Pages

Thursday, December 3, 2015

Ufahamu uhusiano wa hifadhi ya jamii na soko la ajira


Afisa wa Mfuko wa PSPF akiwaelemisha wafanyakazi jinsi ya kujiandikisha, kupeleka michango ya hifadhi ya jamii na kufungua madai ya mafao 
 
Christian Gaya, Mwananchi Alhamisi, Disemba3, 2015

Hifadhi ya jamii imeundwa kwa ajili ya kuwapatia mfanyakazi ulinzi dhidi ya majanga ya kiuchumi na ya kijamii yanayosababishwa na kukoma au kupungua kipato kutokana na maradhi, uzazi, kuumia kazini, ukosefu wa ajira, ulemavu, uzee, kifo na kuongezeka kwa gharama za matibabu.

Hifadhi ya jamii ni kwa ajili ya manufaa ya kumkinga mfanyakazi dhidi ya majanga. Na ili kuwepo na hifadhi ya jamii ambayo ni kinga lazima ichangiwe fedha. Kwa ukweli ni kwamba hifadhi ya jamii inachangiwa na michango kutoka kwa mwajiri na mfanyakazi pamoja.
Kwa kawaida mfanyakazi ambaye ni mwanachama wa mfuko wa pensheni hukatwa asilimia 10 ya jumla ya mapato yake yote kwa mwezi na mwajiri analazimika huchangia asilimia 10 ya mapato yote ya mshahara wa mfanyakazi hivyo na kufanya kuwa jumla ya asilimia 20 na yote hupelekwa kwenye akaunti ya mwanachama wa mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii. 

Au mwajiri huweza kuchangia asilimia 15 na mwajiriwa asilimia 5 au asilimia yote 20 inaweza kutolewa na mwajiri kwa mfanyakazi wake kulingana na makubaliano kama sehemu ya motisha kwa mfanyakazi.

Michango anayochangia mwajiri ni wazi ya kuwa ni gharama kwa mwajiri, ambapo matokeo yake inaweza kusababisha kupunguza faida kwa mwajiri.  Kadri faida inavyopungua kwa mwajiri, hii inaweza kusababisha ukuaji wa kuajiri kwa wafanyakazi kuteremka chini zaidi na hatimaye kusababisha wafanyakazi kupunguzwa au kuachishwa kazi. 

Waajiri pia wanaweza kuwa na njia mbili zingine za kuchagua kutawanya gharama. Wanaweza kutawanya gharama zinazoongezeka kama hizi za michango ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya wafanyakazi wao kwa kuwaongezea ndani ya bei ya huduma au bidhaa za walaji wao.
Hivyo basi, kuongezeka bei ya bidhaa kwenye masoko ya kimataifa mara nyingi inapunguza ushindani wa bidhaa za nchi husika,na hata kupunguza ukuaji wa ajira wakati mwingine. Kwa upande mwingine mwajiri anaweza kuwa na uwezo wa kupunguza mshahara wa mfanyakazi wake.  

Hii itategemea na mpangilio wa soko la ajira lilipo nchini au kwa wafanyakazi kulipizwa makato ya michango kwa mwajiri wao moja kwa moja kwa kupewa mshahara uliopunguzwa tayari na mwajiri au kwa njia ya kuwa na ukuaji mdogo wa ajira, au kuwa na nguvukazi kubwa ambayo haina ajira. 

Kwa kawaida wafanyakazi hupokea mafao wakati wa kustaafu unapowadia, ingawa wao wafanyakazi hulipa kwa ajili ya haya mafao wakati wanapofanya kazi kwa njia ya kuchangia michango yao kila mwezi.

Kuongezeka kwa mafao ya hifadhi ya jamii kwa upande mwingine kunasababisha kuongezeka kwa gharama za kuendesha mfumo wa hifadhi ya jamii. Kwa hiyo hapa kuna mabadilishano kwa wafanyakazi kati ya mfumo wa hifadhi ya jamii wenye mafao makubwa yanayovutia na wenye gharama kubwa na mfumo wa hifadhi ya jamii wenye mafao madogo yasiyovutia na wenye gharama ndogo. 

Mchaguzi na mapangaji wa mfumo huu mara nyingi hufanywa na serikali kwa kufuata matakwa ya wadau wa sekta ya hiafadhi ya jamii au wananchi, kwa kupitia mdhibiti na msimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii mfano kwa hapa Tanzania ni SSRA.

Wafanyakazi wakati mwingine wanaweza kujisikia ya kuwa wangependelea kutumia fedha zao zaidi wakati wa miaka ya kufanya au wangali bado wana nguvu za kufanya kazi na waje watumie kidogo baada ya kustaafu kinyume na utaratibu wa sheria ya sekta ya hifadhi ya jamii.
Wafanyakazi wa aina hiyo unakuta wana ari ndogo sana ya kuendelea kufanya kazi kwa miaka yote ya kufanyia kazi kwenye sekta rasmi.
Wao wangependa kufanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi sehemu ambayo ingewawezesha kupata nafasi nzuri zaidi kuweza kutumia sehemu kubwa ya mapato yao leo badala ya kuwekeza au kuchangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kupata pensheni watakapokuwa hawana nguvukazi kwenye soko la ajira kwa siku sijazo.

Muundo wa gharama na mapato yalichaguliwa na  serikali yanapokuwa ya juu sana, yanaweza kufanya idadi kubwa ya wafanyakazi kuangukia katika kundi hili na kufanya kuongezeka kwa kukua kwa sekta isiyo rasmi na ukwepaji wa kutolipa mchango ya pensheni ya hifadhi ya jamii pia kuongezeka 

Jambo la pili ni kwamba muundo wa mapato na gharama wa sekta ya hifadhi ya jamii kwa hapa Tanzania unaosimamiwa na SSRA unaweza ukawa hautoi thamani nzuri za mafao kwa mfanyakazi. 

Kwa mfano, kama wafanyakazi mara kwa mara wanapokea pensheni ndogo zaidi kuliko thamani ya michango waliyochangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, ni dhahiri ya kwamba wafanyakazi hao hawawezi kuendelea kuchangia tena.
Ni kweli ya kwamba kila mfanyakazi hawezi kupata thamani ya michango ile ile kamili aliyochangia. kwa wale wastaafu waliobahatika kuishi kwa  miaka mingi zaidi  ni wazi ya kuwa watapokea pensheni kubwa zaidi kuliko wale watakao kufa mapema baada ya kustaafu, hii ni kawaida ya utaratibu wa bima ya pensheni ya hifadhi ya jamii inavyofanya kazi.

No comments:

Post a Comment