Pages

Tuesday, May 29, 2012

NSSF yakwama Machinga Complex

7th May 2012
Chapa
Maoni
Jengo la Machinga Complex lililoko Ilala
Sakata la jengo la Machinga Complex lililoko Ilala, Dar es Salaam limebainika kuendesha biashara ambayo hailipi na imeshindikana kulipa deni la mkopo wa ujenzi wake.

Jengo hilo linalomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lilijengwa kwa mkopo kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sh. bilioni 12.9.

Kutokana na kufanya biashara isiyolipa na kushindwa kulipa deni la mkopo huo, NSSF imesema kuwa jengo la Machinga Complex limeshindwa kurudisha fedha hizo ambazo lilizitoa kwa Jiji la Dar es Salaam kama mkopo.

Jengo hilo la ghorofa lilijengwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapatia wamachinga waliozagaa jijini sehemu ya kufanyia biashara zao.

Hadi sasa Jiji limeshindwa kulipa mkopo huo wa NSSF, ambalo kwa sasa deni linakadiriwa kufikia Sh. bilioni 30 kutokana na ongezeko la riba.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya NSSF, Manispaa ya Ilala na Jiji la Dar es Salaam, fedha za kulipia deni hilo zilitarajiwa zitokane na kodi ya jengo hilo ambalo kwa sasa lina idadi ya wamachinga 5,000 waliopanga kwenye vizimba vya kufanyia biashara.

Ofisa Uhusiano Mkuu wa NSSF, Eunice Chiume, amethibitisha kwamba shirika lake mpaka sasa halijalipwa fedha zozote kama sehemu ya kulipia mkopo walioutoa kwa Jiji la Dar es Salaam.

Chiume alilihakikishia NIPASHE kwamba Jiji halijaanza kulipa fedha hizo, huku akikataa kuingia kiundani katika suala hilo ambalo hivi karibuni limekuwa likizua maswali mengi.

Awali wakati wa ujenzi huo unaanza, serikali ilijigamba kwamba ungekuwa na tija ikiwemo kujiendesha kwa faida na kuwahudumia wamachinga wanaozagaa hovyo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, mradi huo hivi sasa umeshindwa kutekeleza malengo hayo sambamba na kushindwa kulipa deni la NSSF.

KAULI YA ZUNGU
Mbunge wa Ilala, Musa Azzan Zungu, ambaye alikuwa katika bodi ya ujenzi wa jengo hilo, aliliambia NIPASHE kuwa kazi aliyokuwa amepewa ni kuwakusanya wamachinga na kuwaingiza katika jengo hilo ili wafanye biashara.

Zungu alisema kazi hiyo aliifanya kwa ufanisi na kufanikiwa kupata wamachinga 5,000 ambapo kila mmoja alitakiwa kulipia kizimba chake Sh. 60,000 kwa mwezi kama kodi.

“Mimi kazi yangu ilimalizika baada ya kuingiza wamachinga 5,000 ili wafanye biashara katika jengo hilo, lakini kazi ya kuhakikisha wanadumu hapo bila kuhama pamoja na kulipa kodi hilo siyo suala langu tena,” alisema Zungu.

Hata hivyo, taarifa kutoka vyanzo vyetu vya habari, zinasema kuwa baadhi ya watalaamu wamekuwa wakishauri yawekwe mabango ya matangazo  juu ya jengo hilo ili kusaidia kulipa deni hilo, lakini suala hilo linakwamishwa kutokana na vitendo vya ufisadi.

Taarifa hizo zinasema kuwa kama ushauri huo ungekubalika na kutekelezwa, jiji lingeweza kupata zaidi ya Sh. milioni 30 kwa mwezi kutokana na mabango ya matangazo ambazo zingesaidia kulipia mkopo wa NSSF.

MEYA MASABURI
Meya wa jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, alipotafutwa hivi karibuni kuzungumzia sakata hilo, aliitupia lawama Manispaa ya Ilala kwa maelezo kuwa ndiyo ilikuwa inashughulika na utaratibu wa kuwaingiza wamachinga katika jengo hilo.

MKURUGENZI ILALA AKOSOA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime, alipotafutwa na NIPASHE ili kutoa ufafanuzi wa sakata hilo, alithibitisha kuwa mradi huo haulipi kama ilivyotarajiwa na waliotoa wazo la kuuanzisha.

Aidha, Fuime alithibitisha kwamba mabilioni ya fedha yalitumika katika kujenga jengo hilo, lakini akaweka bayana kwamba ni mradi ambao hauna faida.

Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Ilala aliongeza kwamba mapato kutoka kwa wamachinga hayatoshi kulipia deni la NSSF ambalo kwa sasa linazidi kuongezeka kutokana na riba.

Fuime alithibitisha kuwa Manispaa ya Ilala ilishirikishwa katika kuanzisha mradi huo, lakini alisema walioingia  katika mkataba ni Ofisi ya jiji la Dar es Salaam pamoja na NSSF.

“NSSF walitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo huku jiji likitoa ardhi kama dhamana yake katika kukamilisha mradi huu,” alisema Fuime.

Alisema mradi wa jengo hilo haulipi kwa kuwa wafanyabishara ndogondogo waliokuwa wamekusudiwa kupewa hawana uwezo wa kulipa fedha ili NSSF warudishe mtaji wao pamoja na riba.

Kwa mujibu wa Fuime, ujenzi wa jengo hilo ulifanyika bila kufanyika utafiti wa kina kubaini aina ya jengo lililotakiwa kujengwa pamoja na eneo lilipotakiwa kuwekwa.

Fuime alisema kuwa kutokana na mambo hayo kutozingatiwa, ndiyo maana NSSF inacheleweshwa kulipwa deni lake na kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa shirika hilo kuchelewa kupata fedha hizo.

“Mmachinga anatakiwa kujengewa jengo la kawaida ambalo siyo ghorofa na kama likiwa ghorofa basi iwe ghorofa moja, lakini sio kama lile jengo la sasa la Machinga Complex ambalo lina ghorofa zaidi ya mbili,” alisema Fuime.

Aidha, Fuime aliliambia NIPASHE kuwa jengo la aina ile lilitakiwa kuweka soko la wamachinga pamoja na kuwa katika kituo cha daladala ili kuvutia wateja.

Fuime alikiri kuwa siasa ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kukwamisha juhudi za watalaamu wanaotaka kubuni njia mbadala za kuwavuta wamachinga wengi ili waingie katika jengo hilo na kufanya biashara.

“Mtalaamu akisema hivi anakuja mwanasiasa anasema acheni watu wangu msiwaguse kwa hiyo mnajikuta mnashindwa kufanikisha miradi mbalimbali inayobuniwa kitalaamu,” alisema.

Aidha, alisema wamachinga waliopewa vizimba katika jengo hilo wengi wao hawakustahili na kwamba waliostahili hawakupata fursa hiyo.

Alifafanua kuwa utaratibu uliotumika kuwaingiza wamachinga hao ni kuwatumia viongozi vya vyama vya wafanyabishara hao na kwamba taratibu kadhaa zilikiukwa.

“Kutokana na makosa hayo yote niliyosema, ni vigumu jengo la Machinga Complex kutengeneza faida hata kama lingekuwepo miaka mingapi kwa kuwa wapangaji wake ambao ni wafanyabiasha ndogo ndogo hawana uwezo wa kulipa mapato ya kutosha,” alisema.

MAONI YA WAMACHINGA
Baadhi ya wafanyabiashara ndogondogo waliozungumza na NIPASHE walisema wakati ujenzi wa jengo hilo unaanza waliamini watapata sehemu nzuri ya kufanyia biashara zao, lakini bahati mbaya eneo hilo limekuwa halilipi kwa kuwa hakuna wateja.

Said Haule, alisema watu waliopewa vizimba vya kufanyia biashara siyo wenzao kwa kuwa walichukuliwa watu wengine na kugawiwa huku wao wakibakia katika soko la Karume.

Haule alisema hakuna mmachinga mwenye mtaji mdogo wa mashati matano ambaye anahitaji kuwa mpangaji katika ghorofa kama lile la Machinga Complex.

John Mwakyoma alisema wamachinga wengi waliokuwa wamelengwa kufanya biashara katika jengo hilo wameachwa nje.

Alisema mbali ya kuachwa nje na kukosa nafasi katika jengo hilo, lakini pia wamachinga waliopewa vizimba wameshindwa kufanya biashara vizuri kwa kuwa ni vidogo pamoja na eneo hilo kutokuwa na wateja.
Mkopo wa NSSF kwa ajili ya Machinga Complex ni moja ya mikopo iliyotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2010/11 kuwa ya utatanishi inayoweza kusababisha fedha za wanachama kupotea.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment