Pages

Sunday, November 22, 2015

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 20 NOVEMBA 2015

images 
Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi huu.
Pia natoa pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge letu limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.
Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika kata mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa sababu kuu mbili:
• Kwanza, ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
• Pili, nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki. Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote niliyoahidi katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka Wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani pia watafanya hivyo hivyo kama tutakavyofanya sisi.
Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Watanzania wote. Tulijiandikisha kwa wingi sana kwa ajili ya kupiga kura, tulishiriki na kufuatilia kwa karibu sana kampeni za uchaguzi, na tukajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. Kinyume na ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema hakuna siku iliyokuwa na utulivu mkubwa na amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba tulivyokwenda kupiga kura. Hata baada ya matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha utulivu mkubwa, na hata pale ambapo matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo baadhi yetu walivyoyatarajia bado tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana mkubwa.
Wale waliotarajia kuwa tutafarakana wameondoka wakiwa wamefadhaika sana huku wakijiuliza hivi hawa Watanzania ni Waafrika wa namna gani. Ndugu zangu Watanzania, kwa mara nyingine tena tumedhihirisha, kwetu sisi wenyewe, kwa Afrika na dunia, kwamba sisi ni kisiwa cha Amani katika bahari iliyochafuka. Tunayo haja ya kujipongeza na kujiwekea nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali hii na kuilinda amani ya nchi yetu. Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa wa vyama vyote na viongozi wa dini ni kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya nchi yetu.
Aidha, napenda niungane na ninyi pamoja na Watanzania wote kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama (Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na Usalama wa Taifa pamoja na mgambo) kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama katika kipindi chote cha uchaguzi.
Nawapongeza pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa namna walivyosimamia zoezi zima la uchaguzi toka hatua za awali za kujiandikisha hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo. Mmetimiza wajibu wenu kwa weledi na umahiri mkubwa katika mazingira magumu na yenye changamoto nyingi. Hongereni, hongereni sana!
Mheshimiwa Spika;
Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru viongozi wakuu wa nchi yetu walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri walioifanyia nchi yetu. Natambua mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kujenga misingi imara wa umoja, mshikamano na amani ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa na kuijenga misingi yake. Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) kwa kupanua na kuimarisha misingi ya uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee Kikwete (Mzee wa Maisha Bora) kwa kuendeleza misingi hiyo na kupanua fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo yao. Wamefanya kazi kubwa. Nawashukuru sana na ninawatakia uzee mwema na maisha marefu ili tuzidi kuchuma busara zao.

No comments:

Post a Comment