGUFU VYA VYUMBA VYA MADARASA KATIKA HALMASHAURI NCHINI

LIA1 
Na Beatrice Lyimo
MAELEZO- Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa maagizo kwa  Mabaraza ya Madiwani nchini kufanya mapitio katika shule zote za Halmashauri ili kujua upungufu wa madarasa na kuanza mkakati wa utekelezaji wa  ujenzi wake.
Aliyasema hayo leo  wakati akipokea mchango wa madawati kwa shule ya msingi Chamazi kutoka Wizara Ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais la upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari nchini.
Mhe. Majaliwa alisema  suala la upatikanaji wa madawati linakwenda sambamba na ujenzi wa madarasa hivyo ni wajibu wa kila halmashauri kuweka mkakati wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwani elimu bora ni pamoja na kuwa na mazingira rafiki ya kusomea.
‘Mbali na utekelezaji wa agizo la Rais juu ya mkakati wa upatikanaji wa madawati, suala hili linakwenda sambamba na ujenzi wa madarasa hivyo Serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi huo  kwa maeneo machache hivyo ni jukumu la halmashauri kuhakikisha mnaandaa mikakati ya kuongeza vyumba vya madarasa’ alisema Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa Serikali imeanza mkakati wa utekelezaji wa mpango wa  kutumia mfumo mpya wa upandishaji  madaraja walimu kwa kuwa  mfumo wa uliuotumika awali haukuwa na tija kwa maslahi ya walimu nchini.
Akipokea madawati hayo Waziri mkuu alisema kuwa anajua shida iliyopo ya upungufu wa madawati katika wilaya ya Temeke hivyo na kugawa madawati hayo katika shule tatu zilizopo katika Wilaya hiyo ikiwemo shule ya msingi Chamazi, shule ya msingi Mbande pamoja na shule ya msingi Majimatitu .
Kwa upande wake Waziri wa Wizara Ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi  Augustine Mahiga alisema  wizara yake ina jukumu la kuhakikisha inaitangaza nchi ili kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi wa nchi, na kuongeza kuwa elimu bora ni msingi imara katika kufanikisha hilo.
Waziri Mahiga alisema Ubalozi wa Kuwait nchini pamoja na Jumuiya ya Mabohora wameikabidhi Serikali jumla 405 ili kuunga mkono jitihada za Rais ikiwemo
“Serikali ya Kuwait kupitia Ubalozi wake hapa nchini wametoa madawati  300 na kuahidi kutoa mengine 300 na Jumuiya ya Mabohora nao wamechangia madawati 105” alisema Balozi Mahiga.
Kwa mujibu wa Waziri Mahiga alisema watumishi wa Wizara yake walichanga kiasi cha Tsh. Milioni 100 ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha umma ili kuhamasisha umma kuhusu zoezi la upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na Sekondari nchini.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKABIDHI HUNDI YA TSH. 85 MILIONI KWA JESHI LA MAGEREZA ZITAKAZOTUMIKA KUTENGENEZEA MADAWATI, JIJINI DAR

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi mfano wa hundi Afisa Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, SACP. John Masunga(kushoto) leo Julai 28, 2016 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chamazi. Waziri Mkuu amelekeza Fedha hizo zitumike kutengeneza madawati ya shule za msingi Majimatitu na Mbande zilizopo Wilayani Temeke.
MBO2 
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa ameketi kwenye madawati yaliyotolewa kwa Msaada wa Ubalozi wa Kuwait Nchini Tanzania kama inavyoonekana katika picha(Picha na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).
…………………………………………………………………………………………………………………………………
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) amekabidhi hundi ya Tsh. 85 Milioni kwa Uongozi wa Jeshi la Magereza  ili litengeneze jumla ya madawati  1,703 yatakayotumika katika Shule za Msingi za Majimatitu na Mbande zilizopo Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.
Hafla ya makabidhiano hayo  yamefanyika  leo tarehe 28 Julai, 2016 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chamazi iliyopo Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es salaam ambapo Waziri Mkuu Majaliwa  amekabidhi madawati katika Shule ya Msingi Chamazi yaliyotolewa na Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania na Jumuiya ya Mabohora Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa  amewashukuru na kuwapongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kutoa mchango huo na pia amewapongeza wadau wengine ambao wameitikia wito wa Rais Magufuli wa kuchangia madawati kwa lengo la kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.
Waziri Mkuu Majaliwa  amesema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza katika shule mbali mbali imeongezeka hali iliyosababisha upungufu wa madawati lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.
Aidha,  amelitaka na Jeshi la Magereza kutengeneza madawati hayo mapema iwezekanavyo ili yakamilike haraka na kuanza kutumika katika Shule za Msingi Majimatitu na Mbande kwani shule hizo zinakabiliwa na idadi kubwa ya Wanafunzi hapa Jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Ramadhani Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam, Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, Wananchi pamoja na wanafunzi wa Shule ya msingi Chamazi.
Lucas Mboje, Mrakibu Msaidizi wa Magereza,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
28 Julai, 2016.

TUNAZISUBIRI NEC NA ZEC KUIPIGIA KURA YA MAONI KATIBA INAYOPENDEKEZWA

MWAB1Mwenyekiti wa  Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi  (KIKUHAMI ) chini ya WiLDAF  Bibi Thabita Siwale akizungumza kumshukuru Waziri wa Mambo ya Katiba na sheria Dkt Harrison Mwakyembe walipokutana nae Ofisini kwake jijini Dar es salaam
MWAB2 
Uongozi  wa Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi  (KIKUHAMI ) chini ya WiLDAF  katika picha ya pamoja na  Waziri wa Mambo ya Katiba na sheria Dkt Harrison Mwakyembe  na katibi Mkuu Prof Sifuni Mchome walipokutana nao Wizarani jijini Dar es salam
MWAB3 
waziri wa Mambo ya Katiba na sheria Dkt Harrison Mwakyembe akizungumza na Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi  (KIKUHAMI ) chini ya WiLDAF uliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam
……………………………………………………………………………………………………………
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Harrison Mwakyembe amesema Serikali inazisubiri Tume ya Uchaguzi nchini (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanziba (ZEC) zimalize majadiliano yao ili mchakato wa kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa ufanyike.
Mhe. Mwakyembe ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokutana na uongozi wa Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi  (KIKUHAMI ) kilichoko chini ya Chama cha Wanawake katika Sheria na Maendeleo  Afrika – WiLDAF.
Amesema zoezi hilo lingekuwa limeshakamilika ila Tume za Uchaguzi ziliona ni bora liahirishwe kwanza ili kupisha zoezi la Kikatiba lililokuwa likiikabili nchi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana likamilike na kwamba kukamilika kwa zoezi hilo kunatoa fursa kwa Serikali kuendelea na mpango wake wa kuendesha kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa ili kupata Katiba Mpya ya Tanzania.
Aliongeza kuwa Katiba Inayopendekezwa ina vitu vingi sana ambavyo vitasaidia upatikanaji wa haki za wanawake na kuondoa uonevu dhidi yao na hivyo kufanikisha harakati ambazo wadau mbalimbali wa wanawake nchini wamekuwa wakizipigania na hivyo kukamilika wakati Katiba mpya itakapokuwa imepatikana.
Aidha Mhe. Waziri ameutaka uongozi huo wa KIKUHAMI kupitia WiLDAF kuwasilisha Wizarani mapendekezo yao juu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za Mirathi nchini wanazoziona zinawakandamiza wanawake ili ziweze kufanyiwa marekebisho na ziendane na wakati uliopo.
“si mnataka sheria mbalimbali za mirathi zibadilishwe?, leteni mapendekezo yenu , hili ni jukumu letu sote, sisi tupo na hapa wizarani tunao wataalamu watazipitia na kuona namna ya kuzifanyia kazi, ili ziendane na wakati uliopo sasa, alisema na kuongeza kuwa ndio maana amesema Katiba Inayopendekezwa ina vipengele vingi ambavyo vitasaidia kuondoa uonevu kwa wanawake nchini  itakapopitishwa na wananchi kupitia kura ya maoni.”
KIKUHAMI chini ya Uongozi wa Bibi Thabita Siwale ulimuomba Waziiri wa Katiba na Sheria Dkt Mwakyembe kuangalia uwezekano wa kuondoa sheria zinazowakandamiza wanawake hasa zile za mirathi kwani zinawafanya wanawake hasa wajane kunyanyasika katika nchi yao

RAIS WA SIMBA SPORTS CLUB EVANS AVEVA AZINDUA WIKI YA SIMBA NA SIMBA DAY 2016.

Rais wa Simba Sport Club  Evans Aveva akizungumza na Vyombo vya Habari leo wakati wa Uzinduzi wa Simba Week Akiwa Sambamba Katibu Mkuu wa Simba Patrik Kahemela (Kulia) na Afisa Masoko na Mawasiliano Kutoka Eaggroup Richard Ryaganda( kushoto) .
Simba inasherehekea wiki maalum iliyo Batizwa Jina la Simba Week ambayoImezinduliwa Leo na Rais wa Simba Sport Club Ndugu Evans Aveva na  hufikia kilele chake Tarehe 8 Mwezi Agosti. Mwaka huu siku hii ya Simba week itakuwa na uzito wa kipekee kwani Klabu ya Simba itakuwa inaanza Sherehe za kuadhimisha Miaka 80 ya klabu Hiyo. Sherehe za Wiki ya Simba zinaenda sambamba na dhima yetu ya kuendeleza Mabadiliko chanya ndani ya Simba bado inaendelea kushika kasi, Katika kipindi cha mwaka mzima.  
Katika Kipindi Hiki Simba  Sport Club imekuwa na utaratibu wa kuwa na siku maalum kwaajili ya kufurahi, kuwatambulisha Rasmi wachezaji,Jezi za timu na kujiandaa kwa Msimu Mpya, siku hii imekuwa Maarufu kama Simba Day. Tangu  Ianzishwe imekua ikiboreka Siku hadi siku, mwaka huu Imeona ni Muhimu kuiboresha zaidi na hususani kuangalia Mchango wa timu Hiyo kwa Jamii inayoizunguka. 
 Simba iliamua kuanzisha Simba Week ambayo lengo lake kuu ni kuwa wiki ya Simba Sports Club kufanya kazi za Jamii, kukuza vipaji vya soka vya vijana, kutembelea  Wadau wa Maendeleo na pia Shughuli Nyingine Zenye Tija kwa Timu..Siku ya Simba Day, Simba Sports Club itacheza Mechi naInter Clube ya Angola kwenye Mechi hii Wachezaji Wapya wataonekana Rasmi baada ya Maandalizi. 

Nyauhenga ateuliwa kuwa Kaimu Meneja

index 
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amemteua Bw. Eliud Nyauhenga kuwa Kaimu Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB).
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri huyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jijini Dar es Salaam inaeleza kuwa, uteuzi huo umefanyika baada ya Meneja wa Bodi hiyo Bw. Joseph Haule kumaliza mkataba wake.
“Kwa mamlaka niliyonayo chini ya Sheria ya Bodi ya Mfuko wa Barabara Sura 220 ya mwaka 2006, nimemteua Bw. Eliud Nyauhenga kuwa Kaimu Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara tangu Julai 27 mwaka huu”, alisema Mbarawa.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, kabla ya uteuzi huo  Bw. Eliud Nyauhenga alikuwa Meneja Msaidizi wa Bodi hiyo.
Aidha, katika taarifa hiyo, Waziri huyo amempongeza Bw. Joseph Haule kwa kuuongoza Mfuko huo kwa weledi, uadilifu na mafanikio makubwa tangu ulivyoanzishwa mwaka 2000.
Bodi ya Mfuko wa Barabara ilianzishwa kwa Sheria Na. 11 ya mwaka 1998 chini ya Sheria ya Ushuru wa Barabara Na.2 ikiwa na jukumu la kusimamia makusanyo, matumizi na ufuatiliaji wa Bodi hiyo,

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA AKEMEA TAMKO LA CHADEMA

index 
Nimepokea kwa masikitiko tamko la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lililotolewa jana tarehe 27 Julai, 2016 kupitia vyombo vya habari, kuhusu hali ya demokrasia ya vyama vingi hapa nchini. Tamko hilo limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, kuudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani. Ili kuepuka kurejea tamko lote, nimeona ni vyema nitoe mfano wa maneno yafuatayo yaliyosemwa, ambayo yanakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa:-
“CHADEMA tunasema tunaitangaza siku ya tarehe 1 Septemba, 2016 kama siku ambayo itakuwa ni siku ya mikutano nchi nzima ikiwamo maandamano ambapo ngazi zetu mbalimbali za chama kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa tutafanya mikutano in defiance ya order ya Rais, ya Jeshi la Polisi kwamba haturuhusiwi kufanya mikutano ya kisheria”
Kimsingi, Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 kifungu 9 (2)(c) inakataza chama cha siasa kutumia au kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu kama njia ya kufikia malengo yake ya kisiasa.
Aidha, kifungu cha 9(2)(f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu viongozi au wanachama wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha au ikapelekea kutokea uvunjifu wa amani. Vile vile kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, Tangazo la Serikali namba 215 la mwaka 2017, zinakataza chama cha siasa kutumia lugha za matusi, kashfa, uongo na uchochezi.
Kanuni ya 5(1)(d) inakitaka kila chama cha siasa kutotoa maneno yoyote au maandishi ambayo ni uongo. Kuhusu mtu yoyote au chama cha siasa chochote.
Kanuni ya 5(1)(f) inasema kuwa, kila chama cha siasa kina wajibu wa kulaani na kupinga yafuatayo:-
(i)                  Matumizi ya lugha ya matusi;
(ii)                 Vitendo vya kibabe na vurugu; na
(iii)   Matumizi ya nguvu ili kujipatia umaarufu wa chama au sababu yoyote ile.
Hivyo, tamko la CHADEMA ni ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Aidha, hii siyo mara ya kwanza kwa CHADEMA kutumia lugha za namna hii za kuhamasisha uvunjifu wa amani (civil disorder).
Natumia fursa hii kukemea tamko hilo hadharani, kwa mujibu wa kanuni ya 6(2) ya Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa. Pia nawaasa CHADEMA wasiendeleze tabia hii.
Mwisho, napenda kusisitiza kuwa, kwa dhamana niliyopewa kama Msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa, napenda kutumia fursa hii kuviasa vyama vyote vya siasa vitimize wajibu wao kwa weledi kama taasisi za kisiasa.
Ni vema Viongozi wa Vyama vya Siasa  wakaonyesha taswira stahiki ya wanasiasa wakomavu, au Vyama vya Siasa vya kutolea mfano ndani na nje ya mipaka yetu, kwa kuzingatia Sheria za Nchi katika kuendesha shughuli za kisiasa.
Vyama vya Siasa viepuke vitendo, kauli au matamshi yenye mlengo wa kusababisha uchochezi au kufarakanisha Umma na Serikali yao.
Madhali zipo Sheria na njia stahiki za kidemokrasia za mawasiliano na Taasisi za Umma, basi navisihi Vyama vyote vya Siasa kuzingatia utaratibu huo wa mawasiliano kwa mujibu wa Sheria zilizopo. Aidha, uvumilivu wa kisiasa katika azma za kudumisha ukuaji wa kidemokrasia nchini haukwepeki.
Tudumishe amani ya nchi yetu.
“MUNGU IBARIKI TANZANIA”
Jaji Francis S.K. Mutungi
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
 
28 Julai, 2016

MPANGO WA OFISI YA WAZIRI MKUU KUHAMIA DODOMA WIKI IJAYO WAKAMILIKA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Uratibu, na Watu Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama (Mb)amepokea  Mpango Mkakati  wa Kuhamia Dodoma  wiki ijayo wa Ofisi ya Waziri Mkuu leo Jijini Dar es Salaam tarehe 28 Julai,2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo.
Mhagama amekutana na wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi katika kukamilisha Mpango Mkakati huo ili kukamilisha utekelezaji huo.
pos2Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali akiwasilisha Issa Nchasi akiwaitisha wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Mpango wa Ofisi hiyo kuhamia Dodoma wiki ijayo.
pos1 
Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa Mpango Mkakati wa Kuhamia Dodoma leo Jijini Dar es  Salaam tarehe 28 Julai, 2016.
pos3 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama na Naibu Waziri anayeshughulikia ( Watu Wenye Ulemavu )Abdallah Possi  pamoja na wakuu wa Idara wakifuatilia uwasilishwaji wa Mpango Mkakati wa Kuhamia Dodoma wa Ofisi hiyo, leo  Jijini Dar es Salaam tarehe 28 Julai, 2016.
pos4 
Maafisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa Mpango Mkakati wa kuhamia Dodoma katika  JIjini Dar es Salaam tarehe 28 Julai,2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo.

NAIBU WAZIRI HAMAD MASAUNI AONGOZA KIKAO CHA KUJADILI MKAKATI WA KUPUNGUZA AJALI NCHINI

suf1 
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza katika kikao cha Baraza hilo cha kujadili Mkakati wa Kupunguza Ajali nchini. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni Katibu wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna, Mohamed Mpinga. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
suf2 
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto meza kuu) akimsikiliza Mjumbe wa Kikao hicho, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dk. Zakaria Mganilwa (kulia) alipokuwa anachangia mawazo katika Kikao cha kujadili Mkakati wa Kupunguza Ajali nchini. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni Katibu wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna, Mohamed Mpinga. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
suf3 
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza katika kikao cha Baraza hilo cha kujadili Mkakati wa Kupunguza Ajali nchini. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa Baraza hilo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
suf4 
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto meza kuu) akimsikiliza Katibu wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna, Mohamed Mpinga (kulia meza kuu) alipokuwa akizungumza katika Kikao cha kujadili Mkakati wa Kupunguza Ajali nchini. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

No comments:

Post a Comment