Pages

Wednesday, July 6, 2022

TANROADS KUKAMILISHA BARABARA YA MZUNGUKO DODOMA KWA WAKATI



 NA MWANDISHI WETU, DODA

WAKALA ya Barabara Tanzania (TANROADS) umesema utahakikisha ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje katika Jiji la Dodoma (Outer Ring Road) yenye urefu wa kilometa 112.3 inakamilika kwa wakati.

TANROADS imesema kwa sasa wakandarasi wanaendelea na kazi ambapo kipande cha kwanza chenye urefu

wa kilometa 52 cha kuanzia Nala-Veyula-Mtumba- Ihumwa, Mkandarasi amefikia asilimia 9.8 na kipande cha pili chenye urefu wa kilometa 60  cha kuanzia Ihumwa (Bandari kavu) – Matumbulu – Nala, Mkandarasi amefikia asilimia 6 na kazi zote zinaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari Mhandisi wa Miradi wa TANROADS Dodoma, Mhandisi Colman Ramadhan alisema ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kugharimu sh.bilion 221 hadi kukamilika kwake.

“Kukamilika kwa barabara hii kutatuwezesha kupunguza changamoto ya msongamano mkubwa wa magari barabarani iliyopo katika Jiji la Dodoma kwa sasa, hasa baada ya serikali kuhamia Dodoma na malori yanayolazimika kukatiza katikati ya Jiji kwenda Iringa, Singida, Morogoro na Arusha

Aliongeza kuwa “ Kwa kasi hii ambayo wakandarasi wanaendelea nayo tuna uhakika kuwa watamaliza kazi kwa wakati ambapo tutahakikisha  hadi kufikia mwisho wa mwaka 2024 mradi huu uwe umekamilika.

Kwa upande wake Afisa Mazingira na Jamii katika Mradi wa huo Ignatus Ngamesha alisema mkandarasi anayejenga mradi huo pia atajenga vituo vya afya vinne katika kata ya Nala,Ihumwa,Veyula na Mtumba.

Alisema pia jamii itanufaika na ujenzi wa visima vya maji pamoja na ajira za muda na za moja kwa moja kwa wakazi wanaosihi jirani na mradi unapotekelezwa.

“Kuna kata inaitwa Mndemu tumetoa mifuko 100 ya simenti,lori mbili za  kupeleka mawe na kifusi kila mwezi  kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Mndemu, pia tunatengeneza barabara katika kijiji cha mndemu ili wananchi waweze kupita kwa urahisi,”alisema.



No comments:

Post a Comment