NA MWANDISHI WETU, MTWARA.
Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Abdallah Malela ametoa wito kwa Waajiri Mkoani humo kutekeleza wajibu wa kisheria unaowataka kuwasilisha michango stahiki ya wafanyakazi wao kwa wakati kwenye
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).Bw. Malela ameyasema hayo wakati akifungua semina ya Mafunzo kwa Waajiri iliyoandaliwa na NSSF na kufanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu mkoani Mtwara.
“Kwa kufanya hivyo mtakuwa mmerahisisha ulipwaji wa Mafao na stahiki zingine kwa wakati na kuwaepusha na usumbufu na msongo wa mawazo”. Alisema.
Akifafanua zaidi alisema ofisi ya Mkuu wa mkoa imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusiana na baadhi ya waajiri kutotimiza wajibu huo wa kisheria wa kuwasilisha michango ya kila mwezi.
Bw. Malela aliweka wazi kwamba mwajiri anapowasiliaha michango ya wafanyakazi wake kwa wakati NSSF, inaongeza ari ya utendaji kazi kwa mwanachama husika kwa vile atakuwa na uhakika wa kesho yake kwa kupata Pensheni na Mafao mazuri baada ya kustaafu.
“Lazima tufahamu kwamba mfanyakazi anayestaafu akiwa na uhakika wa Pensheni hatoweza kuhangaika ikiwa michango yake iliwasilishwa kwa wakati NSSF”. Alisisitiza.
Bw. Malela ameipongeza NSSF kwa kuandaa semina hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo kwa kuwapatia elimu waajiri mkoani Mtwara kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria lakinia pia kufahamu huduma zitolewazo na Mfuko.
“Napenda kuwashukuru viongozi wa NSSF kwa kuandaa semina hii kwa kuwa imekuwa na manufaa makubwa kwa waajiri kwa kuwakunbusha wajibu wao kwa wafanyakazi.” Alisema.
Aidha alitoa wito kwa NSSF kuendelea na jitihada zake za kuandikisha wanachama wapya wale walio kwenye ajira rasmi na ambao wako katika sekta isiyo rasmi mkoani humo.
Kwa upande wake Meneja wa NSSF mkoa wa Mtwara Bw. Rebule Maira alisema lengo la NSSF mkoa wa Mtwara kuandaa semina hiyo ni kuwaelimisha waajiri hao kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mfuko lakini pia kujenga uhusiano mwema kati ya Mfuko na Waajiri hao.
Bw. Maira pia alisema kitendo cha mwajiri kutowasilisha Michango stahiki na kwa wakati huwasababishia usumbufu mkubwa wanachama unapowadia wakati wa kupata stahili zao za Mafao.
Alisema takwimu zinaonyesha mkoa wa Mtwara una jumla ya waajiri 467 Kati yao 251 ndio wanaotekeleza wajibu wa kisheria wa kuwasilisha michango stahiki huku waajiri 87 hawawasilishi michango yao ipasavyo na hivyo kusababisha Deni la zaidi ya bilioni 2.9 ambazo wanadaiwa waajiri hao.
No comments:
Post a Comment