Pages

Friday, July 22, 2022

MAELFU YA WASTAAFU NSSF, PSSSF JIJINI DAR ES SALAAM WAJITOKEZA KWENYE KIKAO CHA KUTATUA KERO CHINI YA WAZIRI PROFESA NDALICHAKO



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako (katikati) akizungumza na baadhi ya wastaafu wakati wa zoezi la kusikiliza kero walizonazo kwenye jengo la NSSF Mafao House, Ilala jijini Dar es Salaam Julai 22, 2022. Kulia kwa Profesa Ndalichalo ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba, akiangalia moja ya nyaraka za wastaafu zilizowasilishwa kwake.







NA KHALFAN SAID, DAR ES SALAAM

MAELFU ya wastaafu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii NSSF na PSSSF wamejitokeza kwenye mkutano alioitisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako jijini Dar es Salaam ili kusikilizwa na kutatuliwa kero zao.

Profesa Ndalichako ambaye alifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) CPA. Hosea Kashimba, kwa pamoja walitumia siku nzima kusikiliza kero za wastaafu na baadhi kuzipatia ufumbuzi.

“Leo nimetoa fursa kwenu ninyi wastaafu tukutane ili kama kuna mtu ambaye ana changamoto inayohusiana na Mafao yanayolipwa na NSSF au PSSSF apate fursa ya kuelezea changamoto zake.” Alisema.

Alisema amekuwa akipata changamoto mbalimbali za wastaafu na kuzitaja kuwa ni pamoja na zinazotokana na mapunjo zinazopelekea mstaafu kupata Malipo ya Mkupuo pungufu na Pensheni nayo inakuwa kidogo kuliko inavyotakiwa, Waajiri kutowasilisha michango, lakini pia uelewa tu.

“Ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwetu   sisi wasaidizi wake ni lazima tuhakikishe tunatatua kero ambazo ziko katika maeneo yetu,” alisema na kuongeza.. na mimi Mheshimiwa Rais amenipa dhamana ya kuongoza kundi ambalo analiheshimu sana yule ni mama anawaheshimu wazee na hataki kusikia wazee ambao wamelitumikia taifa hili kwa weledi wametufikisha hapa tulipofika wakihangaika.” Alisema.

Alisema ni kweli pia zipo changamoto za Mashirika kutowasilisha michango kwa wakati, na baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri na Mashirika ya Umma.

“Tunategemea wiki ijayo kupata orodha yote ya Taasisi, Halmashauri, Majiji ambayo hayawasilishi michango, wanapaswa kujua ili mtu alipwe mafao yake ni lazima waajiri wote wawasilishe michango kwa wakati.” Alibainisha.

“Kikao hiki kitakuwa endelevu na mimi leo sitoki hapa, nitakaa hapa hata kama saa sita usiku niwasikilize wote mmoja baada ya mwingine, kwa kushirikiana na watendaji wa Mifuko yote miwili watatatua changamoto zenu hapa.” Alitoa hakikisho.

Profesa Ndalichako alianza zoezi la kusikiliza kero majira ya saa 3 asubuhi na kuendelea hadi saa 2;45 usiku.

Kwa upande wao Wastaafu wamepongeza uamuzi huo wa Waziri kukutana nao kwani ni nafasi nzuri kwao kuwasilisha kero zinazowakabili.

“Kwakweli kitendo hiki kinachotokea hapa ambapo Waziri wa Kazi ametuita wastaafu ni kitu cha kutufariji sana na kimepokelewa na wengi, tunamshukuru Rais wetu mama Samia kwa upendo alio nao na maelekezo anayoyatoa wka watendaji wake.” Alisema Bi.Martha Adams Lyimo ambaye alikuwa mtumishi wa Wizara ya Afya.

“Mtu akisikilizwa inasaidia kupunguza kama sio kuondoa matatizo ambayo yanajitokeza kwa sababu yawezekana matatizo mengine yanatokana na uelewa tu kwa hiyo jambo hili nimelifurahia sana la Mheshimiwa Waziri kukutana na wastaafu.” Alisema Mstaafu mwingine Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Jamal Rwambo.

No comments:

Post a Comment