Kwa ufupi
Inadaiwa kuwa Lusinde alikutana na Makamu Mwenyekiti katika Hoteli ya New Mwanza ambako wabunge hao walikuwa wamefikia na kubahatika kuzungumza naye ambapo
SAKATA la Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutapeli
Sh1.6 bilioni za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeingia
sura mpya baada ya Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde
kulifikisha kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula, akidai
hiki ni chanzo cha chama chake kupoteza ushindi katika uchaguzi mkuu.
Habari ambazo zilipatikana kutoka ndani ya CCM na kuthibitishwa na mbunge huyo wa CCM, Livingstone Lusinde zimeeleza kuwa uamuzi huo wa kumshtaki Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Willson Kabwe umekuja kutokana na kubainika kwamba tendo la kupata wakati mgumu kwa CCM katika medani za kisiasa kumechangiwa na makosa ya mkurugenzi huyo.
Inadaiwa kuwa Lusinde alikutana na Makamu Mwenyekiti katika Hoteli ya New Mwanza ambako wabunge hao walikuwa wamefikia na kubahatika kuzungumza naye ambapo walimweleza, kwamba iwapo wanataka CCM kubadilisha hali ya hewa Mwanza na kushinda uchaguzi, ni lazima ihakikishe inamwajibisha Mkurugenzi wa Jiji, Willson Kabwe.
Akithibitisha taarifa hizo, Mbunge huyo wa Mtera Livingstone Lusinde alisema hayo yalikuwa mazungumzo ya kawaida kabisa kwa kiongozi wake wa chama na kwamba hayakuwa mashtaka bali alikuwa akitoa picha ya baadhi ya mambo ambayo ameyaona katika ziara yao kama wabunge wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii. “Jamani haya yalikuwa mazungumzo binafsi, nilikutana naye kwa vile sote tulikuwa hoteli moja, nikamweleza mambo haya kwa vile yalinikera sana mimi binafsi.
Mkurugenzi wa Jiji, Kabwe alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusuan na madai hayo alisema hawezi kujadili masuala ya mitaani na kwamba iwapo ataombwa kufanya hivyo na mwajiri wake atakuwa tayari, lakini siyo mazungumzo tu ya watu wawili na kubainisha huo siyo utaratibu wa kazi.
Hivi karibuni,NSSF ikiwakilishwa na Kaimu Mkurungenzi wake Ludovick Mroso, alieleza kuingia mkataba na halmashauri hiyo chini ya Mkurugenzi Kabwe mwaka 2008 kwa ajili ya kununua viwanja 692 ili kujenga nyumba.za kuuza, lakini licha ya kuwalipa, halmashauri hiyo bado haikuweza kuwapatia viwanja NSSF.
Walieleza katika mkataba wao wa Agosti 18, 2008, NSSF iliingia mkataba wa Sh1.8 bilioni kwa ajili ya kupewa viwanja ambapo katika awamu ya kwanza ilihusisha Sh943 milioni sawa na asilimia 50 baada ya mkataba kusainiwa zikiwa ni kwa ajili ya kulipa fidia.
Awamu ya pili ya malipo ilikuwa ni Sh755 milioni sawa na asilimia 30 zikiwa ni fedha zilizopaswa kulipwa baada ya ujenzi wa barabara katika viwanja na malipo ya awamu ya tatu na ya mwisho ilikuwa ni asilimia 20.
Kwa upande wa NSSF waliweza kukamilisha asilimia 80 ya malipo kwa awamu ya kwanza na ya pili kwa kulipia jumla ya Sh1.6 bilioni hadi kufikia Juni 2011, lakini Halmashauri ya Jiji hakuweza kuwakabidhi viwanja hadi jana.
Katika utetezi wa jiji hilo ambao ulitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Tito Mahinya alidai kuwa mpango huo wa viwanja 300 vya NSSF huko Bugarika ulikwama kutokana na eneo hilo kuibuka vurugu baada ya wananchi wamiliki wa mashamba kuhamasishwa na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema) kuanza vurugu.
No comments:
Post a Comment