Pages

Wednesday, July 20, 2022

WASTAAFU DODOMA WAMSHUKURU WAZIRI NDALICHAKO KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZAO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba (wapili kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba, akizungumza na mstaafu wakati wa zoezi la kuwasilisha wastaafu wote wa MIFUKO ya NSSF na PSSSF jijini DODOMA Julai 20, 2022.












 *Wenyewe wasema wamepata Waziri msikivu  anayejali wastaafu 

Na MWANDISHI WETU, DODOMA

Baadhi ya wastaafu wa Mifuko ya PSSSF na NSSF wamejitokeza kusikilizwa  kero zao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako ambaye alikutana na wastaafu hao kwa lengo la kusikiliza changamoto.

“Nimeona nitenge muda kusikiliza changamoto walizonazo wastaafu wa NSSF na PSSSF hivyo zile changamoto ambazo tunaweza kuzitatua papo kwa papo tunafanya hivyo na zile ambazo zinahitaji muda tunachukua vielelezo na kuzifanyia kazi,” alisema Profesa Ndalichako. 

Mkutano huo ulifanyika Julai 20, 2022 Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba pamoja na watendaji wa mifuko hiyo na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri Profesa Ndalichako alisema kupitia mkutano huo wataendelea kujifunza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wastaafu hivyo aliwaomba watendaji wa mifuko hiyo kuweka utaratibu wakusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi.

“Ni jukumu na ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali za wananchi wakiwemo wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii,” alisema.

Waziri Profesa Ndalichako alisema lengo la Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuhakikisha wanatoa huduma kwa wastaafu bila usumbufu wowote na kuwahudumia kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Naye, Mzee Ramadhani Abdallah ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Waziri Profesa Ndalichako ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wastaafu hatua ambayo itapunguza changamoto za wastaafu.

“Nashuruku Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumchagua Waziri Ndalichako ambaye ni msikivu, anayejali wazee, anayejali watumishi waliotumikia nchi hii kwa muda mrefu, hili alilolifanya leo ni jambo kubwa na zuri,” alisema Abdallah.

Kwa upande wake, Mstaafu Maria Kapande  alimshukuru Waziri Ndalichako kwa kukutana na wastaafu ambapo changamoto zao zimesikilizwa na zinaenda kupatiwa ufumbuzi .

No comments:

Post a Comment