Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo
By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:47 PM Apr 09 202SAKATA la kikokotoo cha mafao ya wastaafu limeibuka tena bungeni, baadhi ya wabunge wakinyooshea kidole serikali kwamba ni kiini cha tatizo hilo.
Wamesema kikokotoo kipya kimeibua madhara makubwa kwa wastaafu, wakitaka kamati iundwe ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2024/25, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema ni nia ya serikali kutaka suala la kikokotoo kufanyiwa kazi, hivyo ni jukumu la Bunge kuanza mchakato wake mapema iwezekanavyo.
Amesema Mei 202, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa ahadi ya kushirikiana na mihimili mitatu kulifanyia kazi suala hilo, hivyo Rais yuko tayari kuona mabadiliko ya kikokotoo kwa maslahi ya wastaafu.
“Nimepitia kanuni mbalimbali kama vile hii ya mwezi Mei 2022 ya Agosti 12, 2018, kanuni ya SCRA 2017 na 2018 pia na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge 2017 pamoja na maoni ya Kambi ya Upinzani ya 2017.
“Kikokotoo kilichokuwapo hadi mwaka 2014 kilikuwa ni kikokotoo kizuri na ndicho Watanzania wengi wanakitaka, chenyewe kilikuwa kimechukua asilimia 50 ambacho kilionesha miaka ya kuishi baada ya kustaafu kuwa ni 15 na nusu, pia kilichukua mshahara wa mwisho wa mfanyakazi ambao mara nyingi huwa ni mkubwa," amesema Gambo.
Vilevile, amesema kwa kikokotoo kimepunguza kutoka 1/540 hadi 1/580 pia wamechukua wastani wa miaka 10, wakitafuta miaka mitatu iliyo bora ambapo kwa kawaida lazima mshahara utapungua na kuathiri mafao, pia miaka ya kuishi imepunguzwa hadi 12, kitu alichodai si sahihi.
“Nimechukua mfano, sampuli ya mishahara na nimefanya mahesabu kwa mtumishi ambaye anastaafu akiwa na mshahara Sh. 800,000. Kwa kikokotoo cha kabla ya Julai 2014 katika mfuko wa LAPF na PSPF alikuwa anapata Sh. 57,466,666 na kwa kikokotoo cha sasa anapata Sh. 28,675,862 tofauti ya Sh. milioni 29,190,804. Kwa mwezi atapata Sh. 401,000 kwa kikokotoo cha zamani na cha sasa atapata 388,137,” amesema Gambo.
Amesema katika hali ya kawaida kwenye kikokotoo hicho yamefanyika makosa makubwa kwa kuwa sheria inayoanzishwa inatakiwa kuanzia pale tu ilipotungwa. Kwahiyo, wote ambao sheria hiyo ilikuwakuta walitakiwa kulipwa kwa kikokotoo cha zamani na kipya kusubiri wale watakaoanza kazi.
Pia ametaka serikali kurejesha fedha zote ilizochukua katika mifuko ili kuirudishia uhai kama ilivyoshauriwa katika ripoti ya CAG, pia itenge bajeti kwa ajili ya kuinua mifuko hiyo na zitengenezwe kanuni mpya zisizowaadhibu wastaafu.
Mbunge wa Mbulu Mjini, Issay Paulo amesisitiza kurudi katika meza ya mazungumzo na vyama vya wafanyakazi kukipitia upya kikokotoo hicho kwa kuwa katika maeneo yake amekuwa akikutana na wastaafu wengi wanaolia juu ya suala hilo.
KIFO CHA MBUNGE
Katika hatua nyingine Bunge hilo limeahirishwa hadi Aprili 15 mwaka huu kutokana na kifo cha Mbunge wa Kwahani, Ahmed Yahya Abdulwakil (CCM), aliyefariki dunia ghafla jana kwa shinikizo la damu, pia kupisha sikukuu za Idd El Fitir.
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ametoa taarifa hiyo kwa Bunge jana jioni, akisema mbunge huyo alifariki jana na maziko yatafanyika leo kijijini kwao Buyuni, Zanzibar.
“Waheshimiwa wabunge kwa mujibu wa kanuni yetu ya 173 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, kesho (leo) hakutakuwa na kikao cha Bunge ili kutoa fursa kwa wabunge kushiriki maziko, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi... Amina,” amesema na kuongeza:
“Kwa kuwa hatuna uhakika nini kinaweza kutokea na kwa wakati gani mwandamo wa mwezi utakuwa lini, ninaahirisha shughuli za Bunge mpaka siku ya Jumatatu saa 3:00 asubuhi."
No comments:
Post a Comment