“Hapa Tanzania, Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa kipaumbele kwenye suala la kuwezesha jamii kwa kuwainua kiuchumi wanawake na vijana ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Ouagadougou (“Ouagadougou+10”) la Utekelezaji wa Mpango wa Ajira na kutokomeza umaskini ambalo lilipitishwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika Januari 2015 kama Ajenda ya AU ya 2063.
“Ni wakati muafaka mifuko yetu ya jamii kusaidiana na Serikali zetu kuondoa umasikini miongoni mwa watu wetu. Nitoe rai kwa washiriki wa mkutano huu muangalie uwezekano wa kujadili kwa mapana kuhusiana na namna ya mifuko ya hifadhi ya jamii inavyoweza kusaidia kuinua uchumi wa watu wetu na kusaidia kuondoa umaskini hasa kwa wanawake, vijana na wakulima.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema eneo la bima lilishatolewa maelekezo na Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 22, 2021 wakati alipohutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
“Mheshimiwa Rais alielekeza kwamba suala la bima ya kilimo na bima ya afya kwa wote liangaliwe kwa ukaribu zaidi na kuwekewa mfumo mzuri wa kisheria utakaoainisha namna bora ya utekelezaji wake.”
Alisema Serikali iliangalia pia suala la ukingaji wa majanga kwenye maeneo ya mikusanyiko kama vile masoko, shule na maduka na ikaamua kuweka mfumo wa kisheria wa namna ya kuyakinga majanga haya kwa njia ya bima kwa kupitisha Sheria ya Fedha Na. 05 ya Mwaka 2022 itakayosaidia kukinga maeneo yenye mikusanyiko kama vile masoko, vivuko na majengo ya biashara.
“Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania tunaandaa mwongozo wa bima ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuhakikisha kundi hili kubwa linapata uhakika wa uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi hasa kwenye kipindi hiki chenye changamoto kubwa za mabadiliko ya tabia nchi.”
No comments:
Post a Comment