Madaktari
wa Tanzania katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete, wakishirikiana na wenzao wa India walifanikiwa kufanya upasuaji wa
moyo wa aina yake Tanzania.Upasuaji huo ujulikanao kama ‘bypass surgery’
ulishirikisha kupandikizwa kwa mishipa ya damu kutoka sehemu nyingine ya mwili
moyoni bila kutumia mashine ya kusimamisha moyo na mapafu.Kwa kawaida madaktari
wanasema upasuaji wa moyo hufanyika baada ya moyo na mapafu kusimama.
Christian Gaya, Majira Ijumaa Juni, 24, 2016
Utafiti kutoka nchi kumi na
tano za Kiafrika ikiwemo Tanzania unaonesha idadi kubwa ya watu wa kipato cha
chini wanakimbilia kukopa na kuuza rasilimali zao ili kuweza kwenda pamoja na
gharama za matibabu. Hali hii imepelekea familia nyingi kuingia kwenye janga la
umasikini zaidi na afya zao kuwa mbaya zaidi huko vijijini.
Pia utafiti uliofanywa
kutoka katika nchi sita za Kiafrika unaonesha kuwa idadi ya asilimia zaidi ya
nne (4%) ya wazee wanasumbuliwa na magonjwa sugu ya moyo na kisukari hasa pale
wanapofikisha umri wa miaka zaidi ya sitini ukilinganisha na wale ambao wako
chini ya umri wa miaka sitini.
Pamoja na hayo bado serikali
kama ya Tanzania, inatumia kiwango kidogo sana cha kipato kwa kichwa cha mtu
kwa matumizi ya afya ukiachilia mbali hifadhi ya jamii ukilinganisha na nchi
zilizoendelea.
Gharama hasa ya matibabu
mara nyingi anaachiwa mwananchi ambaye hana uwezo wa kubeba mzigo bila msaada
wowote kutoka serikalini au jumuia yeyote.
Afya
maana yake ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwepo kwa
maradhi. Wote tunajua ya kuwa afya bora ni nguzo na raslimali muhimu katika
kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta
maisha bora na kupunguza
umaskini.
Kwa
mantiki hii afya inalenga kuwa na ustawi endelevu kwa jamii kwa kuzingatia
mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa zilizopo katika
kuleta maisha bora.
Mwaka 2014 jopo la Madaktari bingwa wa
magonjwa ya macho, kisukari na shinikizo la damu, lililokuwa linazunguka nchi
nzima lilibaini kuwa asilimia 79 kubwa ya watanzania waliopimwa magonjwa hayo
ni wazee kati ya mamilioni ya watanzania waliofikiwa na huduma hizo, ambao
wamepata matibabu pamoja na kupewa elimu ya kukabiliana na magonjwa hayo.
Magonjwa ya mara kwa mara na ya muda
mrefu, ni hali ya kawaida kwa wazee walio wengi wakiwemo akina mama na watoto.
Hali hii inahitaji uangalizi na matunzo maalum ya kitaalam. Pamoja na ukweli
huo, huduma za afya hazipatikani kwa urahisi kwa wazee na watoto walio wengi na
mara nyingi ni ghali.
Utaratibu wa kutoa huduma bure kwa
wazee bado una mapungufu. Wazee walio wengi hasa wa vijijini wanaachwa nje ya
utaratibu wa kupata huduma kutokana na kushindwa kuthibitisha kwamba wana umri
wa miaka 60 na hawana uwezo wa kuchangia gharama hizo.
Mfuko wa bima ya afya umeanzisha
mradi wa kuwasogezea huduma mbalimbali wateja wake zikiwemo huduma za madaktari
bingwa katika maeneo ya pembezoni.
Uchache wa madaktari bingwa hapa
nchini umekuwa ni changamoto kubwa sana umekuwa ukisababisha matatizo makubwa
kwa wazee, vijana na watoto kwa kupoteza maisha kwa kukosa matibabu sahihi au
kushindwa kuzifikia huduma ziliko kutokana na umbali wa kijiografia
Na ndiyo maana mfuko wa bima ya afya
mwaka 2013 walianzisha mpango wa huduma za madaktari bingwa maalumu wa
kuwapeleka wataalamu katika mikoa ambayo miundo mbinu yake ni mibovu ili wazee,
vijana na watoto wa maeneo hayo nao waweze kunufaika na huduma za NHIF zikiwemo
za upasuaji na aina za magonjwa makubwa.
Taarifa zinaonesha ya kuwa kwa
kipindi kuanzia Januari mpaka Machi 2015 mfuko ulifanikiwa kupeleka madaktari
bingwa katika mkoa wa Tabora ambapo jumla ya wagonjwa 634 wakiwemo wazee,
vijana na watoto walionwa na wataalamu hao ambapo kati ya hao wagonjwa 27
walifanyiwa upasuaji, huduma ambazo zisingeweza kufanyika mkoani hapo bila
huduma hii ya madaktari bingwa wa vijijini.
Pia utafiti unaonesha ya kuwa tangu
mpango huu uanze wagonjwa 6,535 wamenufaika na huduma za wataalamu hao huku
wagojwa 238 wakifanyiwa upasuaji, huduma ambazo wangetakiwa kuzifuata Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, Bugando Mwanza, KCMC Moshi, Mbeya au maeneo mengine
ambapo wangetumia muda mwingi na gharama kubwa katika kuzipata huduma kama
hizi.
Mpaka
sasa kuna uhaba mkubwa wa madaktari bingwa hasa wa wanawake na watoto katika
maeneo ya nje ya mijini, hali inayowafanya wanaoishi kwenye vijiji mbalimbali
nchini kuikosa huduma ambayo kimsingi ni haki yao.
Madaktari bingwa wasio na
vituo maalumu, inatakiwa wapelekwe kila mkoa nchini ikiwa kama utekelezaji wa
moja ya mikakati ya Mfuko huu ya kuboresha huduma za afya kwa wanachama wake,
ili kusaidia wanachama kupata huduma za madaktari bingwa kutoka maeneo yao,
hasa wa vijijini, ili kupunguza gharama na muda wa kusafirisha wagonjwa nje ya
mkoa au nchi.
Kuimarishwa kwa utoaji huduma za madaktari bingwa kutachangia kuhamasisha wanachama wenye sifa za kujiunga na Mfuko kuongezeka, na kufanya Watanzania wengi kunufaika na huduma za Mfuko huo.
Jambo la muhimu ni kuhakikisha ya kuwa mfuko unawahamasisha wananchi wa vijijini ili wajiunge na mifuko ya afya ya jamii, kwani kwa sababu kwa kufanya hivyo utakuwa na mchango mkubwa katika kusaidia huduma za matibabu vijijini kwa njia ya huduma za madaktari bingwa na huduma nyinginezo.
Watanzania wanategemea mpango kuwa
endelevu zaidi kwa sababu umeonesha huduma kama hizi kusaidia kuokoa maisha ya
watanzania wengi ambao hawana uwezo wa kifedha na gharama za kuzifuata
zinakopatikana. Hivyo ni juu ya wananchi kuhakikisha ya kuwa fursa kama hii
inatumiwa vizuri na siyo vinginevyo.
No comments:
Post a Comment