Muktasari:
Ana haki pia ya kuwa na uamuzi wa kuchagua mfuko wa kujiunga ingawa kwa sheria ya sasa ni uamuzi wa mwajiriwa mwenyewe kwa wale wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza.
Mfanyakazi ana haki ya kupata elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta rasmi na isiyo rasmi kabla ya uandikishwaji kufanyika.
Mwajiriwa akishaandikishwa anapaswa kupata kadi. Kadi ni mali ya mwajiriwa siyo ya Mwajiri na mwajiri haruhusiwi kutunza kadi ya mwanachama. Anayeruhusiwa kutunza kadi ya uanachama ni mfanyakazi mwenyewe. Pale inapotokea mabadiliko yoyote kuhusu taarifa za mwajiriwa au mwajiri, inakuwa ni wajibu wa mwajiri kutoa taarifa kwa mfuko wa hifadhi ya jamii husika ndani ya siku 30 ya mabadiliko hayo.
Mfuko wa hifadhi ya jamii una wajibu wa kuandikisha wanachama, kukusanya michango kutoka kwa wanachama, kuwekeza michango ya wanachama na kulipa mafao kwa wanachama.
Mfuko wa hifadhi ya jamii una wajibu wa kuwaelimisha wanachama na waajiri juu ya mahitaji yote ya mfuko, na kuwaonyesha jinsi ya kujaza fomu mbalimbali.
Mfuko una wajibu wa kuelimisha wanachama juu ya mafao wanayotakiwa kupata kutoka kwenye mifuko hiyo.
Kwa upande mwingine mfuko una wajibu wa kuweka uhusiano na wanachama na pale wanachama wanapogundua kuwa waajiri wao hawajapeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, wanatakiwa kutoa taarifa kwenye mifuko.
Mfanyakazi akitoa taarifa ya kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa itunzwe kama siri kwa ajili ya kumlinda mfanyakazi na taarifa inapotolewa kazi hufanyika mapema ili kurekebisha matatizo ya mchangiaji.
Ni wajibu wa waajiri na wafanyakazi kutoa hizo taarifa mapema. Wasingojee mpaka waache kazi au waachishwe kazi. Kwa kufanya hivyo, wakati mwingine inakuwa ni vigumu kutatua matatizo yanayo mkabili, wakati yuko nje ya ajira.
Pia, ni wajibu wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuchukua hatua za kisheria mapema kwa waajiri ambao hawataki kupeleka michango kwa wakati.
Vilevile mwajiri atachukuliwa hatua pale anapofanya makusudi kutowaandikisha wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Wafanyakazi pia wana wajibu wa kuhakikisha kuwa michango yao iliyokatwa na waajiri iko sahihi na pale wanapoona ya kuwa wana wasiwasi na waajiri juu ya michango yao iliyokatwa, wanatakiwa kutoa taarifa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Vilevile, ni haki ya mfanyakazi, yaani mwanachama, kupata taarifa ya michango yake anayokatwa kila mwezi.
Waajiri pia wana wajibu wa kutunza kumbukumbu zote za malipo ili kuwezesha mifuko ya hifadhi ya jamii, inapofanya ukaguzi iwe rahisi kupata kumbukumbu hizo.
Mwajiri yeyote anawajibika kujiandikisha katika shirika kama mlipa michango na kupewa namba ya uandikishaji mara tu anapoanza shughuli zake.
Mwajiri yeyote awajibike kuwaandikisha wafanyakazi wote alio nao na kupewa namba za uanachama.
Mwanachama ana haki ya kupewa kitambulisho cha uanachama ambacho kinatumika kwa ajili ya kupata mafao na huduma yoyote nyingine kutoka katika mfuko wowote aliojiandikisha nao.
Lengo kubwa la msimamizi na mdhibiti wa mifuko pensheni ya hifadhi ya jamii iwe ni kumhakikishia mwanachama usalama wa kupata pensheni.
Wajibu wa mifuko ni kuhakikisha ya kuwa inawashirikisha wadau wake wote wakuu hasa waajiri, serikali, wanachama na familia zao katika mpango mzima wa uchangiaji. Hivyo, uwakilishi wao lazima uwemo ndani ya utawala wa mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii mara kwa mara.
Vilevile inatambulika kuwa hata Serikali ina kazi kubwa juu ya mifuko hii ya hifadhi ya jamii hasa kwa kuangalia na kusimamia kiwango cha kinga juu ya majanga yanayoikumba jamii.
Serikali ndiyo mdhamini mkuu wa mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii. Serikali kuwa mdhamini ina maana ya kuwa mfuko wowote ukifilisika ndiyo itakayowajibika kuwalipa wanachama na wategemezi wao.
Tatizo hapa ni utekelezaji kama vile Serikali au Mwajiri kutowajibika ipasavyo kulipa michango ya pensheni kwa mujibu wa sheria.
Christian Gaya ni mwanzilishi wa kituo cha HakiPensheni Tanzania pia ni mshauri wa masuala ya pensheni. [email protected] au 0655131341
No comments:
Post a Comment